Utata kuhusu mauaji ya mgonjwa kwa kukatwa koo KNH wazidi
KITENDAWILI kuhusu mauaji ya mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kilizidi kuongezeka Jumanne baada ya wafanyikazi na maafisa wa usalama kuwaambia wachunguzi kwamba hakukuwa na vurugu katika hospitali hiyo usiku ambao mwanamume huyo aliuawa.
Hata hivyo, ushahidi huu wa hivi punde unakinzana na matokeo ya uchunguzi wa awali ya afisa wa DCI wa Kilimani ambaye aliwahoji wagonjwa kadhaa kuhusu matukio ya usiku wa Februari 6 kabla ya wachunguzi wa mauaji kuanza..
Mgonjwa mmoja aliwaambia wachunguzi kwamba kulikuwa na vurugu katika wodi iliyokuwa karibu saa sita usiku. Hata hivyo, hakuna mgonjwa hata mmoja katika wodi hiyo aliyemuona mshambuliaji huyo. Gilbert Kinyua alipatikana amefariki katika wodi hiyo asubuhi ya Februari 7.
Wachunguzi wa mauaji wamerekodi taarifa kutoka kwa watu watano wanaoamini kuwa wanaweza kuwa na habari muhimu ambazo zinaweza kusaidia kufichua muuaji wa Gilbert Kinyua.
Miongoni mwa waliorekodi taarifa na polisi ni pamoja na walinzi na wafanyakazi waliokuwa zamu usiku wa mauaji hayo.
Afisa anayefahamu kuhusu uchunguzi huo jana alisema walinzi waliokuwa zamu usiku wa Alhamisi iliyopita walisema waliarifiwa kuhusu mauaji hayo na muuguzi ambaye alikuwa akikagua wagonjwa asubuhi iliyofuata.
Wachunguzi hao pia wamerekodi taarifa kutoka kwa mke wa Kinyua, Susan Wanjiku.
Wachunguzi wa mauaji waliitwa Ijumaa kusaidia kutatua mauaji hayo ya kutatanisha ya Bw Kinyua.
Koo la Bw Kinyua lilikatwa na mtu au watu wasiojulikana alipokuwa amelazwa hospitalini.
Hata hivyo, wachunguzi hao bado hawajamhoji mgonjwa wa kiume aliyekuwa chumba kimoja cha wadi na marehemu.
Daktari wa magonjwa ya akili anayemhudumia mgonjwa huyo wa kiume, anayesemekana kupata nafuu kutokana na maradhi ya akili, hajawaruhusu wapelelezi kuzungumza naye.
Polisi wanaamini kuwa mgonjwa huyo anaweza kutoa maelezo muhimu ambayo yanaweza kusaidia kufichua muuaji wa Bw Kinyua.
Siku ya Ijumaa wiki jana, wachunguzi wa eneo la uhalifu walitembelea hospitali hiyo na kukagua picha za CCTV za usiku uliopita lakini bado hawajapata sababu zozote za kuaminika kuhusu mauaji hayo, chanzo kinachofahamu kuhusu uchunguzi kilisema Jumamosi.
Kisu ambacho kilikuwa kimeangushwa kwenye paa la orofa ya kwanza ya hospitali hiyo na ambacho inaaminika kuwa silaha ya mauaji ni miongoni mwa vitu ambavyo wachunguzi wamekusanya kwa uchunguzi wa alama za vidole.
Bw Kinyua alilazwa katika hospitali hiyo mnamo Desemba 11, 2024.
Alipatikana amefariki katika kitanda chake cha Wodi 7B huko KNH Ijumaa asubuhi.
Mnamo Ijumaa, KNH ilithibitisha kisa hicho, na kusema hospitali hiyo ilikuwa ikishirikiana na polisi kutegua mauaji hayo.