• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Utupaji holela wa taka wavuka mipaka Githurai

Utupaji holela wa taka wavuka mipaka Githurai

Na SAMMY WAWERU

BW Francis Munene alipohamia Githurai 44, mtaa ulioko kiungani mwa jiji la Nairobi, hata ingawa haukuwa safi vile alifurahia kuhusishwa nao.

Unasifiwa kuwa na nyumba za kukodi za bei nafuu, wengi wenye mapato ya chini na kadri wakijisitiri humo.

Raslimali kama vile maji eneo hilo si hoja, ukilinganishwa na mitaa mingine kaunti ya Nairobi ambayo licha ya ubora wake suala la maji limesalia kuwa balaa bin belua.

Miaka mitano baadaye, Bw Munene ambaye ni mhudumu wa tuktuk kati ya Githurai 45, Githurai 44 na Zimmerman, hatamani kamwe kuhusishwa na mtaa huo wa Githurai 44.

Sababu kuu ikiwa kukithiri kwa kiwango cha chafu.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mkazi huyo amelalama kuhusu utupaji holela wa taka, suala ambalo limegeuza nyingi ya sehemu kuwa kiini cha uvundo.

Isitoshe, taka zinazojumuisha mifuko ya karatasi za plastiki zilizopigwa marufuku 2017, mikebe na sodo, zinahatarisha usalama wa mazingira.

Si salama kamwe kulingana na Munene, ambaye kila baada ya dakika kadha au saa hupitia humo akisafirisha abiria kwa tuktuk.

Taswira ya eneo ambako taka hutupwa bila utaratibu maalum. Picha/ Sammy Waweru

Katika mojawapo ya njia inayounganisha Githurai 44 na Zimmerman, mrundiko wa taka unaogofya. Taka za kila aina, zimesambaa kiasi cha kufika barabarani, ambayo awali ilikuwa ikipitika.

“Haipaswi kuwa jaa,” Munene akasema akionekana kujawa na ghadhabu.

Mita kama 500 hivi, kipo kituo cha chifu ambaye ana maafisa tawala wa askari (AP).

“Uchafuzi huu wote hufanyika serikali ikitazama tu,” mkazi aliyeomba kutochapisha jina lake akalalamika.

Kulingana na wenyeji eneo hilo lililogeuzwa jaa, linaweza kutwaliwa liwe la manufaa ikiwa kero hilo litaangaziwa. Badala yake, wanapendekeza lifanywe soko, kujenga maduka wakazi wawekeze kwenye biashara.

“Kwa sasa hakuna linayefaa, linachangia kuharibu mazingira,” asema Bw Munene.

Anaongeza: “Likisafishwa, maduka yajengwe au hata vibanda, litabuni nafasi za ajira kwa watakaoweka kazi.” Ni kauli inayopigwa jeki na wengi wa wakazi tuliozungumza nao.

Msimu huu wa mvua ya gharika, limegeuka kuwa makazi ya wadudu hatari kama vile mbu. Mdudu huyo ni msambazaji wa ugonjwa hatari wa Malaria.

Ugonjwa wa Kipindupindu unasababishwa na uchafu wa mazingira ya aina hiyo. Eneo hilo lina majengo ya makazi ya kukodi.

Mbali na kuwa kiini cha magonjwa, wenyeji wanahisi ni torokeo la wezi na wahuni. “Kwa mpita njia, akikutana na wezi wampige ngeta na kumuibia, wamtishie kumrusha humo ataweza kujiokoa kweli?” anashangaa Bw Munene.

Kwa kutazama jaa hilo kwa umakinifu, linaonekana kuwa shimo, ambalo linaongeza hatari si tu kwa wapita njia ila kwa watoto wa wenyeji.

Halmashauri ya kitaifa ya mazingira Nema, pamoja na wizara husika ya mazingira serikali ya Kaunti ya Nairobi na ile kuu, ndizo asasi husika, na zinaendelea kufumbia macho uchafuzi unaoendelea hilo.

Katika kila jengo la kupangisha wamiliki wanapaswa kuwa na mpangilio maalum wa ukusanyaji taka, ambapo wapangaji hutozwa ada fulani. Taka hizo hazipaswi kutupwa kiholela, ikizingatiwa kuwa tumeona baadhi ya wabunifu wakizigeuza kuwa bidhaa za ujenzi.

Serikali ya kaunti na asasi husika ziwajibikie usafi na usalama wa mazingira.

Kinachoshuhudiwa Githurai 44 ni taswira tu ya mengi ya maeneo Kaunti ya Nairobi, ambayo mazingira yake hayakaliki.

You can share this post!

AKILIMALI: Mkulima anavyofaidi kutokana na ukuzaji na...

Kifo kingine feri mwanamume akidaiwa kutumbukiza gari lake

adminleo