Uuzaji wa sidiria umempa riziki kwa miaka mitano
Na SAMMY WAWERU
Sekta ya Juakali inawakilisha zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini, hivyo basi inaorodheshwa kati ya sekta muhimu na zinazochangia kwa kiasi kikuu ukuaji wa uchumi.
Inajumuisha wafanyabiashara wa kiwango cha chini na kile cha kadri, ndio SMEs.
Wanaochangia kuimarika kwa uchumi katika sekta ya Juakali wakitajwa, Eunice Njoki hatakosa kujumuishwa kwenye listi.
Ni mfanyabiashara muuzaji wa mavazi ya jinsia ya kike eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu. Eunice ana uzoefu wa miaka saba mfululizo katika uuzaji wa sidiria.
“Niliingilia uuzaji wa mavazi haya mnamo 2013,” akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano.
Mfanyabiashara huyu ambaye ni mama wa mtoto mmoja, mvulana mwenye umri wa miaka tisa, anasema kuzamia uuzaji wa sidiria ni hatua asiyojutia kamwe kwani alikuwa amehangaika kwa muda katika kazi za kuajiriwa.
Baada ya kuhitimu kidato cha nne 2008, Eunice anasema kwa sababu ya ukosefu wa fedha hakuweza kujiunga na taasisi ya elimu ya juu. Alitamani kusomea kozi ya ualimu.
Licha ya changamoto hizo, alitafuta vibarua vya hapa na pale jijini Nairobi ili kujiendeleza kimaisha. Eunice anadokeza kwamba kati ya 2009 na 2012 aliajiriwa kuuza bidhaa kama vile nguo na vifaa vya kieletroniki jijini, katika maduka tofauti jijini.
“Kazi ya kuajiriwa ina presha na msukumo, ikizingatiwa kuwa lazima iraukiwe asubuhi na mapema. Hata hivyo nilivumilia,” anaeleza.
Alikuwa mfanyakazi aliyejipanga polepole, kwa kuweka akiba, licha ya kipato cha chini anachosema alijikuna kichwa kugawanya kukithi mahitaji ya kimsingi, ikiwemo kulipa kodi ya nyumba na chakula.
Mama huyu anasema kufikia mwanzoni mwa 2013 alikuwa ameweka kibindoni akiba ya Sh30, 000. “Nilikodi kibanda nilichokuwa nikilipia Sh3, 000 kila mwezi. Nilikuwa nimefanya utafiti wa kutosha na kubaini uuzaji wa sidiria hukuwa na watu wengi katika masoko mbalimbali eneo la Ruiru,” Eunice anasema.
Utangulizi hata hivyo haukuwa rahisi, hasa kuhamasisha wateja ambao ni jinsia ya kike kwamba anauza sidiria.
Mfanyabiashara huyu anasema mwaka wa kwanza alijishughulisha kutafuta wateja, wakati mwingine akichuuza mavazi hayo na kuelekeza wateja anakouzia.
Mwaka 2015 alianza kufurahia matunda ya biashara ya uuzaji wa sidiria, akikumbuka kuna siku alifanya mauzo yasiyopungua mavazi 200.
Huyanunua katika soko maarufu la Gikomba, jijini Nairobi. Bei ya sidiria anazouza ni kati ya Sh50 – 150.
Tangu Kenya ithibitishe kisa cha kwanza cha Covid – 19, sawa na wafanyabiashara wengine, Eunice pia anasema biashara yake imeathirika. “Wafanyabiashara wa kiwango cha chini ndio tumeathirika pakubwa na janga la corona. Hata hivyo, sikosi mapato ya riziki, kukithi familia yangu mahitaji ya kimsingi na pia kurejesha stoki ya kazi,” anaelezea.
Sekta mbalimbali, ikiwemo ya biashara, zinalia kuhangaishwa na athari za virusi vya corona, ambavyo kwa sasa vipo katika kila kona ya ulimwengu.
“Awali, nilikuwa nikihudumia zaidi ya wateja 80 kwa siku. Kufuatia athari za janga la corona, wamepungua hadi chini ya 30,” Samson Gitau, mhudumu wa M – Pesa Ruiru, akasema katika mahojiano.
Licha ya serikali katika makadirio ya bajeti mwaka wa fedha 2020/2021 kudai kutengea SMEs mgao wa fedha ili kuwanusuru, Eunice anasema ingekuwa afueni iwapo kodi ya ushuru unaotozwa bidhaa nyingi zinazouzwa na wafanyabiashara wa kiwango cha chini ingepunguzwa zaidi.
“Wakati mwingine hukosa kupata sidiria sokoni. Ni changamoto ambazo pia huathiriki wauzaji wa bidhaa zingine. Afueni ingekuwa kupunguziwa ushuru zaidi,” anahimiza serikali.