Makala

Uvamizi hospitali Kitengela Saba Saba ulivyolazimu wajawazito kujificha chini ya vitanda

Na FRIDAH OKACHI July 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UVAMUZI uliofanywa na vijana Julai 7, 2025 katika Hospitali ya Kaunti ndogo ya Kitengela, uliwatia uwoga wanawake wajawazito, wengi wao wakijificha kwenye vyoo na wengine kuingia chini ya vitanda.

Bi Winnie Kagio, 28, alisema wakati wa uvamizi huo, alikuwa miongoni mwa wanawake wawili waliokuwa wakijifungua kwa wakati huo ambapo kundi la vijana hao liliingia kwenye chumba chao.

Bi Kagio alisema vijana hao waliingia wakiwa na hasira wakitaka mwenzao ambaye alikuwa ameumia kushughulikiwa bila kujali chumba hicho hakiruhusiwi watu wengi.

“Zile kelele ziliniogopesha mno na bado nina wasiwasi maana sijui iwapo watarudi leo. Walipoingia nilipata mwanya wa kutorokea na kwenda kujifungia kwenye choo,” alieleza Bi Kagio.

Bi Peninnah Nduko, 34, aliingiwa na wasiwasi ambao uliosababisha kuchukua malaika wake na kuingia chini ya kitanda.

“Kuna mwenzetu ambaye alikuwa amejifungua, tulimsaidia kwa kuchukua mwanawe na kuingia chini ya kitanda,” alisimulia Bi Nduko.

Kulingana na muunguzi katika chumba cha uzazi Bi Harriet Maorwe, chumba cha wanaweke waliokuwa wanasubiri kujifungua walikuwa tisa, huku wawili wakiwa kwenye hatua ya mwisho ya kupokea watoto wao.

“Tumelazimika kutoa huduma za msongo wa mawazo kwa wanawake hao. Kilichonisikitisha waliingia hadi sehemu ambayo wawili walikuwa wanajifungua. Mmoja wao alijifungua na kushindwa kupokea mtoto wake. Nesi mmoja alimsaidia maana alikuwa anataka kumwangusha kwa uwoga,” alisema Bi Maorwe.

Vurumai hiyo, ilipelekea madaktari na wauguzi kujawa na hofu tele, wengi wao wakikimbilia usalama kwa kujificha kwenye vyumba tofauti na kuvalia mavazi ya wagonjwa ili wasiumizwe.

Tabibu wa ugonjwa wa ngozi Bw Tatio San alisema vijana hao walifika na mwili wa Brian Kimutai wakitaka hospitali hiyo kufanya upasuaji wa haraka kwa kutoa risasi kama ushahidi.

Amri hiyo ikiwa tatanishi kwa kuwa hawakuwa na rekodi zozote kutoka kwa serikali na hivyo ilihitaji chumba cha maiti kuchukua mwili kwanza, hali iliyosababisha hasira kwa vijana hao.

“Vijana hao walikuwa walevi, walianza kutupa mawe kwenye madirisha na kuvunja vifaa vya hospitali. Mmoja wao aligonga kioo kwa kutumia mkono na kupata jeraha mbaya,” alisema Bw San.

Ajali hiyo ilichangia vijana hao kufika katika chumba cha upasuaji alipokuwa mwanamke mmoja ambaye alikuwa akifanyiwa upasuaji wa kupata mtoto (C- Section).

“Walisukuma mlango na kupata madaktari wawili wa upasuaji. Walitaka mgonjwa wao kuhudumiwa. Hivyo daktari mmoja aliondoka kwenye upasuaji huo na kuanza kumshughulikia na yule mwingine akiendelea kuokoa maisha ya mama na mtoto ambao hali yao ni shwari,” alieleza Bw San.

Alikemea hatua ya vijana hao kuvamia vyumba hivyo ambavo huhitaji usafi wa hali ya juu.

Mwenyekiti wa Muungano wa Matabibu nchini Bw Peter Wachira alighadhabishwa na hali hiyo, huku akipendekeza wakati wa maandamano, maafisa wa polisi kupelekwa kwenye hospitali ili kutoa ulinzi kwa wanachama wake.