Makala

Uvumbuzi wa chumba cha kupiga nduru sekunde 12 kuondoa msongo wa mawazo

Na FRIDAH OKACHI September 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UVUMBUZI wa chumba cha kupiga mayowe na wataalum wa teknolojia kutoka Shirika la Thalia, unatoa fursa ya kupunguza mawazo kwa mhusika akitumia sekunde kumi na mbili pekee.

Mwanasaikolojia Milly Ann Anyango anasema kuwa wakati wa kupiga mayowe ndani ya chumba hicho, mwathiriwa hupata utulivu na kupata nguvu mpya.

“Saa zingine kwa maisha tunapitia maisha magumu, vitu vigumu au unaweza kuwa umefiwa. Chumba hicho kinakusaidia uweze kutoa hisia ambazo uko nazo. Yule anayeingia katika chumba hicho huelekezwa na kufahamishwa ni sehemu salama. Hapo ndani una haki ya kupiga nduru kwa sekunde 12 kisha unatoka ukiwa na nguvu mpya na upo salama,” alieleza Bi Anyango.

Mwanasaikolojia huyo, alisema upigaji wa mayowe ni njia ya kimwili ambayo huwezesha mwili au mawazo yako kuwa huru kwa asilimia 65.

“Anayeingia anatoka akiwa ametulia pamoja na kuwa na nguvu mpya. Zoezi la kupiga mayowe lina ufanisi wake,” aliongeza.

Alithibitisha usalama wa chumba hicho ikilinganishwa na nyumbani ambapo kama mzazi hawezi kupata sehemu ya siri ya kupiga mayowe. Alisema tofauti na nyumbani kuna usiri mwingi ambao hauhitajiki kujulikana au kuulizwa sababu za kupiga nduru na walio karibu nawe.

“Hapa hautapata unyanyapaa wowote au kuulizwa na watu fulani mbona unapiga kelele au unasumbuliwa na nini? Ni wewe pekee yako. Unajua wakati unapiga nduru ukiwa nyumbani watoto, wanafamilia au waliokaribu nawe watakuuliza iwapo upo sawa. Wengine watakuorodhesha kuwa una wazimu,” alidokeza Bi Anyango.

Mwanasaikolojia Milly Ann Anyango akifafanua jinsi mawazo hupunguzwa kwa sekunde 12. Picha|Fridah Okachi

Hata hivyo, chumba hicho hutumiwa na watu wa tabaka mbalimbali. Bi Anyango alisema zoezi hilo ambalo linapunguza mawazo halichagui umri.

Bi Joy Wangari Ndiragu, 26, ni miongoni mwa wale ambao wametumia chumba hicho na kupata afueni. Pia alidai kuwa mfumo ambao umetumika pale ni wa akili unde ambao unamwezesha mwathiriwa kupata ripoti yake ya moja kwa moja.

“Kuna akili uunde pale ambayo inakupa kiwango cha jinsi ulivyopiga mayowe, kiwango cha mawazo ambayo uko nayo na jinsi umeweza kunufaika. Wakati niliingia sikujua nini kitanifanyikia, kwa hivyo niliingia ili kujaribu na nikashtuka kuona mawazo yaliyokuwa yakinisumbua yamepungua. Kwanza mle ndani nilipiga nduru mara mbili…wakati nilitoka nikahisi mawazo yangu yamepungua,” alisema Bi Ndiragu.

Pia, wasanii hapa nchini wahimizwa kupunguza msongo wa mawazo ambayo wanayapata kupitia kazi zao.

Bw Josephat Muchesia Mutsotso almaarufu Mchungaji ambaye ni mcheshi aliyepata fursa ya kuingia kwenye chumba hicho, alisifia uvumbuzi huo licha ya mawazo yake kupungua kwa asilimia kidogo.

“Ni mahali pazuri pa kupunguza msongo wa mawazo ila haikunitolea kwa asilimia mia moja. Pia, ujue unapoendelea kuingia pale inasaidia polepole kupunguza ila kwako binafsi ni vyema kupanga muda mwafaka,” alisema mcheshi Mutsotso.

“Unajua hapa Kenya, kuchekesha Mkenya sio kitu cha kawaida ama sio rahisi. Kwa hivyo Wakenya ama waundaji maudhui humu nchini, ningependa kuwahimiza waweze kutumia chombo kama kile ambapo ukiwa na yale mawazo yaondolewe. Kabla ya sisi kuwa kwenye jukwaa, pale nyuma unaambiwa toa wasiwasi, na chumba kile kitakufaa zaidi,” alihimiza mcheshi huyo.

Joy Wangari Ndiragu ambaye aliingia ndani na kunufaika baada ya kupiga mayowe. Picha|Fridah Okachi

Bw Evans Jiboda Malmas, 32, ni miongoni mwa wabunifu waliotumia teknolojia kwa kuboresha chumba hicho kidogo.

Bw Malmas alisema chumba hicho maalum kimeundwa kwa mtazamo wa kiteknolojia ili kusaidia katika tiba kwa kuziba sauti na kunasa makelele ya mtu, kisha kuyahifadhi kwa ajili ya kuchambuliwa. Chumba hicho kimetengenezwa kwa tabaka (Layers) tatu ili kuzuia sauti kutoka ndani au nje ya muundo huo.

Kwa mujibu wa Malmas, tabaka la kwanza linaundwa kwa mbao na ubao wa kawaida. Tabaka la pili na la tatu ndipo kunapowekwa gondoro la kuzuia sauti na nyuzi za glasi kutoka viwandani, ambazo ndizo zinazofanya kazi kubwa ya kuziba sauti. Juu ya gondoro hilo, chumba humaliziwa kwa ngozi ili kukamilisha mwonekano wa kisasa.

“Kinachofanya kazi kubwa zaidi katika kuzuia sauti ni nyuzi za glasi. Tulitumia nyuzi zenye ukubwa wa futi 4 kwa futi 6.5, ambazo ziligharimu Sh30,000 kufunika chumba kizima,” alisema Malmas.

Kwa sasa, timu hiyo ya ubunifu inalenga kuendeleza mradi huo kwa kusambaza katika maeneo mbalimbali hapa nchinni huku ikitafuta washirika na wawekezaji.

Josephat Muchesi almaarufu Mchungaji ambaye ametumia chumba hicho. Picha|Fridah Okachi

“Mpango wetu ni wa kutengeneza vyumba vingi zaidi na kuboresha muundo kwa kutumia vifaa bora zaidi, kwani kiwango cha msongamano wa nyenzo ndicho kinachoamua ubora wa kuzuia sauti.”

Bw Malmas na timu yake wanatarajia kuchangia mapinduzi ya tiba na teknolojia, huku wakitoa suluhisho la kiubunifu linaloweza kubadili jinsi sauti na hisia zinavyoshughulikiwa katika mazingira ya kitabibu.

Mvumbuzi huyo akisema kuwa uvumbuzi huo ni kutokana na utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa mojawapo ya njia ya kupunguza mawazo ni kupiga mayowe ambayo ni rahisi na kila mmoja anaweza kufanya.