Viatu vinavyoundwa kwa magamba ya samaki
NA FRIDAH OKACHI
KIJIJI cha Wath Orego, Kaunti ya Kisumu, ni chenye shughuli kibao, kuanzia kilimo na biashara.
Katika kijiji hicho hicho, ndiko Newton Owino anaendeleza biashara yake ya kipekee licha kuwa mkulima.
Wengi wakiamini kuwa viatu na mishipi huundwa kwa ngozi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo, Owino anaondoa dhana hiyo.
Mjasirimali huyu huunda bidhaa hizo kwa kutumia ngozi, yaani magamba ya samaki.
Unapozuru kilipo kiwanda cha shughuli hiyo, mazingira yatakayokulaki ama kukukaribisha ni ya kijani cha miti, ndizi na mimea mbalimbali ambayo hutumia kama malighafi (huchanganya na magamba ya samaki).
Owino ni msomi wa masuala ya Kemia na anafichua kwamba alianzisha biashara ya kuunda viatu kwa kutumia ngozi ya samaki 2012.
“Uvumbuzi huu ulitokana na kuona jinsi mazingira yalikuwa yakichafuliwa kupitia magamba ya samaki,” anasema.
Baadhi ya kampuni za kuuza samaki baada ya kuvua na kuwaondoa magamba na viungo vya ndani, Owino anasikitika wakati huo hazikuwa zikijali usalama wa mazingira.
Anasema aliandama kampuni kama tisa hivi, ambazo ziliitikia kumsambazia magamba ya samaki.
“Oparesheni yangu pia ililenga kuimarisha ubora wa mazingira, na nilioandama hawakusita kuhusu wazo langu,” asimulia.
Mapendekezo yake pia yalishirikisha Halmashauri ya Kitaifa ya Mazingira (Nema), taasisi ya kiserikali iliyozuru alikonuwia kuanzisha shughuli hiyo na kuiidhinisha.
Miaka 11 baadaye, Owino ana kila sababu ya kutabasamu kufuatia hatua alizopiga.
Anabaini kwamba huwa hatumii kemikali zozote katika kuunda viatu vyake.
Aidha, hutumia mihogo, ndizi na mboga kama malighafi.
Huku bidhaa zake akiuza kati ya Sh500 hadi Sh3, 000, mfanyabiashara huyu anasema zinamezewa na masoko ya ng’ambo ila kiwanda chake ni kidogo kukidhi mahitaji hayo.
“Mwaka 2017, nilijaribu kusaka leseni ya kupanua kiwanda kiwe kikubwa ila vigezo na masharti yaliyowekwa yalikuwa ghali mno,” anasikitika.
Isitoshe, sheria na kanuni za kuuza bidhaa zake nje ya nchi anasema zimekuwa kikwazo kikuu kupanua mianya ya soko.
Huku gharama uchumi ikiendelea kuwa ghali, anasema anategemea kampuni 3 pekee za samaki kumsambazia maganda.
“Nilipoanza, nilikuwa nategemea kampuni 9 ila sasa zimesalia 3 pekee. Mazingira magumu ya biashara yamechangia biashara nyingi kufungwa.”
Hatua hiyo hasa inatokana na nyongeza ya ushuru (VAT) na ada, ambazo zinaendelea kupandishwa kila uchao hivyo basi kuathiri mazingira ya biashara za mapato ya kadri na ya chini (MSMEs).
“Kupata maganda ya samaki imekuwa kibarua,” Owino akasema wakati wa mahojiano ya kipekee.
Yote tisa, kumi, mfanyabiashara huyu anasema hatakata tamaa huku akiomba serikali ya Rais William Ruto kuweka mazingira faafu kwa wafanyabiashara ili kuwekeza pakubwa katika sekta ya viwanda.
Amebuni nafasi 17 za ajira, kati yao 6 wakiwa ni walemavu.