Makala

VIDUBWASHA: Kukabili harufu mbaya kinywani (KIKAR Bad smell checker)

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

IDADI kubwa ya watu wanasumbuliwa na tatizo la kutoa harufu mbaya kinywani.

Lakini wataalamu wa afya ya mdomo wanasema kuwa wengi wa watu walio na harufu mbaya mdomoni hawajui.

Marafiki wanaona haya kukuambia kwamba mdomo unatoa harufu mbaya hivyo tatizo hilo huendelea kwa muda mrefu bila kujua.

Taasisi ya Afya ya Mdomo nchini Amerika inasema kuwa kunuka kwa mdomo husababishwa na bakteria waliomo mdomoni.

Inasema kunuka kwa mdomo kunaweza kuwa dalili kwamba mwathiriwa anaugua maradhi ya fizi.

Uvutaji wa sigara, kahawa, kitunguu na kadhalika ni miongoni mwa visababishi vya mdomo kunuka.

Ukosefu wa mate ya kutosha mdomoni pia kunasababisha kunuka kwa mdomo. Mate husafisha mdomo na hivyo yanapokuwa haba, mdomo hukauka.

Kikar ni miongoni mwa vifaa tele ambavyo vimetengenezwa kuwezesha watu kutambua ikiwa midomo yao inatoa harufu mbovu au la.

Kinakuwezesha kutambua kiwango cha harufu inayotolewa na mdomo wako.

Kifaa hiki hukweleza ikiwa mdomo unanuka sana, unanuka kwa kadri au uko sawa.

Wataalamu wanashauri kusugua meno angalau mara mbili kwa siku baada ya kula. Kadhalika, wanashauri kwamba unaposugua meno, sugua pia na ulimi na hata kuachana na uvutaji wa sigara.