Makala

Vijana kupokea mafunzo ya kuwasaidia kuboresha biashara zao

Na WINNIE ONYANDO December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAMLAKA inayosimamia Biashara Ndogo-ndogo (MSEA), imeanzisha rasmi mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu masuala ya biashara ili kuwawezesha kuinuka kiuchumi.

Mradi huo wa Kenya Jobs and Economic Transformation (KJET) unalenga makundi 94 ya biashara nchini.

Mafunzo hayo ya awamu ya kwanza yalianza Novemba 10, 2025, na yanaendeshwa katika kaunti 10 kabla ya kufikia kaunti zote 47 katika kipindi cha wiki tano zijazo.

Mafunzo hayo yanalenga kuboresha uzalishaji na ukuaji katika sekta ya MSMEs).

Kupitia mitaala ya moduli 12, wahusika wataweza kujenga ujuzi wao wa kutenda kazi utakaowasaidia kuongeza tija, kuimarisha ushindani na kufikia masoko mapya.

Mafunzo hayo yanajumuisha mazoezi, mifano halisi na kazi za makundi zinazoongozwa na wakufunzi waliobobea.

Kijana akisikiza kwa makini mafunzo kuhusu biashara yanayoendesha na Mamlaka inayosimamia Biashara Ndogo-ndogo (MSEA). Picha|Evan Habil.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa MSEA, Bw Henry Rithaa, alisema mradi huo unalenga kuoresha MSMEs ili iwe injini ya ubunifu, ajira na ukuaji shirikishi wa kiuchumi.

Baada ya mafunzo, makundi hayo yataendelea na awamu ya pili itakayojumuisha mafunzo ya miezi mitatu na ushauri wa karibu kutoka kwa wataalamu ili kusaidia utekelezaji wa mafunzo.

Haya yanajiri miezi michache tu baada ya serikali kuanzisha mikakati mipya ya kiuchumi inayolenga kuwapa vijana fursa za kiuchumi huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.

Mkakati wa uzinduzi wa mradi wa NYOTA unaolenga kuwapa vijana 100,000 pesa za kuanzisha biashara ndogondogo.

Oktoba 7, 2025, serikali ilizundua mradi huo wa Sh5 bilioni katika hatua inayofasiriwa kama mbinu ya kuwashawishi vijana wamchague Rais William Ruto mnamo 2027.

Kila kijana atapokea Sh50,000.