Makala

Vijana wageuza Ziwa Kenyatta kuwa Sodoma na Gomora

March 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

ZIWA Kenyatta linapatikana eneo la Mpeketoni, kaunti ya Lamu.

Ziwa hili ndilo kubwa zaidi na ambalo lina maji yasiyo na chumvi kote Lamu.

Ni ziwa linalotegemewa na zaidi ya wakazi 60,000 wa tarafa ya Mpeketoni na viunga vyake ambao hupata maji ya kunywa na matumizi mengine majumbani.

Wakazi pia hutumia maji ya Ziwa Kenyatta kuendeleza kilimo cha unyunyizaji maji mashambani na pia kunywesha mifugo wao.

Miaka ya hivi karibuni Ziwa Kenyatta limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoshukisha hadhi ya chemichemi hiyo kuu ya maji.

Changamoto ya hivi punde zaidi kushuhudiwa ni ile ya vijana ‘wapiga sherehe’ ambao sasa wameligeuza Ziwa Kenyatta kuwa Sodoma na Gomora.

Kulingana na wasimamizi wa bodi mbalimbali zinazolinda Ziwa Kenyatta, vijana wamekuwa wakifika ziwani humo wikendi inapojiri kwa minajili ya kufurahia mandhari.

Mwenyekiti wa Bodi ya Watumiaji wa Rasilimali za Ziwa Kenyatta (LKWRUA), Bw David Muiga, alieleza kutamaushwa kwake na tabia ya vijana hao wapenda raha ambao sherehe zao zimekuwa zikiishia kutumia vibaya misitu au vichaka vidogo vidogo vipatikanavyo kando kando ya Ziwa Kenyatta kama lojing’i zao.

Kulingana na Bw Muiga, kumekuwa na visa ambapo mipira ya kujamiiana almaarufu kondomu imekuwa ikipatikana kwenye mazingira ya Ziwa Kenyatta, hasa vichaka vya karibu.

Aliitaja tabia ya vijana hao ya kufanya ngono bila kiasi, hasa kwenye mazingira ya Ziwa Kenyatta kuwa kero na aibu.

“Ningewaomba hao vijana wanaofika hapa ziwani, iwe ni wikendi au katikati ya juma kujivinjari wawe wastaarabu na pia waje wakiwa wamejipanga. Lazima watunze usafi wa hili ziwa letu. Wasitumie vibaya msitu huu mdogo upatikanao hapa. Nawasisitizia waje wakiwa na nidhamu na heshima kwa ziwa letu na umma kwa ujumla,” akasema Bw Muiga.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Watumiaji wa Maji ya Ziwa Kenyatta (LAKWA), Bw Benson Kariuki pia aliwafokea vijana hao kwa kile alichokitaja kuwa ni kuhatarisha maisha ya viumbe wa majini wanaoishi ziwani humo.

Kulingana na Bw Kariuki, ambaye pia ni katibu wa LKWRUA, nailoni, mifuko ya plastiki, mikebe ya chakula na pia mipira ya kujamiiana inayoachwa kandokando ya Ziwa Kenyatta baada ya vijana kujivinjari mchana kutwa au usiku kucha mara nyingi imekuwa ikibebwa na maji punde kunaponyesha, hivyo kuelekezwa au kuingizwa ziwani.

“Mipira ya kondomu, mifuko ya nailoni au plastiki ikifikishwa ndani ya ziwa inamaanisha samaki waliopo pale watakula taka hizo, hivyo kudhurika. Lazima watu waache kuchafua haya mazingira ya ziwa letu kutokana na raha zao zisizo na mipaka,” akasema Bw Kariuki.

Maafisa hao waliiomba serikali ya kaunti ya Lamu na ile ya kitaifa kufikiria kuweka vyoo vya kisasa kando kando ya ziwa ili kusaidia wanaozuru eneo hilo kupata kujisitiri sehemu salama baada ya kujivinjari.

Walisema Ziwa Kenyatta kwa sasa limekuwa kivutio cha familia nyingi na hata watalii wanaozuru hapo, kukaa masaa yote wakitazama na kufurahia mandhari ya ziwa hilo.

Vile vile waliirai serikali kwamba badala ya kuangazia tu utalii wa mchanga mweupe kwenye fukwe za Bahari Hindi kule kisiwani Lamu na kwingineko, wakati umewadia wa wao kufikiria utalii wa maeneo ya nchi kavu.

“Familia nyingi zaja Ziwa Kenyatta kujivinjari. Kwa sababu hakuna miundomsingi mwafaka, ikiwemo vyoo, wao huishia kwenda haja kubwa vichakani, hivyo kuharibu kabisa mazingira ziwani. Ni vyema wajenge hoteli na mikahawa, nyumba za gesti na pia vyoo hapa Ziwa Kenyatta. Wakifanya hivyo vijana na hata familia zitaweza kuja kupiga kambi hapa Ziwa Kenyatta, iwe ni siku mbili, tatu au hata wiki nzima wakifurahia mazingira ya ziwa letu bila ya kukera wengine,” akasema Bw Kariuki.

Maafisa hao pia waliomba mikakati ya haraka ifanywe kuona kwamba sehemu maalumu za kukusanyia taka kando kando ya Ziwa Kenyatta zinatengwa na vibirika vya kutumbukiza taka hizo vijengwe.

Hilo litawafanya wanaozuru eneo hilo kujivinjari kupata fursa njema ya kutupa taka zao, ikiwemo hiyo mikebe, maboksi, mifuko ya chakula na hata mipira ya kujamiiana iliyotumika sehemu salama.

Si mara ya kwanza kwa Ziwa Kenyatta kugonga vichwa vya habari nchini.

Kati ya 2016 na 2017, ziwa hilo liliathiriwa pakubwa na ukame uliorindima, hivyo kupelekea maji ya ziwa hilo kukauka.

Hali hiyo iliacha maelfu ya viumbe waliokuwa wakishi ndani ya ziwa, ikiwemo samaki, viboko, vyura na vinginevyo vikifariki.

Changamoto zingine zinazokabili Ziwa Kenyatta ni tabia ya wakulima kuendeleza kilimo chao kandokando ya ziwa, hivyo kuchangia mmomonyoko wa udongo na kemikali kuchanganyika ziwani na kupunguza kina chake huku viumbe hai wakidhurika na hata kufa kiholela kila mara.

Wafugaji pia wamekuwa wakisafirisha mamia ya mifugo wao kutoka pande tofauti tofauti za Lamu na kaunti jirani ya Tana River kuwafikisha ziwani kunywa maji, hivyo kuchafua mazingira ya ziwa hilo.

Pia kumekuwa na hulka ya wakazi kufikisha pikipiki zao ziwani, ambapo huziingiza ndani ya ziwa kuziosha moja kwa moja japo changamoto hiyo ilitatuliwa kupitia hamasa za kila mara kwa wananchi.

Ziwa Kenyatta, ambalo lina ukubwa wa karibu kilomita tano mraba, awali lilikuwa likijulikana kama Ziwa Mkunguya.

Jina la Ziwa Kenyatta lilijiri miaka ya sabini (1970s) wakati mwanzilishi wa taifa hili, Mzee Jomo Kenyatta alipotembelea eneo hilo, kubadilisha jina la Ziwa Mkunguya na kulibandika jina lake mwenyewe.