Vijana wanaounda mapambo kwa kutumia mifupa
NA FRIDAH OKACHI
NYAMA ni kitoweo chenye mashabiki wengi nchini, na inaposhabikiwa wengi hutupa mifupa.
Wengine, huipa wanyama wa nyumbani kama vile mbwa na paka.
Wewe unapoila, hufanya nini nayo?
Katika mtaa wa mabanda wa Kibra, kundi moja la vijana kwao mifupa ni dhahabu.
Ni kitega uchumi kinachowaingizia mapato ili kusukuma gurudumu la maisha.
Kibra Ornaments Organization, kundi la vijana wapatao 19, huunda mapambo kwa kutumia mifupa.
Bidhaa wanazotengeneza zinajumuisha; mikufu, shanga, vipuli, na vifaa vya jikoni kama vile vikombe na vijiko.
Kundi hilo lilianzishwa 2015, wakiwa na lengo la kujiendeleza kimaisha ikiwa na pamoja na kudumisha usafi katika mazingira.
“Ni biashara ya sanaa ambayo imetupiga jeki pakubwa kimaisha,” Charles Oigo, mwasisi na msimamizi anafunguka.
Kulingana na Oigo, 37, hutoa mifupa kutoka masoko mbalimbali Kaunti ya Nairobi, hususan kwenye buchari, vichinjio na wanaochemsha nyama.
Biashara hiyo ikiwa iligharimu mtaji wa Sh470, 000, mwanzo wanapopata mifupa huichagua, Oigo akisema shughuli hiyo vilevile kando na ukaguzi wa macho, hutumia mashine kutambua ile bora.
Aidha, kiwanda chao kina jumla ya mashine, moja ikiwa ni ya kuchagua, nyingine ya kusaga na kuyeyusha, kukausha na kuunda bidhaa.
Uundaji bidhaa, wao wenyewe ndio hutengeneza.
Husambaza bidhaa zetu kwa duka moja jijini Nairobi, anasema Dennis Orero, fundi wa mitambo na msimamizi wa mauzo.
“Kila wiki, mwanachama hakosi kupokea mapato yasiyopungua Sh20, 000,” Orero anafichua.
Ni kazi ya ubunifu ambayo imewasaidia pakubwa kujiendeleza na kujikimu kimaisha, Orero akikiri kufanya maendeleo makubwa.
Ubunifu wa kundi hilo katika sanaa una mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya juakali, ikizingatiwa kuwa inatumia malighafi yanayofasiriwa kuwa taka na kuyaongeza thamani.
Kulingana na Ripoti ya Ukuaji wa Uchumi Mwaka 2022 ya Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), inaonyesha sekta ya juakali ilichangia asilimia 25 ya mapato ya kitaifa.
Mtaalamu wa Masuala ya Kiuchumi, Godfrey Ayaro, anasema sekta ya juakali inapaswa kupigwa jeki kwa kiwango kikubwa kufuatia mchango wake hasa katika kubuni nafasi za ajira nchini.
Aidha, juakali inakadiriwa kubuni zaidi ya asilimia 80 ya nguvukazi nchini.
“Isipuuzwe, serikali iipige jeki kwa hali na mali,” mtaalamu huyo anahimiza.
Kibra Ornaments Organization ina imani kuwa ni kwa muda tu itambe, na kuingia kwenye orodha ya kampuni zinazoingiza mamilioni ya pesa.
Licha ya ufanisi wake, kundi hilo linapata ushindani mkuu kutoka kwa bidhaa sawa na wanazounda.