Vijiji jirani na kituo cha uzalishaji umeme vyakaa gizani
NA OSCAR KAKAI
NI saa mbili usiku katika kijiji cha cha Riting kwenye kingo za Mto Turkwel, huku utulivu ukitanda pamoja na giza totoro.
Nyumba nyingi zilizopo ni zilizojengwa kwa udongo huku kijiji kikionekana kutelekezwa na kukosa maendeleo.
Kulingana na wanakijiji kiza huwatorosha nje na kila mtu huingia nyumbani kwake kulala mwendo wa saa moja jioni. Hii ni kutokana na kukosa stima kwenye kijiji hicho ambacho kiko karibu na mtambo wa kuzalisha umeme wa Turkwel.
Mtambo huo ambao uligharimu Sh6 bilioni na uliopo umbali wa kilomita 76 kutoka mji wa Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi, haujasaidia wenyeji.
Kituo cha kibiashara cha Riting na kijiji ambacho kiko kilomita nne kutoka mtambo wa umeme wa Turkwel, hakijaunganishwa na umeme kwa muda mrefu tangu mtambo huo ujengwe na kampuni ya Ufaransa na kuzinduliwa na aliyekuwa rais Daniel Arap Moi.
Wakazi zaidi ya 5,000 wanatumia taa za chemni zinazotumia mafuta taa huku wachache wakitumia sola. Hali hii imebainika kuwahatarisha wakazi hasa wanapokumbwa na dharura za kiafya na usalama usiku.
Kulingana na wakazi, ukosefu wa stima ni changamoto kuu kwao.
Licha ya mtambo huo wa kuzalisha umeme kutoa megawati 106, wakazi hawana lolote la kujivunia.
Nyaya za stima ambazo zimepita eneo hilo zinakera wakazi ambao hawana matumaini ya kupata stima na maendeleo mengine kwa jamii.
“Tumetengwa na serikali. Tangu mwaka wa 1980, stima ilitolewa hapa hadi Nairobi lakini wakazi hawajawahi kuiona. Biashara zetu haziwezi kunawiri sababu tuko gizani. Tunaomba kampuni ya Kenya Power kutuletea stima,” alisema Bw Dennis Yarapong, mkazi wa Riting.
Bw Yarapong anasema kuwa vijiji vingi vina nyoka ambao huvamia watu nyakati za usiku.
Mbunge wa Kacheliba, Bw Titus Lotee, alisema kuwa umaskini umechangia watoto wengi kuacha shule licha ya kampuni hiyo kuwa na uwezo wa kuwapa ufadhili wa masomo.
“Mtambo huo uko na manufaa gani? Wakazi wanaendelea kuumia na uchochole huku kampuni ikiendelea kupata faida. Ni vyema kampuni hiyo kusadia jamii,” alisema Bw Lotee.
Hata hivyo, Waziri wa Kawi, Bw Davis Chirchir, alisema kuwa anafahamu kuhusu kilio cha wakazi ambao hawana stima na shida hiyo itatatuliwa punde tu nyaya za stima zitakapowekwa.
“Tuko na mpango wa kuhakikisha kuwa jamii ya eneo hilo inanufaika na stima,” alisema waziri Chirchir.