Makala

Vijiji Lamu wakazi hawatumii simu za mkononi miaka 60 tangu uhuru

Na KALUME KAZUNGU April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya wakazi 20,000 wa karibu vijiji 10 vya Lamu wameikashifu serikali na kampuni zinazohusika na mawasiliano nchini kwa kuwatelekeza.

Wakazi wa vijiji vya Maisha Masha, Kangawati, Jipendeni, Lake Amu, baadhi ya sehemu za Baharini, Pangani, Mkunumbi, Kipungani na Witu, vyote vikipatikana Lamu Magharibi, hawajakuwa wakitumia simu zao za mkononi kutokana na kukosekana kwa mawimbi ya mawasiliano maeneo yao.

Idadi kubwa ya vijiji husika vilianzishwa tangu Kenya ilipopata uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Katika mahojiano na Taifa Leo, wakazi walisema kukosekana kwa mawasiliano vijijini kumewanyima fursa muhimu za kujiendeleza kibiashara, kielimu, kisiasa na kijamii.

Sehemu mojawapo ya kijiji cha Pangani, Lamu Magharibi. Pangani ni miongoni mwa vijiji vinavyokabiliwa na ukosefu wa mawimbi ya mawasiliano. Picha|Kalume Kazungu

Kinyume na wakazi wa maeneo mengine ya nchi ambapo kuwepo kwa mawasiliano kumewawezesha kufuatilia habari na mijadala mingine mitandaoni, ikiwemo Facebook, Instagram, X (Twitter), WhatsApp, wakazi wa vijiji vya Lamu wamebaki gizani bila kufahamu kinachoendelea nchini na ulimwenguni.

Emmanuel Kimwa, mkazi wa Lake Amu, alishinikiza haja ya serikali na kampuni za mawasiliano kufika vijijini kutathmini hali na kuhakikisha minara ya mawasiliano imejengwa mara moja.

“Tumechoka kutelekezwa. Itakuwaje tuko karne ya 21 na bado tumesalia gizani bila mawasiliano? Ni miaka 62 sasa tangu uhuru upatikane. Serikali na kampuni husika zije huku mashinani kutuwekea hiyo minara au milingoti ya mawasiliano angalau nasi tuunganishwe na ulimwengu,” akasema Bw Kimwa.

Kadzo Chengo, mkazi wa Jipendeni, alihoji sababu zinazoisukuma serikali na kampuni za mawasiliano kuendelea kughairi kusuluhisha tatizo la ukosefu wa mawasiliano vijijini mwao.

Bi Chengo alikiri kuwa walimu na wanafunzi wanapata shida katika kuuendeleza mtaala mpya wa CBC ambao unahitaji teknolojia kwa wingi.

“Wanafunzi na walimu wote wanahangaika kutekeleza CBC. Huwezi hata kutumia simu yako kufundishia wanafunzi. Hakuna mawimbi ya mawasiliano wala stima. Warekebishe hili jambo,” akasema Bi Chengo.

Mbali na elimu, ukosefu wa mawasiliano na umeme pia umetatiza masuala ya afya.

Charo Chumbi, mkazi wa Maisha Masha, alisema hawajaweza kunufaika na mpango wa madaktari wa watoto nyanjani kiteknolojia, yaani Daktari Smart Telemedicine kutokana na ukosefu wa mawasiliano vijijini mwao.

Mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Mangai, msitu wa Boni, Lamu Mashariki. Karibu vijiji kumi vya Lamu Magharibi vinakabiliwa na ukosefu wa mawimbi ya mawasiliano wakazi wakiishinikiza serikali kuwajengea minara hiyo ili kuunganishwa na ulimwengu. Picha|Kalume Kazungu

Kitengo cha Daktari Smart Telemedicine kilifunguliwa ndani ya hospitali ya Mpeketoni tangu Novemba 2021.

Anasema ili kutumia simu zao mara nyingi wamelazimika kupanda pikipiki kusafiri kati ya kilomita 6 na 10 kufika mjini Mpeketoni.

Akihutubia umma mjini Mokowe, Mbunge wa Lamu Magharibi Stanley Muthama alikiri kuwa kukosekana kwa mawasiliano vijijini kumeathiri karibu sekta zote, ikiwemo usalama, elimu, biashara, kijamii nakadhalika.

Bw Muthama aliitaka serikali na kampuni husika za mawasiliano nchini kufanya hima kujenga minara vijijini kuwawezesha wakazi kutumia simu zao za mkononi kama Wakenya wengine.

“Nimeandika zaidi ya barua sita kuomba kampuni za mawasiliano kuangalia hali ilivyo vijijini mwetu. Minara michache ya mawasiliano iliyokuwepo iliharibika tangu mwaka jana ilhali vijiji vikiachwa gizani bila mawasiliano. Ni ombi langu kwamba serikali na kampuni husika zitasikia kilio chetu na kutatua shida ya mawasiliano,” akasema Bw Muthama.

Februari, 2025, visiwa vya Shanga, Siyu na Mkokoni vilivyoko Lamu Mashariki viliunganishwa kwa mawasiliano kwa mara ya kwanza katika historia.