Makala

Vikundi 13 Thika vyapokea fedha za Uwezo Fund kujiendeleza

September 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

VIKUNDI 13 kutoka mjini Thika vimenufaika na fedha za mikopo za Uwezo Fund kwa lengo la kuendesha biashara zao.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alivikabidhi hundi za fedha za takribani Sh1.8 milioni.

Miongoni mwa vikundi hivyo, kulikuwa na vikundi viwili vya viziwi na vipofu ambao pia walipokea fedha zao za kuendesha miradi mbalimbali.

Bw Wainaina alisema vikundi hivyo vinajihusisha na biashara za useremala, uchuuzi, ufugaji wa mbuzi na nguruwe, na pia ususi.

Alisema vikundi hivyo tayari vimepewa hamasisho la jinsi ambavyo vinaweza kutumia mikopo hiyo kwa njia inayostahili.

“Tayari natarajia wengi waliopewa fedha hizo watazitumia kwa njia nzuri ya uwazi itakayowanufaisha wote.

Alisema lengo lake kuu ni kuona ya kwamba ajenda nne muhimu za serikali zinazingatiwa ili kuafikia malengo hayo.

Alitoa mwito kwa vijana popote walipo waungane na kutafuta miradi muhimu itakayowanufaisha kibiashara.

Alitoa mfano wa vijana 20 walioungana pamoja na kuanza kuendesha biashara ya viazi na baada ya kununua mitambo ya kukausha na kuvichonga sasa wanaweza kujitegemea pakubwa.

“Niliwapa vijana hao mawaidha na kwa wakati huu, wanaweza kupata hadi zaidi ya Shilingi laki mbili kila mwezi,” alisema Bw Wainaina akihutubia makundi hayo mnamo Jumatano.

Bi Jecinta Syombua ambaye ni kipofu anasema amejiunga na kikundi cha Kuvumiliana Self Help Group ambacho kiko katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika.

“Sisi tulipokea Sh100,000 ili tujiendeleze hasa na ufugaji wa mbuzi ambao kwa sasa ni 13. Pia tunaendesha maswala ya ususi na tuna watu 25 kwenye kikundi chetu,” alisema Bi Syombua.

Naye kinara wa wachuuzi 44 mjini Thika, Bw Dancan Karuku anasema walipokea hundi ya Sh200,000 ili kuendeleza ujenzi wa jumba lenye orofa sita ambapo tayari orofa ya kwanza inakaribia kukamilika.

“Maono yetu ni kwamba hata tukistaafu katika kazi zetu bila shaka bado tutapata pesa za kujikimu uzeeni,” alisema Bw Karuku.

Bi Pauline Wanjiru Ndung’u wa kikundi cha Kiandutu Centre Base chenye wanachama wapatao 20 anasema wamenunua kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari mbili kwa lengo la kujiendeleza.

“Kwa wakati huu tunafuga kuku wapatao 30 ambapo tunazidi kuuza mayai. Kila mmoja wetu anajitolea kuona ya kwamba mradi huo wetu unanawiri kwa manufaa yetu wenyewe,” alisema Bi Ndung’u.

Alisema wanataka kuona ya kwamba ifikapo mwaka 2020 watakuwa wamepiga hatua kwa kujiendeleza.