• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 3:58 PM
Viongozi waambiwa waachie asasi maalum vita dhidi ya pombe

Viongozi waambiwa waachie asasi maalum vita dhidi ya pombe

NA MWANGI MUIRURI

VITA dhidi ya pombe haramu, mihadarati na ukosefu wa nidhamu miongoni mwa wamiliki wa baa ambavyo vimezinduliwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa sasa vinapata upinzani mkali, walalamishi wakidai viongozi wanavitumia vibaya.

Walalamishi pia wanadai vimetiwa doa na ufisadi.

Wadau katika sekta hiyo sasa wanalia kwamba baadhi ya maafisa wa serikali pamoja na wanasiasa wamechukulia vita hivyo kama vya kisasi na vya kusaka utajiri wa bwerere.

Kisa walichokimulika ni kile cha mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi ambaye akiwa ameandamana na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga, walivamia stoo ya serikali katika Kaunti ndogo ya Mathira Magharibi mnamo Februari 26, 2024, na kuharibu shehena ya pombe ya thamani ya Sh4.5 milioni.

Mlalamishi anadai pombe ya kampuni ya Patiala ilirejelewa na wanasiasa hao kuwa ni haramu hata kabla ya taasisi ya ukadiriaji wa ubora wa bidhaa (Kebs) kutoa ripoti yake ya ukaguzi.

Baadaye Kebs ilitoa ripoti mnamo Februari 27, 2024, ikiitaka kampuni hiyo ya Patiala kusitisha usambazaji wa aina kadha za pombe yake kwa msingi kwamba kulikuwa na malalamishi.

Baadhi ya wakazi wa eneobunge la Mathira washiriki harakati za kuharibu pombe iliyodaiwa kuwa ya mauti. PICHA | MWANGI MUIRURI

Ilichukukuliwa ni vita vya msukumo wa kisiasa Kebs iliposema malalamiko ya umma na wala sio ukadiriaji wa ubora na usalama wa kiafya.

Hata hivyo, kupitia wakili Danstan Omari mnamo Februari 29, 2024, mmiliki alipata agizo la mahakama kutoka kitengo cha jopo la ukadiriaji ubora ikitupilia mbali amri hiyo ya Kebs hadi kesi ya utathmini iandaliwe na iamuriwe.

“Tunateta kama wanasheria na wawekezaji kwamba vita hivi ambavyo ni vya maana vimeingiwa na ukora usioeleweka wa kuvunja sheria kiholela na kuwanyima wengine haki zao ili kujizolea sifa za kisiasa,” akasema Bw Omari.

Bw Omari alilalama kwamba “mkondo wa sheria ulihitaji pombe hiyo ishukiwe kuwa haramu, wakadiriaji wa ubora waitwe watekeleze ukaguzi na kisha watoe ripoti ya kuidhinisha au ya kudunisha”.

Lakini kilichojiri kutoka kwa wanasiasa hao, akasema Bw Omari, “ni kujitwika majukumu ya ukaguzi ubora na wakaafikia hatua ya kuharibu utajiri wa mtu kwa msingi usio halali”.

Katika mitaa, polisi wanadaiwa kutekeleza misako katika baa bila kuandamana na maafisa wa Kebs na kuishia kutoa hukumu zisizo na mashiko ya kisheria.

“Mimi ni mmiliki wa baa katika Kaunti ya Murang’a. Mnamo Ijumaa wiki jana, maafisa waliingia katika baa yangu na wakasema wamepata dokezi nilikuwa nikiuza pombe haramu. Waliniambia niwape Sh10,000 ama nikamatwe nikalale kwa seli na kisha mahakamani nitozwe Sh50,000,” akasema mwekezaji.

Anasema kwamba alikopa ili kuepuka balaa na akawapa maafisa hao, hali ambayo anadai imewakumba wengi wa wamiliki wa baa.

Mmojawapo wa wakazi wa eneobunge la Mathira ashiriki harakati za kuharibu pombe iliyodaiwa kuwa ya mauti. PICHA | MWANGI MUIRURI

Katika Kijiji cha Maica ma Thi kilichoko Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini, maafisa wa serikali wanadaiwa kushika doria huku wakiwakamata vijana kwa msingi ni washukiwa wa utengenezaji wa chang’aa.

“Sisi tulikuwa tunapika chang’aa mwaka 2023 lakini tumebadilika baada ya kupata kazi ya kutekeleza usafi mitaani ambayo serikali ya Kaunti imetoa. Lakini tukitoka kwa hiyo kazi baadhi yetu tunatiwa mbaroni tukiitwa wapishi wa chang’aa. Si haki,” akasema Bw James Njoroge, mkazi.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Joshua Nkanatha aliambia Taifa Jumapili kwamba malalamishi yote yasiyowasilishwa kwa wakubwa kwa njia rasmi, hayawezi yakathibitishwa.

“Ningetaka kusema wazi kwamba malalamiko yote dhidi ya maafisa wangu nyanjani iwapo yatawasilishwa kwa njia rasmi nitahakikisha kwamba yanachunguzwa na hatua za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya wote walio kwa lawama,” akasema Bw Nkanatha.

Kamishna wa Murang’a Joshua Nkanatha. PICHA | MAKTABA

Katika Kaunti ya Kirinyaga, mwenyekiti wa wawekezaji wa sekta ya hoteli na baa Catherine Kinyua aliteta kwamba maafisa wa usalama walichukulia janga ambapo watu 23 waliaga dunia baada ya kubugia pombe ya sumu, kuanza kudhulumu wamiliki wa baa.

“Serikali ya Kaunti ikiungwa mkono na ile ya kitaifa, ilitoa amri baa zote zifungwe. Kile kilifuatia ni ufisadi mkuu ambapo ili baa yako ikubaliwe kufungua kazi, unatakiwa kutoa hongo ya kati ya Sh20,000 na Sh50,000 kando na kulipa leseni upya,” akasema Bi Kinyua.

Aliongeza kwamba serikali ya kaunti pia ilichukua fursa hiyo kudai malipo ya leseni yaliyokuwa yamefutiliwa mbali wakati wa janga la Covid-19.

“Ile pesa serikali imepata kihalali na kiharamu kutoka kwetu si kidogo. Hii ya sheria ya mtu mmoja akikosea sisi wote tunaambatanishwa na makosa hayo, ni ukiukaji wa haki zetu za kimsingi na hakuna lile tungefanya kwa kuwa serikali yote ilikuwa imekesha kwetu,” akasema mmiliki wa baa, Bw Leonard Gitari.

Kamishna mshirikishi wa eneo la Kati Fred Shisia alisema kwamba “kuna mengi yatasemwa katika hivi vita lakini la maana ni kwamba tunafaa kuelewa hatutakoma hadi tufanikiwe kuafikia malengo yetu.”

“Kwa wote walio na malalamishi, tutatilia maanani iwapo yataletwa kwa msingi rasmi,” akasema Bw Shisia.

Ingawa wengi wanakubali kwamba vita dhidi ya ulevi kiholela na utumizi wa mihadarati, hali za ukandamizaji, ufisadi na ubaguzi wa utekelezaji sheria ni baadhi ya masuala yamezidi kusononesha wengi.

“Serikali ikome kutumia njia za mkato katika utekelezaji sheria. Ifunge kiini cha pombe haramu na pia iwape vijana kazi ili wakome kurandaranda wakisaka ‘afueni za maisha’ ndani ya baa,” akasema aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni.

Bw Kioni aliita serikali ikome uzembe na iwajibikie masuala ya uadilifu katika hali zote za kutoa huduma za kiutawala.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wapinga bei ya mbolea ya gharama nafuu

Eneo la Tusitiri latajwa kuwa ngome ya mapepo katika Bahari...

T L