Makala

Vita dhidi ya pombe vyageuka ujenzi wa mnara wa Babeli

March 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA MWANGI MUIRURI

VITA vinavyoendeshwa Mlima Kenya dhidi ya pombe ya mauti, mihadarati na utundu wa wamiliki wa baa vimegeuka sawa na ule ujenzi wa mnara wa Babeli ambapo wajenzi walionuia kumfikia Mungu walikosa kuelewana lugha.

Sawa na mnara huo, vita hivyo vya pombe vimegeuka kuwa hali ya kuelekezeana vidole vya lawama kuongea kwa lugha ya kukinzana.

Naibu Rais Rigathi Gachagua anadai kwamba tatizo la ulevi usiodhibitiwa lililetwa na magavana pamoja na mawaziri wao.

“Magavana wakisaka ushuru pamoja na mawaziri wao, ndio walitoa leseni kiholela hadi tukawa na shida tuliyo nayo kwa sasa. Walipeana leseni za kuuza pombe kwa karibu kila mtu, wengine wakiwa nazo lakini bado hawajafungua baa. Leseni za baa zilitolewa kama vitambulisho,” akasema Bw Gachagua.

Nao magavana wanaelekeza lawama kwa kamati za masuala ya usalama ambazo husimamiwa na makamishna wa kaunti. Makamishna nao wanalaumu mahakama kwa kuwa kimbilio la wakora wa ulevi na mihadarati.

Mwishoni mwa mwaka 2023, Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata alisema kwamba maduka ya uuzaji pombe almaarufu ‘Wine and Spirits’ yalikuwa yamejaa kila pembe ya kaunti, sababu ikiwa ushirika wa kamati ya usalama.

Kamishna Patrick Mukuria wakati huo aliteta kwamba kazi ya kusajili na kutoa leseni ilikuwa ya Bw Kang’ata.

Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki naye anasema wanasiasa wanahujumu vita hivyo na hawafai kujihusisha navyo.

“Huu ni msako wa kiusalama wa kusaidia vizazi na hatutaki wanasiasa ndani yake. Maafisa wa kiusalama ndio wanashirikisha operesheni hizi kwa msingi wa usalama wa kitaifa na wanasiasa wanafaa wakae mbali bila kuingilia,” akasema.

Mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi pamoja na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga, wameapa wataendelea kujihusisha na vita hivyo na hawatakubali pombe ya mauti kuuzwa katika Kaunti ya Nyeri.

Mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi aongoza wafuasi wake kuharibu chupa 34,000 za pombe ya kampuni ya Patiala katika eneobunge la Mathira. PICHA | MWANGI MUIRURI

Wawili hao tayari wameshavamia stoo ya serikali katika eneobunge la Mathira ambapo shehena ya pombe iliyokuwa ikingojea maafisa wa kuidunisha au kuiharamisha kufika na kutoa ripoti yao.

Hata kabla ya maafisa hao kufika na kukagua shehena hiyo, wanasiasa hao wawili walifika na wakavunja stoo hiyo huku wakiongoza wafuasi wao kuharibu chupa 34, 000 za pombe hiyo.

Kwa upande wao, wamiliki wa baa wanailaumu serikali kwa kile wanachokitaja kuwa na lengo la kupigana na biashara halali, huku wengine wakiteta kugeuzwa kuwa shamba la kuvunwa hongo na maafisa wa kiusalama pamoja na wale wa Kaunti.

Mrengo wa Azimio ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni unateta kwamba “serikali iliyoingia mamlakani ikisema italinda riziki za mahasla ndiyo hiyo imegeuka kuwa adui mkuu wa kuvunja ajira na kuwatuma wengi kwa umaskini”.

Naye Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria ametaja vita hivyo vinavyoendelezwa na Bw Gachagua kuwa “butu na visivyo na umakinifu wa kimawazo ambapo malengo yanayokusudiwa yanamezwa na uhasi unaohusika kiasi kwamba hali inabakia kuwa mbaya zaidi”.

Hayo yakijiri, Bw Gachagua amenukuliwa akisema kwamba “mimi sijali kupoteza umaarufu wa kisiasa kwa kuwa nina kwangu na bibi yangu iwapo nitakosa kuchaguliwa kutokana na hivi vita vya kuokoa vizazi”.
Lakini magavana wengine wanashuku Bw Gachagua kama anayewasaliti kwa wapigakura.

“Mimi nitahitaji kuchaguliwa kwa awamu ya pili. Bw Gachagua anajua waziwazi kwamba yeye hataomba kura kwa kuwa Rais William Ruto ndiye atakuwa akiomba awamu ya pili huku akimbeba mgombezi mwenza. Hakuna vile nitakosana na wamiliki wa baa ndio nimfurahishe Bw Gachagua,” akasema gavana mmoja wa eneo la Kati.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Martha Koome amekariri kwamba “mahakamani sio kwa kuwasilishwa hisia za kibinafsi mbali ni ngome ya haki kwa wote kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na kesi zitaamuliwa kwa kuzingatia misingi ya haki”.

Mnamo Februari 10, 2024, akiwa katika Kaunti ya Murang’a, Bw Gachagua alikuwa ameteta kwamba “mahakama hizi za dada yetu ambaye ni Bi Koome zinasaidia kero hii kutulemea huku wanaokufa ni watoto wetu…Tutaongea naye atwambie ni kwa nini maafisa wake hawaoni shida tuliyo nayo ya vijana wetu kuharibiwa na kupotea ndani ya ulevi kiholela”.

Huku hao wakilumbana, nao walevi wanateta kwamba kuachishwa pombe ghafla huenda kuwaue kwa kulemewa na ‘lock’.

Wameteta kwamba hata sayansi imesema kwamba uzoeefu unafaa kutamatishwa kwa utaratibu wala sio ghafla kwa vitisho vya kukamatwa na kufungwa jela kama inayofanyika kwa sasa.

Nao mabwanyenye wa kutengeneza pombe wanateta kwamba kuna mapendeleo ya kutoa leseni huku wale waliokuwa katika mrengo wa Azimio katika siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 wakinyimwa nafasi ya kuwa katika biashara hiyo ili waliokuwa wanaunga walio serikalini kwa sasa watuzwe na leseni.

[email protected]