Makala

Vita vya ubabe wa siasa Mlima Kenya vyaendelea chini

March 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA MWANGI MUIRURI

Japo vita vya ubabe wa kisiasa Mlima Kenya vinaonekana kutulia, vinaendelea chini kwa chini wanaosakata ngoma wakiibuka na mbinu mpya za kurushiana maneno.
Hii ni licha ya Rais William Ruto Februari 2024 kuzima makabiliano ya wafuasi wa Mbunge wa Kiharu na wale wa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ambao walikuwa wamepapurana hadharani.

Bw Nyoro, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, amegeuza ngoma yake kuwa ya kuunda daraja na wanasiasa kutoka maeneo ya nje ya Mlima Kenya, naye Bw Gachagua akibakia tu kutandaza ubabe wake katika vijiji vya Agikuyu, Aembu na Ameru.

“Sifanyi kampeni bali kile ninafanya ni kusaidia Rais kuunganisha taifa na pia kuuza sera za utawala wake bora. Rais ametukanya kupiga siasa za kuongea kuhusu wengine na pia kujibizana na yote utaona nikifanya usihusishe siasa za ushindani,” akasema Bw Nyoro.
Hata hivyo, mwelekezi wa siasa zake za ubabe Mlima Kenya, Bw Joe Nyutu, ambaye ni Seneta wa Murang’a anasisitiza kwamba “licha ya kuheshimu Rais na amri yake ya kutukanya tusishiriki siasa za ubabe, hali ni kwamba Bw Nyoro ni nyota inayong’aa na wakati wake ukifika wa kutupa mwelekeo, tutaichangamkia”.

Huku kitendawili kikiwa; wakati huo utakuwa upi, Bw Nyutu anasema “ya Mungu ni mengi, inaweza kuwa ni kesho, mwaka ujao, 2027, 2032 au hata 2047 bado umri unamkubalia”.

“Hakuna letu la mikakati limekwama, tuko kiwanjani”.

Kwa upande wake, Bw Gachagua amezidi kujitangaza kama kinara wa wanasiasa wote wa Mlima Kenya, huku akiwataka waungane nyuma yake kwa minajili ya 2027 na 2032.

“Mwaka 2027 tutaungana nyuma ya kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto nikiwa mgombea mwenza. Mambo ya 2032 tuyaachie Mungu. Mimi nitakuwa ninashughulikia vita dhidi ya pombe na mihadarati. Pia makateli katika sekta ya kilimo. Wote wanaotaka kiti, wasubiri tumalize awamu yetu ili tuwapange,” akasema mnamo Februari 15, 2024 akiwa Kaunti ya Murang’a alikoandamana na Rais.

Mito ya Bw Gachagua inaangazia ari pia ya kumezea mate Ikulu, hasa ikizingatiwa kwamba alionya mahasidi wake kwamba “usinione tu hivihivi hata mimi licha ya kuwa sio mwerevu sana bado siwezi nikasemwa ni mjinga… Kuna yale pia mimi nayajua”.

Wawili hao wakikimbizana nyanjani, Waziri wa Utumishi wa Umma, Bw Moses Kuria amezindua harakati za kuunganisha Mlima Kenya akitumia ligi ya kandanda.

Kwenye mahojiano, aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba ameshakutana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) ili kumsaidia kuandaa dimba la maeneo bunge 66 lililong’oa nanga Februari 4, 2024.

“Mshindi wa ligi hiyo atatia kibindoni zawadi ya Sh5 milioni, wa pili akijipa zake Sh3 milioni, naye wa tatu akijipa Sh 1 milioni,” akasema.

Alisema kwamba shabaha ya dimba hilo, ni kuleta pamoja vijana wa Mlima Kenya

“Isitoshe, ninaongea nao kuwapa ushauri nasaha wa msimamo wa sasa na wa baadaye kuhusu taifa la Kenya,” Waziri Kuria akasema.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki kwa upande wake anaonekana kushughulika na kujiangazia kama mchapa kazi.

Katika kura za maoni za hivi karibuni, Bw Kindiki anadaiwa kukiri kwamba hana haja na mjadala wa siasa za urithi.

Hata hivyo, wafuasi wake kutoka Kaunti ya Tharaka Nithi wakiongozwa na mshirikishi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA ) Bw Alex Muthomi ameshikilia kwamba “kinara wetu kwa sasa yuko bizi akihudumia majukumu yake ya wizara, lakini 2027 tutadai nafasi yake iliyoporwa 2022”.
Kinara wa Narc Kenya Bi Martha Karua kwa sasa ametangaza kwamba atarejelea kujenga chama chake katika kaunti zote 47 na pia ajiweke pema kwanza katika ngome ya Mlima Kenya.
“Tutaanza na kuandaa kongamano la Mlima Kenya katika mahali takatifu pa kimila kule Limuru, Kaunti ya Kiambu. Hapo ndipo tutatoka na kauli yetu kama jamii kuhusu 2027 na baadaye,” akasema Bi Karua.
Aidha, akiungana na mshirika mkuu wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta; aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Bw Jeremiah Kioni, wamezindua vuguvugu la Kamwene ambalo humaanisha ‘masilahi yetu’ ili kuleta pamoja wapiga kura wa Mlima Kenya katika kapu la 2027.
Mwingine ambaye ameshtua wengi kutokana na ujasiri wake wa kujitosa katika makuu ya siasa za Mlimani, ni aliyekuwa kinara wa kundi haramu la Mungiki, Bw Maina Njenga.

Akipinga Bw Gachagua moja kwa moja, Njenga ambaye amejipata akitiwa mbaroni pamoja na wafuasi wake na kisha kushtakiwa anasema kwamba “hakuna kiti cha mtu kisiasa na chochote kile kinachowaniwa huamriwa kwa kura wala sio kupitia kujitakasa au kukinyakua”.

Anashikilia kwamba ikiwa watu wanaenzi demokrasia ambayo ilipiganiwa kwa jasho, damu na machozi, ni lazima wote wapewe nafasi ya kuwania.
Bw Njenga anasema analenga vijana ambao kwa muda sasa wamekuwa wa kutumiwa na kisha wanawekwa pembeni utawala ukitekelezwa.
“Safari hii tumeapa kwamba ni lazima vijana watakuwa mawindoni 2027. Kisha windo likinaswa wawe hapo likigawanywa na hatimaye wawe kwa hiyo meza ya mlo,” akasema.
Mwanasiasa mwingine ambaye ametangaza nia ya kupaa kisiasa, ni mbunge maalum, Bi Sabina Chege.

“Mimi kwa sasa napambana kutwaa mikoba ya chama cha kisiasa cha Jubilee ili tukijenge, tukipambe na hatimaye tukirejeshe katika sifa zake za 2017 hadi 2022 ambapo ndicho kilikuwa tawala. Baada ya hapo, hata ninaweza nikawashtua kwa kuibuka mwanamke wa kwanza Rais nchini,” akasema.
Mwanamke mwingine ambaye pembeni anaonekana akiwa windoni ni Bi Anne Waiguru ambaye ni Gavana wa sasa Kirinyaga.

Akiwa anahudumu awamu ya pili na ya mwisho Kikatiba, anatazamiwa kuwa katika mstari wa mbele kutoa mwelekeo wa Mlima Kenya 2027.
Kwa sasa, anaonekana akitumia wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (CoG) ambapo hukaidi hata baadhi ya misimamo ya serikali kuu kama njia ya kuonekana mtetezi sugu wa ugatuzi.
Tayari, mbunge wa Mwea Bi Mary Maingi ametangaza kwamba “wanaume watukome hizi siasa zao za ubabe na wajue kwamba hata Bi Waiguru anatosha na ikiwa atasusia, wanawake ambao tuko tayari kuvurugana tukisaka makuu ya Mlima na nchi tuko wengi”.
Katika harakati hizo, Bi Waiguru ameonekana kuwa na ushirika na Gavana wa Embu Bi Cecily Mbarire ambaye ndiye mwenyekiti wa chama cha Rais cha UDA.
Bi Mbarire tayari ametangaza kwamba nafasi ya wanawake katika siasa za Mlima Kenya pamoja na nchi nzima sio ya kubatishwa, ni ya uhakika.