Makala

VITUKO: Ndoto yamchochea Sofia kuyoyomea mtaani Ngomeni kumtafuta mumewe

May 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMUEL SHIUNDU

SOFIA alihangaika sana usiku huo.

Hakutulia tangu ampigie simu mumewe na kujibiwa na sauti ya kike.

Kila usingizi ulipomhurumia na kumnyemelea lau kwa sekunde chache, ndoto za kila nui zilimpita kichwani.

Wakati mmoja aliota Sindwele akikataa kumsikiliza na kumfurusha.

“Uliringa nilipokuhitaji! Sasa umefwata nini huku kwa mlevi? Aisee ni wakati wangu kukuringia,” Sindwele alibwata.

Mara akaota wakipapurana na binti fulani. Walikuwa wakizozania Sindwele.

Sindwele alipoulizwa kuchagua kati ya Sofia na binti huyo, akachagua binti huyo.

“Sofia nilimpenda licha ya wokovu wake na kelele zake, lakini yeye kauchukia ulevi wangu. Ulevi tu! Nastahabu huyu binti anayejua kwamba mtu akipenda boga, hupenda na ua lake.”

Ndoto hizo pamoja na maneno ya Sindwele yalimparamishia Sofia usingizi kabisa.

Akastahanu kukodoa macho na kusubiri machweo.

‘Lazima asubuhi ikifika nirejee kwa mume wangu. Hivi hata nikimwacha nitakwenda wapi? Nani atakayenioa na huu umri wangu unaoinamia magharibi?’ alijiuliza huku akigaragara kitandani kama hindi linalookwa.

Mtu kuitwa uchawini

Aliporauka, alitimka kama mtu aliyeitwa uchawini.

Akafika katika mtaa wa Ngomeni alikoishi Sindwele.

Ngomeni alipishana na majirani wa Sindwele. Mmoja wa majirani hawa alikuwa kijana barobaro mchafumchafu aliyeapa kwamba hakuwa hakutumia mihadarati.

Alisema kuwa uchafu huo alikuwa kaurithi kutoka kwa babu yake.

Sofia aliukuta mlango wa mumewe ukiwa wazi. Mwenyewe hakuwa nyumbani. Yule kijana mchafu alipoulizwa alisema kuwa hajamwona kwa siku mbili sasa.

‘Siku mbili mikonono mwa virukanjia wa Bushiangala?’ Sofia aliwaza kwa wahka. Alipojaribu kumpigia simu, simu ililia bila kuchukuliwa, hali hii ikamzidishia wasiwasi.

Aliingia kazini, akafagia nyumba ya Sindwele, akaipangua na kuipanga upya. Alikuwa akitafuta ushahidi wa uwepo wa mke mwenza. Kitu kama kiatu, kitambaa au marashi. Hakuambulia chochote. Lakini hili halikumridhisha. Isingekuwa hivyo basi Sindwele angekuwa hapa.

Na ile sauti ya mwanamke aliyejibu simu ya Sindwele je? “Piga baadaye tafadhali” sauti ile ya kike ilihuika masikioni mwake. Hiyo ‘piga baadaye’ ilimkereketa maini. Na ile ‘tafadhali’ je?

Hii ilimuudhi hata zaidi. Haikuwa tafadhali ya kuomba. Haikuwa na unyenyekevu hata kidogo.

Ilikuwa tafadhali ya kutotaka kusumbuliwa.

Almpigia mumewe simu tena kwa mara ya ngapi sijui. Hatimaye ‘mteja wa nambari’ hakupatikana tena.

Sofia akajibwaga kitandani. Hasira ilishirikiana na wasiwasi kumwondolea furaha na utulivu.

Alikumbuka dhiki alizokutishwa na mwalimu huyu. Akajiambia kwamba licha ya dhiki hizo, hakuwa na mume mwingine. Akaendelea kumsubiri.