VITUKO: Nia fiche ya Farida kumfichulia Pengo njama ya Mwinyi na Tumbo
Na SAMUEL SHIUNDU
Walifika faraghani na kuagiza chakula. Pengo hakula nyama kwa sababu za kidini. “Huu ni mwezi mtukufu wa pasaka aisee! Lazima tususie kila jambo linalotupa raha’ Hili lilimgutusha Farida.
Akatambua kuwa kakutana na mwanamume mwenye msimamo mkali wa kidini. Hakujua kama hii kauli ya Pengo kuhusu ‘kila jambo la raha’ ilihusisha pia yale yaliyomsumbua roho.
Hapo naye akaomba apewe soda baridi kwa keki. Hakutaja pombe asije akadhaniwa mhuni na muumini huyu. Hakuna mwanamke ambaye hujiachilia na kuonyesha udhaifu wake kwa mwanamume kwa mara ya kwanza. Kwake stara ilikuwa ngao iliyomsaidia kuvishinda vita vingi vya aina hii. Akajitunza na kunyenyekea.
Baada ya jambo-sijambo, Farida alimfichulia mwenzake lililowakutanisha katika mkahawa huo. Alimweleza jinsi alivyoyasikiliza mazungumzo kati ya Tumbo na Mwinyi.
“Nilisikia wakizungumzia kitu kama ‘interdiction’. Mwanzoni sikujua maana ya neno hilo. Lakini baada ya kulitafitia, nikagundua kuwa ni jambo kama, kufutwa kazi.” Farida alimfafanulia mwenzake kabla ya kuendelea, “Na anayepangiwa njama hii si mwingine ila wewe mpenzi” akampasulia mbarika hatimaye.
‘Yakoje haya masikio basi?’ Pengo alijiuliza kwa mshangao. Alijua kuwa Mwinyi hakumpenda, lakini hakujua kuwa uhasama wao ulikuwa umefikia kiwango hiki. Akameza mate machungu huku akimsikiliza Farida aliyekuwa akirogonya kama muumini aliyepandwa na roho wa ndimi, “Nilipogundua hili nikajiambia kuwa si haki kabisa!
Si haki kwa kijana mwema kama wewe kupatwa na nakama hii! Ndipo nilipoikumbuka methali ya kikwetu isemayo kuwa, asiyetahadhari hugaagaa kwenye mapito ya majitu.
Nimekuita nikujuze utahadhari kabla ya hatari. Wajua tena ilivyo vibaya kukumbwa na balaa huku mwenyewe huna habari? Wanasema wahenga kuwa, nzi asiye na mshauri huuandama mzoga hadi kaburini. Singetaka uwe nzi huyu.”
Pengo alikumbuka siku aliyokutana na huyu binti Farida kwa mara ya kwanza. Hakuwahi kufikiria kuwa angemfaa. Aliaibika kwa kumpuuza awali. “Sasa nitafanyaje maskini?” Pengo alishangaa.
Kwa kulisikia swali hili la Pengo, Farida alijiwa na matumaini ya kuvuna alilolilenga. Akampa habari nyingine nzuri. “Swala lako lilinikeshesha na kuniliza hadi kisima changu cha machozi kikakauka. Nimekwishazungumza na mkuu wa shule ya Baraka kule Sidindi. Akaniambia umwone.
Mwinyi aliposema wewe wa nini kumbe kunao wanaojiuliza watakupata lini?” Farida alimliwaza kwa misemo ya kikwao.
Pengo alimshukuru Farida kwa fadhila zake. Shilingi mia tatu zikamtoka kulipia chakula chao. Wakaagana na kuahidiana wakutane kesho yake Pengo atakaporejea kutoka Sidindi.