Makala

VITUKO: Selemani aliyeibiwa pikipiki mara mbili sasa dereva mpya wa Pengo

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMUEL SHIUNDU

SELEMANI alisemekana kuwa na mkono wa Msiba.

Lakini kwa vile mwalimu Pengo alikuwa mlokole asiyeamini mambo ya kishirikina, hakufikiwa na uvumi huu uliozunguka kote kijijini.

Alisemekana kalaaniwa na Makandawira.

Pengo alimjua Selemani kama mwendeshaji wa pikipiki maarufu kijijini. Alikuwa mwaminifu kwa wateja na waajiri. Kila mtu alimsifu kwa hili, naye kama mgema akalitia tembo maji.

Akakihama kijiji na kuelekea Pwani. Huko akaajiriwa na Makandawira.

Kama mwajiri wa Makandawira, alichapa kazi kwa uaminifu wake wa awali ili kujiaminisha kwa mwajiri huyu mpya. Akaaminiwa. Kazini akapatana na marafiki. Mmoja wa marafiki hawa alijiita Abu Nuwaz. Selemani hakujua mengi kumhusu Abu. Alilojua tu ni kwamba kijana huyu alikuwa karimu.

Hata alipomwalika kwa chamcha katika Hotel Victoria hapo Pwani, Selemani hakushuku lolote, alipoachwa hotelini na Abu aliyedai kuenda kutoa pesa kwenye mtambo wa ATM, Selemani hakushuku lolote.

Abu alipoazima pikipiki ili afike kwenye benki haraka, Sulemani hakushuku lolote. Sulemani alimngoja Abu hadi akagundua kuwa Abu kampiga chenga. Abu hakuwa wa kurudi. Selemani akakumbuka kuwa jogoo wa shamba hawiki mjini. Akahepa hotelini bila kulipa. Akamhepa Makandawira. Akautoroka mji kurejea kijijini.

Kijijini akaajiriwa na Lokotemu. Huko akapatana na rafiki aliyejiita Mjomba. Huyu hakuwa na pupa ya Abu. Mjomba alichukua muda kujiaminisha. Akamtafutia Selemani kazi nzuri nzuri kwa malipo mazuri. Siku moja naye akampeleka Selemani kwa Nafoyo na kumnunulia chai. Selemani akakumbuka masaibu aliyokutishwa na Abu. Akajiambia kuwa asingeruhusu huyo Mjomba kuenda popote na pikipiki.

Ikawa kila mara anatoka nje ya kibanda kuitazama pikipiki yake. Mjomba hakujua kuwa ingekuwa rahisi hivi. Mara tu Selemani alipoinuka kuenda nje, alitumbukiza tembe fulani kwenye kinywaji cha Selemani. Tembe hiyo ikayeyuka mara moja.

Aliporejea na kuinywa chai yake, Selemani alikumbwa na usingizi wa pono. Alilala hadi alipogutuka na kujuzwa kuwa mwenzake kaondoka na pikipiki. Ndipo ilipombainikia kuwa huyo Mjomba hakuwa mwenyeji wa pale kijijini, hakuna aliyejua alikotoka huyo Mjomba. Hakuna aliyejua jina lake halisi, alijiita tu Mjomba.

Maskini Selemani kalaghaiwa tena! Lokotemu hakuwa wa kukimbiwa, Selemani alilazimika kuuza shamba ili kufidia pikipiki ya wenyewe.

Aliponunua pikipiki, Pengo alirejea kijijini kumtafuta mwendeshaji yule maarufu.

Aliwaogopa vijana wa Sidindi ambao walisemekana kuwahini waajiri wao na kuwatumbuiza mashangingi.

Kijijini akampata Selemani. Akarejea naye mjini Sidindi. Selemani hakuhitaji kusisitiziwa kuwa makini. Akaepukana na marafiki hususan wa kiume.