VITUKO: Sindwele aingia kwenye mtego wa naibu hedimasta, hasahihishi mitihani
Na SAMUEL SHIUNDU
WALIPOFURUSHWA na Asumini, Pengo na Sindwele waliagana na kuwekeana miadi ya kukutana wakati wa likizo.
“Ulilibabaisha totoshoo lile kwa maswali yako bwana!” Sindwele alimsaili Pengo kwa jicho la umbeya na tabasamu la kihuni.
Naye Pengo hakukosa jibu.
“Tuliwahi kukutana mahali.” Pengo alimjibu mwenzake.
“Sikujua kwamba nawe hukutana na watu wa sampuli hiyo!” sauti ya Sindwele ilisheheni kejeli na hukumu.
Alivyokuwa stadi wa kuzisoma ishara, Pengo alimweleza kwa ufupi kwamba walikutana na binti huyu walipoenda Pwani kwa ziara ya shule.
“Ile moja ya Maka au nyingine?” Sindwele alionyesha kutoridhishwa na jibu la mwenzake.
“Naam, hiyo ya Maka. Wakati huo huyo Asumini alikuwa mpenzi wa Mtundio” Maelezo ya Pengo yalianza kumwelea Sindwele.
Alikumbuka Pengo alivyosalia Pwani na Bwana Mtundio. Hakuuliza zaidi. “Lakini ulimtaja na Riziki” Lile tabasamu la kihuni lilirejea usoni mwa Sindwele.
Walishauriana wakafumkane ili waende kuzikamilisha kazi za muhula wa pili.
Hayo ya Riziki wangeyazungumza baadaye.
Pengo akashika njia kuelekea Sidindi naye Sindwele akarejea shuleni Bushiangala.
“Mwalimu rundo lile la karatasi linakusubiri usahihishe. Makataa ni leo saa saba mchana” Ndiyo kauli ya naibu mwalimu mkuu iliyomkaribisha Sindwele shuleni. Simba alipotoweka, Sindwele naye akatoweka. Naibu wa Simbamwene alishuku kwamba wawili hawa walikuwa pamoja wakizifuja pesa za shule.
Hili lilitosha kumtokosa naibu huyu wa mwalimu mkuu kwa hasira. Huku kutosahihisha mitihani nako kulitishia kuvuruga shughuli za kufunga shule na kukatoa sababu nzuri ya kumhangaisha Sindwele. ‘Lazima ningurume atambue mkuu ni nani.’ Naibu wa hedimasta alijiambia.
Ubwete kazini
Alikuwa kapokea malalamishi mengi kutoka kwa wanafunzi wa Sindwele kwamba hakumakinikia kazi na kwamba alitoa alama bila kusoma majibu ya wanafunzi. Mtego ukawekwa.
Wanafunzi wa Bushiangala walikuwa na mtindo wa kuandika maswali kwa kalamu ya wino mweusi kisha majibu yake kwa kalamu ya wino wa samawati.
Mara hii wakapanga na mwalimu mkuu.
Wakaandika maswali tu, lakini wakawa na mchezo wa kubadilisha kalamu tu; swali la kwanza kwa wimo mweusi kisha linalofuata kwa wino wa samawati vivyo hivyo hadi swali la mwisho.
Sindwele alipopewa karatasi za wanafunzi, akaingia kazini.
Hakikupita kipindi kirefu, alikuwa akibisha afisini kwa naibu wa mwalimu mkuu na alama za wanafunzi.
Wanafunzi wake wamepita kama kawaida ya wanafunzi waliobahatika kufunzwa na gwiji wa magwiji kama Sindwele.
Laiti angejua kilichomsubiri humo afisini, asingeingia huko kwa tabasamu na bashasha.