VITUKO: Sindwele asaka liwazo la mvinyo Rijino baada ya kukaliwa mguu kausha ukweni
Na SAMUEL SHIUNDU
KUMBE simjui huyu mwanamke’ Sindwele alijiambia aliposhindwa kumshawishi Sofia.
Ilikuwa wazi sasa kwamba Sofia asingemrudia vivi hivi kama alivyotarajia.
‘Umdhaniaye ndiye kumbe…’ alijiwaza huku akijiondosha nyumbani kwa wakwe zake.
‘Nilifanya kosa kufikiria kwamba alikuwa tofauti.’ aliendelea kujiambia huku akipenya kwenye kibarabara kilichojizika msituni kama ushoroba na kilichopita karibu na shule ya upili ya Bushiangala.
‘Nilidhani ni mungwana, kumbe ni Mshiangala wa kawaida kama Washiangala wengine tu! Ama kweli nimemzoea tangu siku zetu za uchumba na sasa sote tunazeeka ila yeye uzee wake naona unakuja vibaya vibaya’ mawazo yaliendelea kumpita Sindwele akilini kwani aliamini kuwa maembe ndiyo yalikuwa yamemfurisha kichwa Sofia na kumfanya akatae kumsikiliza. Hakuona kitu kingine kilichoweza kumpa ujasiri wa kiasi hicho.
‘Lakini maembe ni ya muda, atakuja kujuta yakiisha.’ alijihakikishia hatimaye.
Alikuwa miongoni mwa watu waliowasuta watu wa Bushiangala kwa kuwaambia kwamba wao huringa sana kila msimu wa kuyatundua maembe.
Wasichana walio kwenye ndoa hutunduka na kujawa na kiburi.
Utawasikia baadhi yao wakisema, ‘Kwetu sijaua!’ kwa maana kwamba wangeweza kurejea huko kwao wakati wowote.
Hatua za Sindwele zilimfikisha katika baa maarufu hapo Bushiangala. Mwenye baa hiyo alikusudia kuiita Original Bar lakini matamshi haya yaliwapiga chenga wenyeji wa Bushiangala ndiposa wakaamua kuiita Rijino.
“Karibu hapa Rijino” Sindwele alikaribishwa kwa bashasha na mhudumu.
“Leo umemwacha wapi askofu?” mhudumu alimuuliza huku akimwelekeza mahali pa kukaa. “Askofu?” Sindwele hakukumbuka kuwahi kuandamana na askofu. “Ah yule mwokovu mliyekuja naye akakataa kulewa. Yule bwana soda.” Mhudumu alimjuza.
Akumbuka
Ndipo Sindwele akakumbuka kwamba alikuwa kapitia hapo na Pengo walipokuwa wanatoka kuonana na wazazi wa Sofia miezi kadhaa iliyopita.
“Waonekana kusumbuliwa na mawazo bwana wangu.
Ukifika Rijino wapaswa kujiachilia na kuyafurahia maisha. Usiruhusu matatizo ya dunia yakuvuruge akili” mhudumu alimnasihi kwa sauti legevu iliyoweza kumvutia hata kiziwi.
Japo Sindwele alijua kuwa hivi ndivyo wahudumu hawa huliwaza mteja afikaye hapo, alihisi mtulizo fulani ukimvaa, ndiposa alipoulizwa kuagiza kinywaji, alitoa agizo lililosindikizwa na tabasamu nzuri. Naye mhudumu alifyatua tabasamu iliyompenya Sindwele na kumsahaulisha kisirani cha Sofia.
“Vinywaji vya leo nitagharimia mimi. Baa ya Rijino na shule ya Bushiangala ni washiriki wa karibu.” Mhudumu alimwambia Sindwele huku akimkabidhi chupa kadhaa za Blue moon.
‘Huyu atanisaidia kumwadhibu yule Simba mla nyasi’ Mhudumu alijiambia.
“Ukihitaji chochote nijuze” alimwambia kabla ya kuwaendea wateja wengine.