VITUKO: Vya bwerere hakuna! Sindwele ahimiza Pengo kudai malipo ya ushauri nasaha
Na SAMUEL SHIUNDU
“UNAHITAJI malipo mazuri kwa kazi njema uliyofanya ndugu yangu.” Sindwele alimchokoza Pengo walipokutana katika hoteli ya Jamhuri mtaa wa Ekero.
Wawili hawa hawajatia guu lao shuleni tangu mauko ya aliyekuwa rais wa nchi yao tukufu. ‘Tutaendaje kazini huku taifa linaomboleza?’ ndivyo walipomjibu kila aliyetaka kujua ni kwa nini walikosa kufika kazini.
“Nitalipwa mbinguni kaka.” Pengo alimjuza mwenzake.
“Malipo ni papa hapa duniani, mbinguni ni hesabu tu.” Sindwele alimsisitizia Pengo.
“Ni kweli usemavyo ndugu yangu. Lakini malipo yenyewe hapa duniani na hususan hapo shuleniSidindi unatarajia yatoke wapi? Hebu wewe fikiria, walimu walezi wa mwanafunzi huyo aliyetaka kuacha shule ni wasichana wabichi waliotoka chuoni tu mwezi jana. Hata mshahara wao wa kwanza hawajaupata, sasa watapata wapi pesa ya kunilipa mimi?”
“Hakuna msichana asiye na njia ya kufidia hilo. Usiniambie kuwa hulijui hili. Lakini pia utalijuaje hili na huo wokovu wako uliokujaa. Najua hampaswi kuyajua mambo mengine, ndiposa unawahitaji watu wa dunia kama sisi tukuonyeshe mambo ya dunia hii” Sindwele alimfafanulia mwalimu Pengo.
Baada ya majadiliano marefu. Hatimaye wakaelewana kuandaa kikao ambacho kwacho, Sindwele angemwonyesha mwenzake mambo ya dunia hii. “Ni muhimu pia uwaalike hao wanadada wawili kwenye kikao chetu.” Pengo akasisitiziwa.
Siku hiyo tutahitaji tuwahi mkahawani ili tukapate kinywaji kabla ya kuonana na wenzetu hao. “Kinywaji kipi hicho mwalimu?” Pengo aliuliza kwa tahadhari. “Soda baridi itatutosha” jibu lilikuja.
Hapakuwa na shani yoyote kwa Pengo kunywa soda. Hilo kwake lilimithilika na kufa maji kwa wavuvi wa pemba, lakini soda baridi kwa sindwele…
“Sikuelewi ndugu Sindwele, sijui kama umeupokea wokovu hatimaye.” Pengo alimuuliza.
Sindwele hakuwa kaokoka kama alivyodhaniwa na Pengo. Kwa mujibu wa malezo yake, pombe haikufaa kunywewa na mtu aliyekuwa na nia ya kukutana na rafiki haswa inapokuwa kwamba rafiki mwenyewe ni wa kike.
“Mwanamume ni rahisi kupumbazwa na hawa dada zetu kutokana na ule udhaifu alioumbwa nao wa kiadamu na kisamsoni. Udhaifu huu huongezwa mara dufu na chupa ya pombe.” Sindwele alimtahadharisha Pengo.
Pengo aliridhia kwani alijua kuwa mwenzake alikuwa bingwa wa mambo haya na huenda alikuwa akidhihirisha ukweli wa ile methali kuwa aisifuye mvua kanyewa.
Wakahimizana kupatafuta mahali pazuri pa faragha kwa minajili ya miadi yao na wale wanadada wawili. Kibarua kilichokuwa mbele yao ni kuwashawishi wale dada waukubali mwito.