Vitunguu, dhahabu ambayo bei yake sasa haikamatiki
NA SAMMY WAWERU
KITUNGUU ni kati ya viungo vya mapishi vinavyotumika kwa wingi katika kila boma nchini.
Madhumuni yake yakiwa ni kuongeza ladha kwenye chakula, ukuzaji wake Kenya umeanza kunoga kutokana na kuendelea kuimarika kwa soko.
Ni dhahabu ambayo bei yake kwa sasa haikamatiki.
Kwa mfano, katika masoko mengi mijini, kwa wanunuzi rejareja (consumers) kilo haipungui Sh200.
Ann Wambui, mkulima wa zao hili eneo la Mai Mahiu, Naivasha anaungama kilimo cha vitunguu sasa kimeanza kuboreka.
“Awali, kilo ingeshuka hadi Sh20 bei ya shambani,” anasema.
Sasa, Wambui ana kila sababu ya kutabasamu anapokuza kiungo hiki kwani kwa muda sasa kilo moja bei ya shambani anakiri haijapungua Sh100.
“Wanaovuna na waliovuna kuanzia Machi, Aprili kuelekea Mei, kilo imekuwa ikichezea kati ya Sh100 hadi Sh180 shambani,” anadokeza.
Juma lililopita, kilo moja ilikuwa inanunuliwa wastani wa Sh140 – shambani.
Bei kuimarika, inatokana na mikakati ya serikali kuongeza ushuru na ada kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Rais William Ruto, mwaka uliopita, 2023, alitangaza kuwa mojawapo ya mbinu kuimarisha kilimo cha ndani kwa ndani ni kutoza ushuru bidhaa za kilimo zinazoagizwa kutoka nje, vitunguu vikiwemo.
Kenya imekuwa ikitegemea taifa jirani la Tanzania kupata zao hili ila sasa kiwango cha uagizaji kimepungua kwa asilimia kubwa.
Richard Omondi, mwanzilishi Agri-Irrigation and Solutions Africa Ltd anasema huu ni wakati wa wakulima wa vitunguu kuwekeza pakubwa katika zao hili.
Ekari moja kwa mfano, mtaalamu huyu akikadiria inazalisha kati ya tani 18 hadi tani 20, anasema mkulima ana uhakika kuingiza mapato yasiyopungua kima cha Sh1.8 milioni na bei ya sasa.
“Hapa ninazungumza kilo na wastani wa Sh140, bei ya shambani (farm gate price),” Richard anafafanua.
Vitunguu vinakomaa miezi minne baada ya upanzi.
Aidha, zao hili linafanya bora kwenye udongo wenye rutuba, Mtaalamu Richard akisema mfumo wa kisasa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji unanogesha mazao.
“Kando na vigezo vingine faafu kufanikisha ukuzaji vitunguu kitaalamu, maji ndio ni nguzo muhimu sana. Hivyo, mifumo ya kisasa kuipa mimea maji inasaidia kuongeza mazao,” anashauri.
Na si tu bora kuvilisha kwa maji, mdau huyu anasisitiza haja ya kuvimwagilia maji wakati ufaao.
Mwezi mmoja kabla ya mavuno, mkulima anashauriwa kusitisha unyunyiziaji maji kwa wingi ili visioze – yanapotuama kwenye udongo.
Kabla ya upanzi, udongo unainuliwa kuunda majukwaa mithili ya vitanda.