Makala

VITUNGUU: Wao hutumia hadi laki mbili kwa wiki

October 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA soko kubwa la Kongowea jijini Mombasa, Akilimali ilikutana na Jovin Mwalulu na Mitiso Musyoka ambao ni wafanyabiashara wanaoshirikiana kuuza vitunguu.

Marafiki hawa wawili wenye umri wa miaka 23 kila mmoja walianza kazi hii mnamo mwaka wa 2017.

Kulingana nao, huwa wananunua vitunguu vyao kutoka Tanzania na eneo la Loitoktok karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania.

Mara nyingi, huwa wanaendea bidhaa hizi katika mashamba ya wakulima wanaokuza vitunguu na kununua moja kwa moja kutoka kwa wakuzaji. Lakiniwakati wananunua kutoka upande wa Tanzania, huwa wanaagiza wafanyabiashara wa kati almaarufu mawalaka kuwachukulia zao hili haswa katika maeneo ya Moshi na Singida.

Mwalulu anasema kwamba kwa kawaida huwa wananunua vitunguu hivi kwa vipimo vya kilo na mara nyingi bei ya shambani huwa ni ya kati ya Sh30 na Sh40 kwa kilo moja.

Kila wafikapo shambani kila wiki, wao hununua vitunguu kwa wingi zaidi hadi kufikia kiwango cha kati ya kilo 3,000 na 5,000 kwa ajili ya kuwauzia wateja wao sokoni Kongowea. Ina maana kwamba kiasi kikubwa zaidi cha pesa ambazo wao hutumia kununulia vitunguu kila wiki ni Sh200,000.

Vitunguu hivi vinapofika sokoni huwa wanaviweka kwenye vifurushi vya idadi tofauti tofauti ili wateja wanapofika, wana uwezo wa kujinunulia kiasi chochote kulingana na uwezo wao wa kifedha.

Kulingana nao, wateja wao wengi ni wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya Mombasa, Kwale, Lamu na Kilifi ambao huwa wananunua vitunguu kwa wingi ili nao wawauzie wachuuzi wadogo wadogo.

Wao pia huwa wanapata wanunuzi wa moja kwa moja ambao wanahitaji kiasi kidogo tu cha vitunguu kwa minajili ya matumizi ya nyumbani.

Bw Mwalulu anasema kuwa baadhi ya maduka makubwa na hoteli za kifahari na za haiba ya juu jijini Mombasa ni kati ya wateja wao waaminifu ambao huwa wanawanunua vitunguu kutoka kwao kwa wingi.

Kwa kawaida, huwa wanauza mfuko mmoja wa kilo 13 kwa kati ya Sh750 na Sh 800 au nusu yake ya kilo sita na nusu kwa Sh400. Hata hivyo mara nyingi bei hutegemea kiwango cha vitunguu sokoni na pia msimu husika ambao huathiri sana kiasi cha uhitaji wa zao hili mara kwa mara. Vitunguu vikiwa vingi sokoni, bei hupungua kidogo na kiwango kinapopungua na uhitaji kuongezeka, bei hupanda maradufu.

Gharama ya usafirishaji wa vitunguu pia huchangia kupanda na kushuka kwa bei ya mauzo ya vitunguu sokoni kwani nyakati za mvua, huwa vigumu sana kufikisha bidhaa hizi sokoni na hili huwa na athari za moja kwa moja kwa bei.

“Mara nyingi huwa inatubidi kwendea vitungu shambani ama kuagiza kutoka Tanzania kila baada ya wiki moja au hata siku nne kwa kutegemea kiwango tunachouza katika nyakati, vipindi na misimu maalum,” anasimulia Mwalulu kwa kusisitiza kwamba mengi ya mauzo yao hutokea katika misimu ya sherehe mbalimbali miongoni mwa wakazi wa Kaunti za Mombasa, Kwale, Kilifi na Lamu.

Katika misimu hiyo ya sherehe, wao huweza kujipa zaidi ya Sh600,000 kwa wiki. Wanasema kuwa vitunguu vya Tanzania ndivyo vinavyopendwa sana na wateja wao kwa kuwa vina uwezo wa kudumu kwa muda mrefu bila ya kuharibika.

Kulingana nao, vitunguu hivi vya Red Pinnoy F1, Red Creole, Bombay Red na Texas Early Grano vinavyokuzwa kwa wingi nchini Tanzania vina uwezo wa kudumu kwa kipindi cha hadi mwezi mmoja bila ya kuharibika ikilinganishwa na vingi vya vitunguu vya Kenya ambavyo huanza kuoza baada ya wiki mbili pekee.

Baadhi ya changamoto wanazopitia ni pamoja na gharama ya juu ya usafiri ikizingatiwa ya kuwa bidhaa hizi zinatoka mbali hasa Tanzania na pia barabara nyinginezo kutopitika katika eneo la Loitoktok hususan katika misimu ya mvua.

 

Bw Jovin Mwalulu akiwa katika soko la Kongowea, Mombasa. Picha/ Chris Adungo

Gharama hii huwa inapunguza kiwango chao cha faida ikizingatiwa ya kuwa

kutokana na ushindani mkubwa sokoni, bei huwa ni ya chini mara kwa mara.

Katika nyakati za kiangazi, mavuno hufanyika kwa wingi na bidhaa hii kuongezeka sokoni na hivyo basi bei ya mauzo huteremka maradufu.

Hata hivyo, wanaeleza kuwa kuna faida nyingi zinazotokana na kazi hii, mojawapo ikiwa ni

Kujiajiri badala ya kutegemea kazi za ofisini zisizo na uhakika wa kudumu. Hii ndiyo kazi ambayo wanaitegemea kila siku na wanaijivunia kwa kuwa inawapa riziki ya kujikimu na kutimiza mengi ya mahitaji ya kimsingi ya familia zao. Wakati mwingine

kazi zinapokuwa nyingi au mmoja wao anapoendea bidhaa mashambani, huwa wanalazimika kuajiri kijana

mwingine mmoja ili kuwasaidia kuwahudumia wateja wao wasiokatika.

Wanasema kuwa kutokana na ukosefu wa kazi za kiofisi na nyinginezo za kuajiriwa, wanawashauri vijana wasichague wala kubagua kazi yoyote. Badala yake, wajitume maradufu na wajitahidi katika kazi ambazo zinaonekana kuwa ni za kiwango cha chini kwani pia zina uwezo wa kumwinua mtu kiuchumi.