Makala

Vivukio vya barabara vilivyogeuka maficho ya wahalifu

January 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

WAPITANJIA kwa miguu katika barabara kuu ya Thika – Nairobi, almaarufu Thika Super Highway wameomba kuwekewa mataa ya Mulika Mwizi, katika sehemu zenye vivukio ili kuimarisha usalama wao nyakati za usiku.

Vile vile, wachuuzi wa bidhaa rejareja katika vivukio eneo la Mlolongo na Kasarani wamekiri kuwa mateka wa wahuni wanaowapora wakiwa wamejihami kwa visu.

Barabara ya Nairobi-Nakuru, eneo la Kinoo, Uthiru, na Kangemi, bila kusahau Mombasa Road, visa vya aina hiyo vya uhalifu vimeripotiwa.

Tulizungumza na Isaack Monari mkaazi wa South B, ambaye mara kwa mara hutumia mojawapo ya vivukio vinavyounganisha mtaa wa mabanda wa Mukuru, na analalamikia utovu wa usalama.

Anasema wasafiri wasiomiliki magari ya kibinafsi huwa wanahatarisha maisha yao kutumia vivukio kutoka barabara kuu ya Mombasa, vinavyowaunganisha na makazi yao.

Kulingana na Monari, wahalifu hutumia vivukio kama sehemu zao rasmi za kupumzika.

Pia, biashara za mihadarati huwa zimenoga na hutumika kama maficho yao pindi giza linapoingia.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/habari-mseto/washukiwa-43-wa-uhalifu-makadara-wakamatwa

aMaeneo haya hayapitiki, labda kwa maafisa wa usalama ambao hupiga doria – ambao wamejihami kwa zana za kazi.

“Kwa wengi ni afadhali kutumia barabara kuu ambapo tunapishana na magari badala ya kujipeleka kwa mtego,” anasema.

Anasikitika vivukio Mombasa Road ndivyo hatari zaidi, giza linapobisha hodi.

Anasema wahalifu hutembea huru huku wakijipiga kifua kwa kile wanachodai kuwa ni ngome zao.

Eneo la Railways, mzunguko wa kuingia jijini Nakuru hali ni kama hiyo.

Msanii mmoja wa nyimbo za injili kutoka Nakuru ambaye hakutaka kutambulika anasema, usalama wa kivukio hicho ni wa kutiliwa shaka kwa sababu ya idadi kubwa ya vijana wanaorandaranda mitaani wanaotumia eneo hilo.

Mbali na kuwa karibu na kituo cha Poilisi cha Railways, wakazi wamekuwa wakivamiwa na kuibiwa simu na hata pesa.

“Biashara nyingi karibu na hapa hufungwa mapema kuanzia mwendo wa saa kumi na mbili jioni kwa hofu ya kushambuliwa na kuibiwa mali zao,” asema.

Aidh, shughuli za waendeshaji bodaboda huwa zimefungwa jambo linalofanya magari yasiwashushe abiria katika sehemu yenyewe.

Mwaka wa 2021, wakazi wa Pwani walisusia kutumia madaraja ya barabara kuu wakilalamikia kuhangaishwa na vijana wa kurandaranda mtaani ambao wamegeuka kuwa wahalifu.

Wakazi hawakuona umuhimu wa kutumia barabara zenyewe na hivyo basi hawakujali ikiwa watagongwa na magari au la.