Waathiriwa wakumbuka wapendwa wao Israeli ikiadhimisha miaka miwili tangu shambulio la Hamas
MAMIA ya Waisraeli walijitokeza kuwakumbuka wapendwa wao waliouawa, huku taifa hilo likiadhimisha miaka miwili tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7.
Katika kumbukumbu ya miaka miwili tangu mauaji ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Kundi la Hamas nchini Israeli, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito wa kusitisha vita vya Gaza.
“Kuna haja mapigano hayo yasitishwe haraka iwezekanavyo kwani yameleta maadhara na hasara,” akasema Guterres.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa pendekezo jipya la Rais wa Amerika, Donald Trump, linatoa fursa ya kumaliza mgogoro huo ikiwa ni baada ya miaka miwili ya mauaji.
Oktoba 7, 2023, wapiganaji wa Hamas na makundi mengine ya Kiislamu walitekeleza mauaji mabaya zaidi katika historia ya Israeli, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 kutekwa nyara.
Haya yanajiri huku wajumbe kutoka upande wa Hamas na Israeli wakiendelea na mazungumzo ya amani yalioanza Jumatatu nchini Misri.
Juhudi hiyo inafanyika wakati Trump akisema kuwa kundi la wapiganaji wa Kipalestina liko tayari kufanya maridhiano kuhusu mapendekezo yake ya makubaliano ya amani.
Kwa faragha na chini ya ulinzi mkali, wajumbe walitarajiwa kuzungumza kupitia wapatanishi kati ya pande hizo, ikiwa ni wiki chache tu baada ya Israeli kujaribu kuwaua wajumbe wakuu wa Hamas katika shambulio la Qatar.
Shirika la habari katika nchi hiyo awali liliripoti kuwa wajumbe walikuwa wakijadili maandalizi ya mazingira ya kuachiliwa kwa mateka na wafungwa.
Taarifa ilisema, “Upatanishi wa Misri na Qatar unaendelea ipasavyo na pande zote mbili kuanzisha utaratibu wa kuwaachilia mateka walioko Gaza kwa kubadilishana na Wapalestina walio magerezani Israeli.”
Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kuwa alikuwa “na uhakika” kuwa makubaliano ya amani yanawezekana.
Aidha katika kipindi cha kumbukumbu hiyo pia Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameonya kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.
Mwanadiplomasia Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Kardinali Pietro Parolin, amelaani vikali “mauaji” yanayoendelea Gaza na kusema ni jambo “lisilokubalika” hasa kupuuza idadi ya vifo huko kwa kuzona kama athari zitokanazo kandoni mwa vita.
Parolin alisema vita kati ya Hamas na Israel “vimesababisha madhara makubwa na ya kikatili”, akiongeza kuwa ameguswa sana na idadi ya vifo vya kila siku miongoni mwa Wapalestina, wakiwemo watoto wasio na hatia.