Makala

Wabunge, maseneta kuvutana kuhusu mgao wa fedha kwa serikali za kaunti

Na CHARLES WASONGA October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MIVUTANO mipya inatarajiwa kutokea kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti baada ya maseneta kutupilia mbali pendekezo la kupunguzwa kwa mgao wa bajeti kwa serikali za kaunti kwa kima cha Sh20 bilioni.

Mnamo Agosti 8, 2024 Bunge la Kitaifa liliifanyia marekebisho Mswada wa Ugavi wa Fedha Mapato kati ya Serikali Kuu na Serikali za Kaunti (Division of Revenu Bill) wa 2024 kwa kupunguza mgao wa kaunti kutoka Sh400.1 bilioni hadi Sh380 bilioni.

Wabunge walitekeleza marekebisho hayo kulingana na pendekezo la Rais William Ruto lililotokana na kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 ambao serikali ilitarajia kuutumia kukusanya mapato ya kima cha Sh342 bilioni.

Lakini mnamo Alhamis, maseneta 28 walipiga kura ya kudumisha mgao wa awali wa Sh400.1 bilioni kwa serikali za kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2024/2025.

Maseneta walifikia uamuzi huo baada ya mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Bajeti Ali Roba kupendekeza mabadiliko ya kudumisha kiwango cha mgao wa kaunti kuwa Sh400.1 bilioni.

Hata hivyo, Bw Roba alipendekeza kuwa mgao wa serikali ya kitaifa upunguzwe kutoka Sh2.6 trilioni hadi Sh2.2 trilioni.

“Kamati ya Seneti kuhusu Bajeti imeondoa pendekezo kwamba panapotokea upungufu katika ukusanyaji wa mapato, serikali ya kitaifa na ile ya kaunti zitagawana punguzo hilo kwani hilo haliwezekani,” akasema Seneta huyo wa Mandera.

Mnamo Agosti 2024, Rais Ruto aliwasilisha taarifa katika Seneti akiiagiza kuufanyia mageuzi Mswada wa Ugavi wa Mapato ili kupunguza mgao kwa kaunti kutoka Sh400.1 bilioni hadi Sh380 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

Kiwango hicho cha mgao kiko chini ya kiwango cha mgao kwa kaunti katika mwaka uliopita wa kifedha wa 2023/2024 ambapo serikali 47 za kaunti zilitengewa Sh385 bilioni.

Mnamo Septemba Baraza la Magavana (CoG) na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) zilipinga pendekezo la kupunguzwa kwa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti kutoka Sh400.1 bilioni hadi Sh380 bilioni, kwa misingi kuwa hatua hiyo itaathiri shughuli za utoaji huduma

CoG ilisema kuwa tayari serikali za kaunti zilikuwa zimeandaa bajeti zao kwa misingi ya mgomo wa Sh400.1 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

Kabla kwa kufikiwa kwa kiwango hicho cha Sh400.1 bilioni, Seneti ilikuwa imependekeza kuwa serikali za kaunti zipate Sh415.9 bilioni huku magavana wenyewe wakipendekeza Sh439.5 bilioni.

Mnamo Septemba 2024, Waziri wa Fedha John Mbadi alikuwa na wakati mgumu kuelezea wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha kuhusu sababu ya serikali kupunguza Sh20 bilioni kutoka kwa mgao asilia wa fedha kwa kaunti.

Bw Mbadi aliwaambia kuwa hali hiyo ilisababishwa na kushuka kwa kiwango cha mapato kuwa Sh346 bilioni kufuatia maandamano ya Gen-Z yaliyochangia kuzimwa kwa Mswada wa Fedha wa  2024.

Uamuzi wa Seneti wa kudumisha mgao wa Fedha kwa Serikali za Kaunti kuwa Sh400.1 bilioni sasa unaashiria kuwa kutaundwa kamati ya upatanisho kusaka muafaka kuhusu suala hilo.

Kamati hiyo itashirikisha wabunge wanne kutoka Bunge la Kitaifa na maseneta wanne kuwakilisha Seneti.