Wachafu wakatazwa kufika Lamu
Wanafanya hivyo kwa sababu kwa zaidi ya miaka 700, Lamu imebeba hadhi kubwa duniani.
Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliorodhesha Mji wa Kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo machache duniani yanayotambulika kote duniani kwa kuhifadhi mila, tamaduni na desturi za jadi, karne na karne–yaani Unesco World Heritage Site.
Haya yote yalitokana na jinsi wenyeji wa Lamu, ambao ni Waswahili wa asili ya jamii ya Kibajuni, walivyoamua kuzibeba au kuzihifadhi tamaduni zao hadi kwenye ulimwengu wa leo wa karne ya 21.
Mbali na jamii kufaulu katika kuzihifadhi tamaduni zao, suala jingine lililochangia Mji wa Kale wa Lamu kuvalishwa taji na Unesco ni jinsi mji huo wa kihistoria unavyodumisha usafi.
Kwa wakazi wa Lamu, wadogo kwa wakubwa, vijana kwa wazee, ni desturi kwao kuwaona wakibeba magunia au vikapu baharini, sio kwamba wanatafuta samaki, bali kukusanya taka za kila aina zinazochafua fukwe zao za Bahari Hindi.
Kwao, wanaamini kuwa usafi ni nguzo muhimu katika kudhibiti hadhi ya kisiwa cha Lamu, ikiwemo ile ya Unesco.
Huku sehemu nyingine za nchi na ulimwengu zikisubiri siku maalum, iwe ni ile ya Maadhimisho ya Usafi wa Fukwe za Bahari au Pwani, Siku ya Utalii Duniani au ile ya Mazingira Duniani, ambazo zote huadhimishwa tarehe tofauti tofauti za mwezi Septemba kila mwaka, kwa wakazi wa Lamu mambo ni tofauti kwani kila siku kwao ni muhimu katika kuhakikisha usafi wa mazingira ya mji na fuo za Bahari Hindi unadumishwa.
Na ndio sababu kwa yule ambaye hughairi kushiriki shughuli zozote zinazofungamana na usafi wa kisiwa hicho, huchukuliwa au kuonekana na wanakisiwa kama adui mkubwa kwao.
Mzee Abdalla Omar,71, mmoja wa wazee wa Mji wa Kale wa Lamu, anasema tangu udogoni mwake, yeye ameshuhudia wazazi wake wakishiriki shughuli ya usafi wa mji na fukwe.
Anasema hulka ya usafi waliirithi kutoka kwa mababu zao, hasa baada ya kujulishwa faida zinazoambatana na tabia hiyo.
“Kumbuka jamii yetu ya Wabajuni Lamu imejikita sana katika uvuvi kujiendeleza kimaisha. Taka kama plastiki zikitapakaa ufuoni au kuelea baharini huhatarisha maisha ya viumbe hai, ikiwemo samaki. Plastiki ni sumu kwa samaki, kumaanisha wakifa jamii yetu haina ajira. Na ndio sababu tunajikaza kila mmoja, mdogo kwa mkubwa, kusafisha fukwe zetu mara kwa mara,” akaeleza Bw Omar.
Unapotembea kwenye ufuo wa Shela, kisiwani Lamu, mara nyingi utakutana na vigunia vilivyotundikwa kwenye maeneo maalum kwa minajili ya mja kutupa taka zake.
Hapa pia utajipata kuwa adui au mkiukaji sheria na hata kukamatwa endapo utaendeleza vijitabia vyako vya kurusha taka kiholela.
Kwa anayezuru upande huo wa kisiwa cha Lamu, lazima kuzingatia nidhamu, ikiwemo kujumuika na wenyeji katika kuusafisha ufukwe na kuuacha ukimeremeta metumetu.
Hapo ndipo utafaulu kuujenga urafiki na wanajamii.
Bw Ali Ahmed anasema kisiwa cha Lamu, iwe ni kwenye Mji wa Kale wa Lamu au Shela ni ngome kuu za watalii wanaozuru Lamu.
Anasema ili kudhibiti hadhi hiyo, usafi lazima uzingatiwe.
“Mbali na watu wetu kujipatia riziki kupitia uvuvi baharini, pia utalii ni kitega uchumi kwetu. Sekta zote zinategemea sana usafi wa mazingira. Kuufaidi uvuvi lazima bahari yetu iwe safi. Kwa upande mwingine, kuufurahia utalii ni lazima mazingira yetu ya fukwe na nchi kavu yawe safi. Na hilo nikumaanisha kwa anayechafua mazingira basi ni adui mkubwa wa jamii yetu,” akasema Bw Ahmed.
Kwa upande wake, Bi Maryam Athman, anataja kisiwa cha Lamu kuwa ngome ya dini ya Kiislamu, hivyo unadhifu ni nguzo muhimu kwa jamii hiyo.
Bi Athman anashikilia kuwa usafi wa Lamu lazima uwepo kutokana na kuwepo kwa waumini wa dini ya kiislamu eneo hilo.
Anafafanua kuwa Uislamu kwa jumla ni usafi na kwamba ni wajibu wao kama Waislamu kuuzingatia usafi, si wa mazingira yao tu bali pia yale ya mwili nakadhalika.
Anasema Uislamu unahimiza au kukumbusha waja kwamba katika maisha usafi ni kipimo tosha kwa wenye akili na wale punguani.
Wenye akili lazima waishi mahali nadhifu ilhali wendawazimu mara nyingi utawapata kwenye majaa.
“Na ndio sababu hapa Lamu tunajikaza kuishi kwenye mazingira nadhifu tukijua fika kuwa dini yetu tukufu ya uislamu inaweka wazi suala zima la usafi kuwa alama mojawapo katika alama za imani. Yaani usafi ni nusu ya Imani,” akasema Bi Athman.
“Hii ina maana kwamba Mwislamu ambaye mwili, nyumba, chumba na mazingira yake kwa jumla ni machafu kabisa huyo ana uchache wa imani.”
Mbali na uzoefu wa jadi wa jamii, kudhibiti sekta za kiuchumi na kuzingatia dini, usafi pia ni kiungo muhimu, hasa katika kuidhibiti hadhi ya Unesco iliyokabidhiwa Mji wa Kale wa Lamu zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Kwenye mahojiano ya awali na Taifa Leo, Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kitaifa ya Unesco, Mipango na Utamaduni, Bw Julius Mwahunga, alieleza wasiwasi wake kuhusiana na athari za Uchauzi wa Mazingira zinazoandama Mji wa Kihistoria wa Lamu ambazo huenda zikahatarisha au kusababisha kushushwa hadhi kwa mji huo na Unesco.
“Kuna ongezeko la uchafuzi wa mazingira kisiwani hapa na kwenye fuo za Pwani kwa jumla. Ni wajibu wa wakazi, mashirika na wadau wengine kuja pamoja na kujizatiti kusafisha mazingira na kujiepusha na uchafuzi ili hadhi ya Mji wa Kale wa Lamu isiathirike,” akasema Bw Mwahunga.
Kisiwa cha Lamu kinachojumuisha Mji wa Kale wa Lamu, Shela, Kashmir, Hidabo, Kandahar, Bombay, India, Makafuni, Matondoni na Kipungani, ni makazi ya zaidi ya watu 30,000.