Wahisi uchovu kwa kukosa kazi nzito
NA KALUME KAZUNGU
MAHAMALI, wavunjaji mawe na vibarua wengine wanaotegemea kazi nzito za kuchosha zinazohitaji nguvu nyingi, sasa wanasema wao huhisi uchovu wakikosa kazi hizo.
Bw Elisha Hiribae, ambaye ni hamali katika kisiwa cha Lamu, anasema yeye mara nyingi amejipata kushinda akifanya kazi, akibeba mizigo hii na ile, kuzunguka hapa na pale ilmuradi aepuke uchovu mwilini mwake.
Kwa Bw Hiribae, kazi yake ya uhamali inayohusisha sana yeye kubeba mizigo mizito na kushiriki au kuzitekeleza kazi za sulubu kila kuchao ni afueni kwake kuliko kukaa bure bwerere.
Anafichua kuwa wakati anapojipa wasaa wa kupumzika na kupiga funda la maji, yeye huhisi uchovu na maumivu mengi kinyume na anapokuwa kazini.
Kazi ya Bw Hiribae huhusisha yeye kuamka alfajiri na mapema, kushinda mchana kutwa akifanya kazi na kulala usiku wa manane.
Kisa au hali ya Bw Hiribae inawakilisha maelfu ya mahamali na watu wengine wengi wanaozifanya kazi ngumu maishani katika harakati zao za kulisaka tonge.
Wengi wa waliozoea kazi nzito waliohojiwa na Taifa Leo walidai punde wanapokosa kuinua au kubeba na kusafirisha mizigo mizito basi huhisi uchovu ilhali wengine hata wakiishia hospitalini kutazamwa na madaktari wakijihisi kuwa wagonjwa walio hoi kabisa.
Bw Jacob Bokoro,40, ambaye ni mchimba mawe ya kujengea kwenye migodi ya Manda-Maweni, kaunti ya Lamu, anasema yeye huitekeleza kazi hiyo ya sulubu karibu kila siku kuanzia asubuhi hadi jioni.
Bw Bokoro hufika kwenye machimbo ya mawe ya Manda-Maweni saa kumi na moja alfajiri kila siku, ambapo hutumia sururu, upanga, mwiko na shoka kupasua na kuyachonga mawe, kazi ambayo humlazimu kuondoka machimboni na kurudi nyumbani usiku.
Kwenye migodi ya Manda-Maweni, ardhi huwa ni ngumu si haba.
“Mwili wangu ninapokaa bila kazi huuhisi kuwa mzigo mzito kwangu. Mwili huniuma sana. Na ndiyo sababu nikachagua kwamba heri nifanye kazi kila siku ya wiki kuanzia Jumapili hadi Jumapili inayofuata. Hilo hunipa nafuu kwani huwa sihisi maumivu ya mwili ya sana,” asema Bw Bokoro.
Sila Njenga, ambaye ni msukuma rukwama mjini Lamu, anasema anapoacha kufanya kazi hiyo ngumu kwa masaa machache hujihisi mchovu na usingizi kumwandama.
Bw Njenga ambaye ni baba wa watoto watatu, pia anashikilia kuwa kuna heri kufanya kazi kuliko kukaa bure.
“Ni kama hizi kazi ngumu tunazozifanya zimeigeuza miili na misuli yetu kuwa ni yenye kuzoea mashaka. Punde tunapoipumzisha miili yetu basi mavune yote huamka, hivyo kuhisi kuumwa na mwili, kunyong’onyea na kutaka tu kulala,” asema Bw Njenga.
Mavune ni maumivu ya mwili yanayotokana na uchovu, hasa baada ya kufanya kazi za sulubu.
Je, wataalamu wa afya wana lipi la kuchangia kuwahusu binadamu hawa wanaofanya kazi nzito au kupitia ugumu wa maisha karibu kila siku?
Dkt Chris Marjan wa kisiwa cha Lamu anasema sababu kuu ya binadamu kuhisi kuchoka hata pasipo kutekeleza kazi au kuushughulisha mwili katika jukumu lolote inatokana na kwamba wahusika hawalali vya kutosha.
Dkt Marjan anasisitiza kuwa kutopata mapumziko ya kutosha kila siku, ikiwemo kujipa wasaa wa kulala, kunaweza kusababisha maumivu hayo ya viungo vya mwili.
Anasema kuna baadhi ya watu ambao huishia kuwangwa na kichwa mbali na maumivu mengine ya mwili wanapopumzika kidogo kwa kulala pasipo kutosheka.
“Hawa wenzetu huamka asubuhi sana kutekeleza majukumu yao siku nzima mfululizo hadi kufikia jioni kabisa. Wao hawajatenga muda wa kutosha wa kupumzika ipasavyo. Kutolala vya kutosha kwenyewe tayari ni ugonjwa tosha kwani mja mwishowe huishia kuwa mwenye hasira na kukosa umakinifu,” asema Dkt Marjan.
Sababu nyingine zinazomfanya mtu kuhisi kuchoka kila mara ni jinsi ambavyo kazi zenyewe, hasa zile za mahamali, huhusisha mwili (maungo) na akili kwa wakati mmoja.
Bi Susan Wakesho, ambaye ni daktari wa mifupa na ushauri, anatoa mbinu kadhaa za waja, hasa wale wanaotekeleza majukumu magumu kufanya ili kuepuka uchovu wa kila mara mwilini.
Anasema ni vyema binadamu kujitengea muda wa kutosha wa kupumzika na kulala, hasa usiku.
Hilo litamsaidia kuzirejesha upya nguvu za mwili zilizopotea.
“Kweli fanya kazi lakini mwisho wa siku hakikisha unajitengea muda wa kutosha wa kupumzika na kulala usiku. Tenga angalau masaa saba au tisa yawe ni ya kulala kila usiku. Mwili utapata mapumziko ya kutosha na kuzirudisha upya nguvu,” ashauri Bi Wakesho.
Anatoa ushauri kwa waja pia kudhibiti masaa wanayotumia kukaa wakitazama televisheni kwani mwangaza wa bluu (samawati) unaotolewa na kioo cha runinga waweza kutatiza usingizi wao.
“Ukipumzika vya kutosha inamaanisha mwanzo wa siku yako utakuwa wewe una nguvu mpya,” asema.
Pia anawashauri wanaojihusisha na kazi nzito au za sulubu kudumisha hulka ya kupumzikapumzika kila mara katikati ya kazi.
Anasema dakika chache za mapumziko zinasaidia kurejesha nguvu, hivyo kukusaidia kudumisha umakinifu kazini.
Mbinu nyingine za kuepuka au kuzuia uchovu wa mwili wa mara kwa mara ni kuzingatia lishe bora.
Dkt Wakesho anasisitiza haja ya mtu kula matunda, mboga, nafaka na pia vyakula vya protini kama vile samaki na kuku kwa wingi.
Pia anashauri waja kunywa maji na vitu oevu kwa wingi kila mara wanapotekeleza majukumu yao ya siku.
“Mimi hushauri watu kunywa angalau glasi nane hadi 10 za maji kwa siku,” asema.
Kufanya mazoezi ya mwili kila mara hupunguza uchovu na kuhamisha kabisa msongo wa mawazo ambao pia ni changizo cha mwili kuchoka.