• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 1:12 PM
Wahubiri sauti ya mnyonge

Wahubiri sauti ya mnyonge

NA WANDERI KAMAU

JE, unawafahamu viongozi wa kidini waliowahi kujitokeza na kuwa watetezi wa raia dhidi ya tawala zilizopo bila kuogopa lolote?

Unaweza kuwakumbuka?

Hali hiyo iliibuliwa Jumapili na Askofu Norman King’oo wa Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Machakos, alipojitokeza wazi na kuilaumu serikali ya Kenya Kwanza kutokana na kile alidai ni kupanda kwa gharama ya maisha nchini.

Akiwaongoza mamia ya washirika wa kanisa hilo kwenye ibada ya misa mnamo Jumapili katika eneo la Matungulu, Machakos, Askofu King’oo alitaja ufisadi kuwa chanzo kikuu cha matatizo ya kiuchumi na gharama ya juu ya maisha inayoikumba nchi kwa sasa.

“Hali ya umaskini inapoendelea, hasa miongoni mwa vijana, hatutawahi kuwa na amani. Tunaweza kuendelea kujenga kuta za stima katika makazi yetu, lakini hatutawahi kuwa na amani. Lazima utawala uliopo uwakomboe raia kutoka kwa utumwa huu wa umaskini,” akasema Askofu King’oo.

Kauli yake imeibua kumbukumbu za viongozi wengine wa kidini wanaokumbukwa kwa kauli zao kali dhidi ya serikali kutokana na sera zake za kuwahangaisha raia.

Baadhi ya viongozi hao ni Kasisi Sammy Wainaina wa Kanisa la Kianglikana Kenya (ACK), Kasisi Mstaafu Timothy Njoya wa Kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA), Askofu Anthony Muheria wa Dayosisi ya Nyeri, maaskofu (marehemu) David Gitari, Alexander Muge kati ya wengine wengi.

Askofu Sammy Wainaina amejizolea sifa kwa kuwa mtetezi mkuu wa wanyonge katika kizazi hiki cha viongozi wa makanisa waliopo. Amekuwa sauti kuu ya kuwatetea wanyonge tangu wakati wa serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Mnamo 2021, Dkt Wainaina aliwalaumu Bw Kenyatta na Rais William Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais), kwa kuongeza taharuki ya kisiasa nchini kutokana na tofauti za kisiasa walizokuwa nazo.

Alisema kuwa Kenya ilikuwa kwenye hatari ya kukumbwa na mapigano ya kisiasa na kikabila, kutokana na taharuki iliyokuwepo kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mnamo Desemba, alimlaumu vikali Rais Ruto kutokana na kiwango cha juu cha ufisadi katika serikali yake. Pia, alimlaumu kwa kuendelea kuwatoza Wakenya kiwango cha juu cha ushuru, akisema Rais alikuwa akienda kinyume na ahadi alizotoa kwa raia.

“Wao (Kenya Kwanza) walikuwa sehemu ya serikali iliyopita. Waliilaumu kuwa kuwatoza Wakenya ushuru wa juu. Wao wanafanya nini? Ushuru wao hata uko juu zaidi! Wakati bei za bidha zinashuka katika sehemu tofauti duniani, zinaendelea kupanda hapa Kenya!” akasema.

Dkt Njoya anakumbukwa kwa ukosoaji mkubwa ambao alikuwa akiielekeza serikali ya Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi, kutokana na vitisho ilivyokuwa ikiwaelekeza viongozi wa upinzani na kidini waliokuwa wakiikosoa.

Licha ya umri wake mkubwa, bado amekuwa akiendeleza uanaharakati wake, hasa katika mtandao wa ‘X’.

Askofu Muheria pia amekuwa akiilaumu serikali ya Kenya Kwanza, hasa kutokana na baadhi ya sera zake, kwa mfano sakata ya wizi wa mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) majuzi.

Askofu Muge alifariki katika hali tatanishi mnamo Agosti 1990, siku chache baada ya kuonywa na waziri mmoja katika serikali ya Rais Moi “kutokanyanga Busia”. Hata hivyo, alikaidi agizo hilo. Anakumbukwa kwa kuwa mkosoaji mkuu wa serikali hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Familia zahangaishwa na ‘ugonjwa’ wa wazee kupotea...

Valentino: Wanaume wenye mabibi wengi wataka hakikisho SHIF...

T L