Makala

Wajakazi walia kunyimwa WiFi na waajiri wao wakishukiwa kuingia TikTok kujipeperusha

Na FRIDAH OKACHI July 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAJAKAZI wanalalamikia kunyimwa WiFi na waajiri wao, wakidai hutumia kuwasiliana na familia zao wakati wa dharura.

Wajakazi hao wametaja kunyimwa kutumia WiFi kuwa unyanyasaji kwa kuwa hufanya mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp.

Bi Jackline Kanaiza aliambia Taifa Leo Dijitali ametoa huduma zake kwa mwajiri wake miezi minane japo anakumbwa na changamoto ya kuwasiliana naye kwa kukosa salio kwenye simu yake.

Bi Kanaiza alieleza kuwa kwa wakati mmoja, bosi wake alibadilisha neno la siri la WiFi na kumnyima kutumia.

“Hapa nyumbani kwa bosi wangu, WiFi ndio inatumika kwenye televisheni na simu. Na huwa natumia simu kuwasiliana naye. Sasa hivi nalazimika kununua ‘bundles’ kila wakati baada ya bosi kubadilisha neno la siri,” alianza kueleza Bi Kanaiza.

Binti huyo mwenye umri wa miaka 28, alilalamika akihisi kunyanyaswa kwa kununua salio wakati wa dharura.

“Kuna wakati alifika nyumbani na kudai kuwa natumia WiFi sana kisha kubadilisha. Nilipomuuliza itakuwaje kuwasiliana naye wakati wa dharura, aliniambia kuwa atakuwa ananunua salio jambo ambalo hajatekeleza,” alilalama Bi Kanaiza.

Hata hivyo Bi Kanaiza alikana madai ya kutumia WiFi kwa njia isiyofaa.

Katika mtaa wa Eastleigh, Taifa Dijitali ilikutana na Josephine Nekesa, 27, ambaye anatoa huduma za ulezi na nyumbani. Bi Nekesa, alisema hutumia WiFi kuangalia matukio yanavyojiri nchini kupitia mitandao ya kijamii.

“Wengi wa mabosi hufikiria kuwa hatufai kutumia WiFi zao. Lakini nimepewa ruhusa kuitumia. Mwajiri wa kwanza alinizuia wakati mmoja baada ya kunipata kwenye mtandao wa TikTok,” alisema Bi Nekesa.

Bi Wanjiru naye alimtaja mwajiri wake wa kwanza kumbagua kwani aliwawekea neno la siri la WiFi kwa simu za wanawe na kuwaonya wasimpe.

Alisisitiza kutotofautiana na familia yake kwa kumfanyia kazi za nyumbani na kuipa ulinzi nyumba yake.

 “Sisi ni binadamu kama wale wengine. Sisi huchukuliwa ni kama tuna mapungufu kwa kufanya kazi iliyo na mishahara ya Sh5,000 hadi Sh9,500 kulingana na ukubwa wa nyumba na watoto. Mwajiri wa kwanza alikuwa akizima televisheni asubuhi na kwenda kazini,” alisema Bi Nekesa.

Baadhi ya waajiri wamelalamikia wajakazi wao kutumia WiFi kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kusahau kutekeleza majukumu ya nyumbani.

Celestine Wanja, aliye na watoto watatu alisema kwa wakati mwingi amekuwa akipata ujumbe wa kumfahamisha kuwa mjakazi wake yupo mtandaoni wa TikTok akijipeperusha kwa njia ya moja kwa moja.

“Si mara ya kwanza au pili nimepokea ujumbe wa kuniarifu. Nikifika nyumbani napata kuna kazi ambazo hajafanya. Fikra za kuondoa WiFi nyumbani hunijia kila wakati lakini naona niwache,” alisema Bi Wanja.