Makala

Wajawazito waambiwa kuna Sh5,000 za bure!

January 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Mathioya Edwin Mugo amezindua mradi wa kumtuza kila mwanamke mjamzito katika eneo lake Sh5,000 kama hamasisho la umuhimu wa watu kuzaana.

Bw Mugo alisema kwamba furaha ya viongozi ni kuona watoto wakiongezeka ndipo “tujihakikishie kizazi cha kesho yetu”.

Akiwa katika wadi ya Kamacharia mnamo Jumatano kwa hafla ya kutoa ufadhili wa kupeana chakula kwa walemavu na wanyonge wengine mashinani, Bw Mugo alisema uongozi wake utakuwa wa kujali masilahi mbalimbali “yakiwemo hayo ya uzazi kwa idadi zetu”.

Katika hali hiyo, alisema kwamba hata wale waliojifungua katika kipindi cha miezi sita iliyopita watapokezwa kishawishi cha Sh1,000 kila mmoja ili watamani kurudia uzazi tena.

Katika hafla hiyo, mbunge huyo aliwapanga kwa foleni kina mama wajawazito na akawapokeza mabunda ya hela, nao wengine walio na watoto wa umri wa chini ya miezi saba wakitengewa foleni yao.

Mbunge wa Mathioya Edwin Mugo akimshika mtoto wa mwanamke aliyejifungua ambapo pia alimpokeza kila aliyejifungua kwa kipindi chini ya miezi saba, takriban Sh1,000. PICHA | MWANGI MUIRURI

Hii si mara ya kwanza kwa viinua mgongo vya aina hii kutolewa.

Mbunge wa Maragua Mary Wa Maua amekuwa akitoa Sh1,000 kama zawadi kwa wajawazito.

Naye Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata alitenga bajeti ya kaunti kuwapa walio na mimba kiinua mgongo cha Sh6,000 kila mmoja.

Baadhi ya wataalamu husuta njama hizo za kuchochea wanawake kukimbilia kupachikwa mimba na waume wao ili kupokea pesa hizo, wakifananisha na hongo.

Wenye mtazamo huo hushikilia kwamba wanasiasa wanafaa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wenyeji kuhusu manufaa halisi ya upangaji uzazi.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya uzazi eneo hilo By Lucy Kamau, ni wajibu ya wenyeji kujua kwamba kuzaa mtoto ni mkataba wa miaka mingi.

“Matunzo ya mtoto yanahitaji rasilimali nyingi na hizo Sh5,000 au hiyo Sh1,000 si kitu,” akasema Bi Kamau.

Alisema malipo hayo yanaweza yakatumiwa vibaya hata na watoto wa shule ambao watafikiria Sh5,000 ni pesa nyingi na wakizisaka, wajiingize kwa mtego wa mimba za mapema.

“Suala la kujiuliza ukiwa mwenyeji ni kwa nini hao wanaokupa pesa hizo uzae, ni matajiri lakini wao wenyewe huzaa watoto wawili au watatu pekee. Sasa wanakushinikiza kupitia vishawishi vya pesa wakitaka uzae makumi ya watoto,” akaongeza.

Bi Kamau alishikilia kwamba “msimamo wetu ni familia iwe na watoto ambao itaweza kugharamia mahitaji”.

Alisema kwamba raia wa kipato cha chini asipokuwa makini, anaweza kujipata katika mtego wa kuzaa tu watoto kiholela ambao hataweza kuwalisha na kuwasomesha.

Hapo, alisema hali inayojitokeza ni ya familia za maskini watumwa wa kutegemea familia za matajiri kwa lishe nao hao wachochole wakiwanufaisha wanasiasa kwa kura.

Bi Kamau alilalamika kwamba “huu mtazamo wa kuchochea watu maskini wazae watoto wengi umekumbatiwa hata na wazee ambao mtazamo wao ni kwamba idadi ya Agikuyu inafaa kubakia ya juu kuliko ya jamii nyingine”.

[email protected]