Wajua unaweza kaa kwenye ndoa na bado uhisi upweke?
KATIKA jamii yetu, wengi huamini kuwa kuingia kwenye ndoa ni sawa na kupata rafiki wa karibu wa maisha, mtu wa kukupa faraja na upendo wa kudumu.
Hata hivyo, picha halisi ndani ya nyumba nyingi ni tofauti.
Wapo wanaume na wanawake ambao, licha ya kuwa kwenye ndoa, kulala katika kitanda kimoja au hata kula pamoja, bado wanahisi upweke.
Lakini, je, inawezekanaje mtu awe ndani ya ndoa na bado ahisi kana kwamba yuko pekee yake?
Hizi hapa masuala ambayo yanaweza kukufanya uhisi upweke licha ya kuwa kwenye ndoa:
-
Mawasiliano yaliyokufa
Upweke ndani ya ndoa mara nyingi huanza pale mazungumzo yanapogeuzwa kuwa fupi mno kama habari kama vile
“Utanunua mkate?”
“Umefua?”
“Umemchukua mtoto?”
Mshauri wa masuala ya ndoa na familia, Teresia Watetu, anasema wanandoa wengi wanazoea kuishi kama ndugu na dada badala ya marafiki.
“Hakuna mazungumzo ya kina. Hakuna kuulizana ‘Uko aje?’ Wote wanaona aibu au wanachoka kuulizana mambo kama hayo,” anasema.
-
Kukosa kuthaminiwa
Upendo sio tu kusema “Nakupenda”; ni kuhisi kwamba mpenzi wako anakutambua, anakusikiza na anathamini mchango wako.
Kwa wengi, hisia za kutotambuliwa hujenga ukuta mkubwa wa upweke. Wengine hufanya kila kitu nyumbani—kutunza watoto, kazi, kulea—lakini bado hakuna shukurani.
“Unapokosa kuonekana, hata uwe umeolewa, unaweza kuhisi uko peke yako duniani,” anasema Watetu.
-
Mitazamo tofauti
Kuwa na mitazamo tofauti kuhusu masuala kadhaa sio mbaya ila isiposhughulikiwa ipasavyo, basi mmoja atahisi kana kwamba hasikizwi.
-
Kulemewa na kazi au majukumu
Katika ndoa nyingi za sasa, wanandoa hutoka asubuhi na kurejea usiku wakiwa wamechoka. Hata wakiwa pamoja, akili zao ziko kazini, kwenye simu, au kukimbizana na watoto.
Haya ndiyo mazingira yanayozalisha upweke wa kimya kimya—uko na mtu kimwili, lakini kiakili na kihisia yuko mbali sana.
-
Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii
Katika dunia ya leo, simu imekuwa mshindani mkubwa wa mapenzi.
“Ushawahi kumuona mtu amekaa na mume wake lakini kila mmoja amezamia kwenye TikTok au WhatsApp? Huo ni upweke wa kisasa.”
Hii anasema huaribu sana uhusiano na ndoa.
-
Magonjwa na msongo wa mawazo
Watu wengine huhisi upweke kutokana na msongo wa mawazo, huzuni au majeraha ya zamani. Mara nyingi hizi ni changamoto wanazobeba kimoyomoyo bila kumshirikisha mwenzake, hivyo hisia za upweke huzidi.