Makala

Wakazi Mai Mahiu waiomba serikali iwape maji safi

October 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Maji ni uhai na raslimali muhimu maishani yenye manufaa chungu nzima kwa binadamu, wanyama na pia mimea.

Ni raslimali ambayo kwa wakazi katika eneo la Gishungu, Mai Mahiu, lililoko Kaunti ya Kiambu, kilomita chache kutoka mpaka wa Nakuru na Kiambu inaendelea kuadimika.

Kwa muda mrefu, wakazi hao wanasema wamekuwa wakitegemea maji ya chumvi kutokana na visima na vidimbwi walivyochimba, na ambavyo raslimali hiyo huisha wakati wa kiangazi.

Kulingana na Gedion Macharia, kuwepo kwa maji safi eneo hilo ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu. “Maji safi, ya kunywa na kufanya mapishi huyateka msimu wa mvua na mito ya muda ambayo mikondo yake inatoka katika milima iliyo karibu kama vile Longonot,” mkazi huyo akaambia Taifa Leo.

Huku eneo hilo likiwa maarufu katika uvunaji wa changarawe, kokoto na mawe ya ujenzi, shughuli wanazozitegemea kujipa mapato, kilimo kinaendeshwa na wenye vyanzo vya maji.

“Udongo wa huku ni wenye rutuba kukuza vitunguu (vya mviringo na majani), nyanya na pia mboga aina mbalimbali, ila wanaolima hutegemea maji ya chumvi. Ndiyo yayo hayo huyanywa na kunywesha mifugo,” mkazi mwingine akasema, akihimiza serikali ya kaunti na pia serikali kuu kuwazindulia miradi ya maji safi.

“Huwa tunahangaika sana. Ni gharama kununua maji ya chupa, ya kunywa. Tunachoomba, serikali ituzindulie miradi ya maji safi kutoka maeneo ya milimani,” akasema mkazi huyo, kauli yake ikipigwa jeki na Bw Macharia.

Eneo hilo li kilomita chache mno kutoka ulipo mradi wa reli ya kisasa, SGR, unaounganisha jiji la Nairobi na Thika, na kulingana na wenyeji tuliozungumza nao, wanahoji ikiwa serikali ina uwezo kufanikisha kuwepo kwa garimoshi la kisasa, si kibarua kuwazindulia miradi ya maji safi.

Isitoshe, eneo hilo lina udongo wenye rutuba kuzalisha vitunguu, nyanya na mboga aina tofauti, na wanasema kuwepo kwa maji kutaimarisha shughuli za kilimo, liingie kwenye daftari la maeneo kapu la uzalishaji chakula nchini.

“Kizingiti humu ni uhaba wa maji. Si ajabu tukipata maji ya kutosha, liwe tajika katika kilimo na ufugaji,” akasema mkazi aliyejitambua kama Bw Nicholas.