Wakazi wakumbwa na hofu Chinkororo wakifufuka katika mazishi ya Opore
KATIKA eneo la Gusii, hasa Kaunti za Kisii na Nyamira, kutajwa kwa Chinkororo kunaibua taswira ya vijana shupavu, wenye nguvu na wepesi walio tayari kwa mapigano wakati wowote jamii inapokuwa hatarini.
Miongoni mwa Abagusii, Chinkororo ni wanamgambo ambao walikuwa wakitokea wakati wowote vurugu za kikabila zilipotokea kwenye mpaka wa pamoja na Wakipsigi, Wamasai na wakati mwingine Wajaluo.
Ingawa kikundi hicho kilipigwa marufuku na serikali kwa madai ya kujihusisha na uhalifu, kikundi hicho huibuka tena Kisii mara kwa mara, kulingana hali ya kisiasa au matukio yanayowahitaji.
Mnamo Novemba 9, kundi la wanachama wa kundi hilo lilizua hofu wakati wa mazishi ya mbunge wa zamani wa Bonchari Zebedeo Opore katika kijiji cha Nyamiobo huko Kisii Kusini, kilomita chache kutoka mpaka wa Abagusii na Wajaluo huko Asumbi.
Kwa muda, sherehe ya mazishi iligeuzwa kuwa ukumbi wa vituko baada ya genge hilo kufika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu, ambaye walidai ni baba na wafadhili wao.
‘Sisi ni Chinkororo na tumekuja’
“Sisi ni Chinkororo na tumekuja hapa kutoa heshima zetu za mwisho kwa mtu ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi waliofadhili shughuli zetu za awali,” alisema msemaji wa kundi hilo, aliyejitambulisha kama Keraka Oyondi.
Wakiwa wamevalia shuka nyekundu za Kimasai na wakiwa wamejihami kwa marungu na fimbo ndefu, wanamgambo hao walifanya vituko mbele ya waombolezaji wakitoa sauti za vita kana kwamba walikuwa wakishindana na maadui zao.
Walikuwa na nywele zilizopakwa rangi nyekundu, na kuruka juu na chini kama Morani wa Kimasai wakitaka kupigana.
“Miongoni mwetu hapa kuna wataalamu, kama walimu na wataalam wengine wanaohudumia jamii yetu katika nyadhifa tofauti. Marehemu Opore na wabunge wengine wa awali kutoka Gusii walitufadhili,” alisema Keraka.
Aliwataja waliokuwa wabunge na mawaziri wakiwemo na Simeon Nyachae na Henry Obwocha (wote marehemu), akisema waliwanunulia sare walizokuwa wamevaa.
Marehemu Opore alichangia pesa
“Marehemu (Opore) alituchangia pesa na sare ambazo unaweza kuona tumevaa,” alisema Keraka.
Keraka alisema wabunge hao wa zamani pia walishawishi kuajiriwa kwa wanachama wao serikalini. Alidai viongozi wa Kisii wamesaidia wanachama wa Chinkororo kupata ajira katika huduma ya polisi, ualimu na sekta ya matibabu
Vyanzo vya habari katika eneo hilo vililiambia Taifa Leo kuwa genge hilo lilisafirishwa kutoka eneo la Ramasha eneo la Nyaribari Masaba na dhamira yao ilikuwa ni kuweka ulinzi katika mazishi hayo.
Kuwepo kwao kulizua hofu kwa sababu mazishi hayo yalitarajiwa kuwa ya wasiwasi baada ya mahakama ya Kisii kuamuru kwamba mwanamke mmoja aliyedai kuzaa watoto na Opore aruhusiwe kuhudhuria mazishi hayo chini ya ulinzi wa polisi.
Hili lilikuwa jambo la kustaajabisha kwa sababu maafisa rasmi wa usalama walikuwepo chini ya amri ya Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kisii Charles Kases.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi kutoka kanda hiyo— akiwemo mbunge wa sasa, Dkt Charles Onchoke, Gavana Simba Arati, Seneta Richard Onyonka, Seneta Mteule Essy Okenyuri, wabunge Obadiah Baringo (Bomachoge Borabu), Steve Mogaka (Mugirango Magharibi) na viongozi wengine kutoka Kisii na Nyamira.
Kuvamiwa na wanamgambo hao
Chanzo cha habari kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuhofia kuvamiwa na wanamgambo hao, kilisema wananchi wa kijiji hicho walishangaa mwenyekiti wa kamati ya mazishi alipotangaza kuwepo kwa Chinkororo, na kusema waruhusiwe kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
“Ingawa kulikuwa na kutoelewana katika familia kuhusu kukubali mwanamke aliyeibuka na watoto, akidai kuwa ni mke wa Opore, hatukutarajia Chinkororo waje hapa kama walivyofanya,” kilisema chanzo hicho.
Miongoni mwa Abagusii, Chinkororo (umoja Enkororo) hapo awali walikuwa “jeshi” la kikabila linaloheshimika ambalo hulinda jamii dhidi ya uchokozi kutoka nje.
Hata hivyo, mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, baadhi ya wanasiasa wa Kisii waligeuza kundi hilo kuwa wahalifu na wanamgambo wa kisiasa, ambao walichanganya vikosi na genge linguine lililopigwa marufuku, “Amachuma” ili kuwatisha wapinzani wao wa kisiasa.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA