Wakenya waanza mwaka wakiona giza bila matumaini
WAKENYA wameanza mwaka wa 2025, wakiwa kwenye giza kuhusu nchi yao itakavyokuwa kufuatia hali na matukio ya 2024.
Wengi, hasa vijana ambao waliandamana kupinga serikali wanahisi kuwa wingu jeusi la ukiukaji wa haki za binadamu litaendelea mwaka huu kwa kuwa serikali haijaonyesha nia ya kuheshimu utawala wa sheria.
Maandamano ya vijana yaliangazia changamoto zinazokumba Kenya huku serikali ikijaribu kuongeza mapato kutoka kwa raia wanaokabiliana na gharama ya juu ya maisha na wana hasira kuhusu ufisadi na kile wanachokiona kama majaribio ya kuzima upinzani.
Mwaka unaopoanza, serikali ya Rais William Ruto na sehemu kubwa ya vijana bado wanatofautiana kuhusu mwelekeo ambao nchi inafuata.
Rais Ruto anasisitiza kuwa serikali yake imeweka msingi wa mageuzi ya kiuchumi akitaja mpango wa nyumba za bei nafuu, Bima ya Afya ya Jamii, Mbolea ya Ruzuku, Kushuka kwa bei za mafuta na viwango vya ubadilishaji shilingi kwa dola, Muundo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu na ajira nje ya nchi kama baadhi ya mafanikio.
Hata hivyo, Serikali yake imeshinikiza mipango yake mikuu ambayo yote imepingwa kortini kwa kukosa kushirikisha umma kikamilifu.
zigo la ushuru
Kutoridhika kwa Wakenya kulikozuka mwezi Juni mwaka jana baada ya Bunge kupitisha mswada ambao ungeongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa za chakula na sekta nyinginezo katika uchumi kunatazamiwa kuendelea mwaka huu kukichochewa na kile raia wanachochukulia kuwa ukiukaji wa haki za raia na ukosefu wa usalama unaoendelezwa na maafisa wa usalama.
Kulingana na mashirika ya haki za binadamu, serikali haijachukua hatua zozote za kurekebisha hali zinazokumba raia na haonekani kujali huku wanasiasa wakuu wakiungana dhidi ya vijana.
Wakenya hawana ajira hawana matumaini kwa kuwa wawekezaji wanahepa Kenya na hawajui watakakopata karo ya watoto wao. Wanaishi kwa hofu ya kutekwa wakikosoa serikali.
“Mwajiri wangu alifunga biashara Kenya mwaka jana akilalamilia gharama ya juu ya uendeshaji. Sijui nitatoa wapi karo ya watoto wangu wawili walio sekondari,” aeleza Susan Abura ambaye ni mjane.
Wachambuzi wa siasa wanasema hali ya kisiasa, sera za serikali zinazokandamiza raia na mazingira yasiyovutia wawekezaji yanafanya raia kufungua mwaka wakiwa kwa giza.
“Wanasiasa wakuu kutoka mirengo yote ya kisiasa wameungana serikalini huku vijana wakiendelea kulalamikia mateso. Katika hali kama hii hatutarajii mabadiliko yoyote mwaka huu,” akasema Bw Simon Kiruki, mwanaharakati.
Kero ya utekaji nyara
Licha ya Rais kuleta kuleta washirika wa waliokuwa mahasimu wake katika uchaguzi mkuu wa 2022 Raila Odinga na Uhuru Kenyatta katika serikali jumuishi, vijana wameendelea kutekwa nyara huku 10 wakitekwa nyara na watu wasiojulikana katika wiki chache zilizopita. Polisi wamekanusha kuwa maafisa wao walihusika na utekaji nyara huo.
Akizungumza katika Kaunti ya Homa Bay siku ya Ijumaa, Rais Ruto alisema serikali yake itakomesha dhuluma dhidi ya vijana ishara kwamba anafahamu kinachotendeka na wahusika.
“Hawa watoto ni baraka tulizopewa, kila mzazi atunze watoto wake, sisi serikali tutafanya wajibu wetu, tutamaliza utekaji ili vijana wa Kenya waishi kwa amani,” alisema.
Mwanaharakati Boniface Mwangi anasema vijana wa Kenya wameungana dhidi ya wasomi wa kisiasa ambao wamefanya maisha kuwa magumu kwao.
“Gen Z walikuja pamoja, wakaungana na walikuwa na lengo moja la kuukataa mswada wa sheria ya fedha jambo ambalo lilifanikiwa na wakaenda mbali zaidi kudai mageuzi ya kisiasa na mabadiliko ya baraza la mawaziri na mengine yakatokea na hivyo kulazimisha vigogo wa kisiasa Uhuru Kenyatta, Raila Odinga na Ruto katika kambi moja,” akasema.
‘Tulianza mwaka tukiwa watu waliogawanyika na tunafunga mwaka na serikali yenye msingi mpana. Tumeleta Wakenya wengi pamoja,’ alisema Ruto.
Kuzima upinzani
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hii imeundwa ili kuzima upinzani dhidi ya utawala wake.
‘Inasikitisha kwamba walio madarakani wanachukulia kama hakuna kinachotokea, lakini ukweli ni kwamba hali ni mbaya na mwaka huu sidhani kutakuwa na mabadiliko hasa baada ya Rais Ruto kuvutia waliokuwa wapinzani wake wakuu upande wake. Tabaka la zamani la kisiasa, ikiwa ni pamoja na Rais William Ruto na Raila Odinga wameungana na hawaonekani kujali,” asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Wadadisi wa kisiasa wanatabiri makabiliano zaidi na hali ya haki za binadamu kudorora zaidi iwapo Rais Ruto ataendelea kushikilia msimamo wake na kuendeleza sera ambazo zinakasirisha raia.
“Anacholenga kiongozi wa nchi ni kuhakikisha atashinda muhula wa pili katika uchaguzi wa mwaka wa 2027 na akiwa na vigogo wa kisiasa wa jamii na maeneo anaoamini watamsaidia kwa hilo, hajali kitakachowapata Wakenya,” asema.