Makala

Wakenya wabuni mbinu kukabili gharama ya juu, baada ya kubaini afueni haiji

Na PETER MBURU February 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDADI kubwa ya Wakenya sasa wanawapeleka watoto wao katika shule za bei nafuu, kuhamia nyumba za bei nafuu na kubadili matumizi yao ya pesa kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Utafiti mpya uliofanywa na kampuni ya huduma za kifedha ya Old Mutual, unaonyesha kuwa angalau asilimia 26 ya Wakenya waliohojiwa walihamia nyumba za bei nafuu mwaka jana, asilimia 21 wanatumia bidhaa za bei nafuu na asilimia 19 waliwahamisha watoto wao na kuwapeleka katika shule za bei nafuu.

Kando na hayo, utafiti huo pia ulifichua kuwa asilimia 18 ya Wakenya sasa wanatumia simu na data za bei nafuu.

Hizi ni baadhi tu ya mbinu za kukabiliana na gharama ya juu ya maisha.

“Baadhi ya Wakenya sasa wanawahamisha watoto wao na kuwapeleka katika shule ambazo karo ni ya chini ikilinganishwa na mwaka uliopita,” Utafiti huo wa Old Mutual Financial Services Monitor ulisema.

Baadhi ya Wakenya walionyesha kuwa wanafuata bajeti na kuweka rekodi za gharama zote za nyumbani.

Mitindo ya maisha kama vile kula nyumbani na kupunguza matumizi ya wikendi pia imekuwa kawaida miongoni mwa Wakenya.

Mabadiliko ya mtindo wa maisha ili kukabiliana na gharama ya juu ya maisha yamewasukuma wengi kuzingatia bajeti.

“Baadhi wamepunguza bima ya matibabu ili kukidhi mahitaji yao ya kifedha,” utafiti huo uliongeza.

Inabainisha kuwa mwaka wa 2024 Wakenya wengi au asilimia tano hawakuwa na bima yoyote ya matibabu.

Hili lilikuwa ni ongezeko kutoka asilimia moja tu ya Wakenya ambao walichukua hatua kama hiyo mwaka wa 2023.

Utafiti huo unabainisha kuwa Wakenya wengi sasa wanatafuta njia mbadala ya kuongeza mapato yao ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku nyumbani.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa wengi wanachukua hatua kama hiyo kwani pesa wanazopata wanazitumia zote katika mahitaji ya nyumbani.

Utafiti huo ulibainisha kuwa miongoni mwa wanawake, asilimia 24 hawana pesa zozote mwishoni mwa mwezi, huku asilimia 19 ya wanaume wakifanya kazi ngumu mradi tu wapate pesa za kujitegemea huku ikibainishwa kuwa ni asilimia tatu tu kati ya 10 wanaobaki na pesa mwisho wa mwezi baada ya kugharamia kila kitu nyumbani.

Utafiti huo pia unabainisha kuwa kwa asilimia 37 ya Wakenya waliohojiwa, walisema wana usalama wa kifedha na wana pesa za kutosha kushughulikia masuala ya dharura.