Makala

Wakenya walia ‘Lipa Mdogo Mdogo’ imewageuza mateka

Na MISHI GONGO September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HALI ngumu ya maisha nchini imewasukuma Wakenya wengi kugeukia mipango ya ‘lipa mdogo mdogo’, katika kununua bidhaa mbalimbali.

Bidhaa kama vile fanicha, vyombo vya kielektroniki na hata ardhi sasa zinapatikana kwa lipa mdogo mdogo.

Ijapokuwa wafanyabiashara wengi wamekumbatia mfumo huu wa ulipaji kwa awamu ili kuwawezesha wateja wao ambao hawana uwezo wa kulipa pesa taslimu, wateja sasa wanalia kudhulumiwa.

Baadhi ya waathiriwa wanasema mpango huo unatumika kama mtego wa kibiashara unaowaacha maskini wakihangaika bila msaada.

Bi Lynder Otieno, mhitimu wa chuo kikuu, alikumbwa na hali hii baada ya kununua simu akilipa Sh3,000 kama malipo ya kwanza na Sh80 kila siku kwa muda wa miaka miwili.

“Nilipomaliza deni, simu ikazima kabisa. Nilijaribu kuwasiliana na kampuni lakini nikakosa msaada. Nilikuwa nimelipa karibu Sh50,000 kwa simu ya Sh11,000,” alisema Bi Otieno.

Kisa chake ni mfano tu wa kile ambacho maelfu ya Wakenya ambao wananunua simu, pikipiki, fanicha na hata mashamba wanapitia katika mpango huo.

Bi Ruth Musasya pia alipitia changamoto kama hiyo.

“Nilikuwa nalipa Sh65 kila siku lakini salio halikuisha. Nikitaka taarifa ya malipo waliniambia nifuate ofisi ya Nyali bila kutoa maelezo ya wazi,” alisema.

Kwa upande wake, Bw Denis Omondi, mhudumu wa bodaboda mjini Mombasa, alichukua pikipiki kwa mpango wa lipa mdogo mdogo.

Alilipa Sh33,000 kama malipo ya mwanzo kisha akakubaliana kulipa Sh3,032 kila wiki.

“Nilipokuwa karibu kumaliza deni, walidai ‘tracker’ ya pikipiki imeharibika. Kisha siku moja msaidizi wangu alipata pikipiki haipo pale alipokuwa ameegesha. Nilipojaribu kufuatilia, hakuna hatua ilichukuliwa,” alisema.

Baada ya kutishia kuwashtaki, kampuni ilimuarifu kutembelea afisi iliyo karibu naye kuchukua pikipiki iliyokuwa imetumika.

Hata hivyo, baada ya kufika katika afisi hiyo, walimueleza hawana maagizo ya kumpa pikipiki mpya. Alielekezwa afanye maombi mapya.

Kamanda wa Polisi wa Mombasa Urban, Bw Lucas Chelulot, alisema wengi wa waathiriwa ni watu wa mapato ya chini.

“Wanashawishiwa bila kuelewa masharti. Lakini hadi sasa hakuna aliyeleta malalamiko rasmi,” alisema.

Hata hivyo, sio kila mtu anayelalamika. Bi Bahati Mwakoi ambaye ni mfanyabiashara, alisema wateja wake hutumia mpango huu kununua mavazi ghali kupitia vyama vyao.

“Wanachama huchanga na kila wiki mmoja anapata bidhaa. Imewasaidia wengi,” alisema. Lakini baadhi ya wafanyabiashara wanahofia mpango huo.

“Nauona kama mzigo kwa wateja na hatari kwetu tukikosa kulipwa. Nakuza biashara kwa kuuza taslimu pekee,” Bw Abdulhakim Hamid alisema.

Bi Lilian Atieno alisema mpango wa lipa mdogo mdogo unaonyesha ugumu wa maisha kwa Wakenya wengi.

“Shida ni kuwa hakuna udhibiti wa riba na masharti ya kifedha. Wateja wako hatarini kuporwa,” alisema.

Benki Kuu ya Kenya tayari imeonya kuhusu ongezeko la mikataba isiyo rasmi inayowakandamiza wananchi.

Lakini kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, wengi bado wanakimbilia mpango huu kwa matumaini ya kupata bidhaa walizokuwa hawawezi kuzimudu.