Makala

Wakenya walia waliona mwili wa Raila ‘view once mode’

Na CECIL ODONGO October 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wamelalamikia kasi ambayo walilazimishwa kutazama mwili wa Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye alizikwa Jumapili Kang’o ka Jaramogi, Kaunti ya Siaya.

Bw Odinga alifariki mnamo Jumatano wiki jana na kuletwa nyumbani Alhamisi ambapo alipokelewa na umati mkubwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa JKIA.

Siku hiyo, mwili wa Raila uliratibiwa ungetazamwa majengo ya Bunge lakini mwishowe kutokana na umati mkubwa, ukapelekwa hadi Kasarani.

Baada ya ghasia uwanjani humo ambapo polisi walitumia vitoza machozi, hatimaye vigogo wakiongozwa na Rais William Ruto walitazama mwili wa baba.

Hata hivyo, kwa sababu usiku ulikuwa unaingia na umati ulikuwa mkubwa, ilibidi kila aliyekaribia jeneza kuharakishwa kiasi kuwa baadhi walikuwa hata hawauoni mwili vizuri, wengine wakipita hata bila kutazama.

Mnamo Ijumaa katika uwanja wa Nyayo, tena Wakenya walipata nafasi ya kutazama mwili wa mwendazake baada ya ibada ya kumuenzi kuandaliwa na kuhudhuriwa na Rais William Ruto na viongozi wa kimataifa.

Kuanzia saa saba, Wakenya walitazama mwili huo lakini tena waliofika mbele ya jeneza waliharakishwa kiasi kuwa hawakuwa wakitoa heshima zao vizuri jinsi inavyohitajika katika tamaduni za Afrika.

Hali ilikuwa hiyo hiyo Jumamosi uwanjani Jomo Kenyatta Mamboleo jijini Kisumu kisha baadaye jioni Opoda Farm nyumbani kwa Bw Odinga.

Tukio la kuharakishwa na maafisa wa usalama mbele ya jeneza liliibuliwa jina ‘view once’ mitandaoni wengi wakikashifu vyombo vya usalama na kusema wangepewa muda wa kutosha kumuaga Raila.

“Hivi ndivyo mnawafanya raia wautazame mwili wa Raila Odinga. Wanajeshi wa KDF hamfanyi vizuri,” akaandika MC Adek tatu kwenye ukurasa wake wa Facebook.

“Mambo yamekuwa mengi kiasi kuwa wananchi wanaona Raila Odinga only view once mode (mfumo wa kutazama picha mara moja kisha inafutika yenyewe),” akaandika Nick Koech Tinget.

Kutokana na enzi hizi za utandawazi ambapo wengi hupenda kupiga ‘selfie’, hilo halikuwezekana kutokana na kasi ambapo waliokuwa wakitazama mwili walikimbizwa.

Kando na majeraha, wengine hata walitokwa na viatu na kulazimika kutembea miguu mitupu kwa sababu hakukuwa na hata nafasi ya kurudi nyuma.

Baadhi ya Wakenya walifanyia mzaha masaibu ya wenzao mbele ya jeneza na kukosa kwao kuona vizuri mwili wa Raila.

“Watu 20 walikuwa wakitazama mwili kwa sekunde 2. Lala salama baba,” akaandika Jiri Jirie mtandaoni.

“Nasikia ulipokuwa ukitazama, akili ikishika tu hivyo, unapigwa kofi unasahau umeutazama mwili wa Baba,” akaandika Shanny Mac.