Wakenya walivyojipata katika jeshi la Urusi bila idhini yao
Tafuta kwenye mitandao maneno kama “Waafrika wanaopigana kwa niaba ya Urusi” au “Waafrika waliokamatwa na jeshi la Ukraine” na utapata mamia ya matokeo.
Katika vichwa vya habari hivi, kuna muundo wa kusikitisha unaojitokeza: vijana wa Afrika wanaovutwa na ahadi za ajira zenye mishahara minono au ufadhili wa masomo, lakini wanaishia kushiriki vita wasivyokuwa wamejiandaa.
Fursa ambazo hapo awali zilionekana kuwa halali — ajira ya kulipwa vizuri, masomo ya bure, nafasi ya kuishi nje ya nchi — hubadilika na kuwa madhila, mateso na hatari ya maisha.
Katika enzi ya kidijitali, fursa zinaonekana nyingi. Ukitafuta “ajira nchini Urusi” au “ufadhili wa masomo Urusi,” utakutana na matokeo mengi yanayokuahidi maisha bora.
Hivi majuzi, jeshi la Ukraine lilitoa video ya mwanariadha Mkenya, Evans Kibet, mwenye umri wa miaka 36, aliyejisalimisha kwa wanajeshi wa Kyiv baada ya kutumwa mstari wa mbele na jeshi la Urusi.
Alinaswa na kikosi cha 57 cha wanamaji wa Ukraine huko Kharkiv Oblast, karibu na mji wa Vovchansk.
Katika mahojiano ya video baada ya kukamatwa, Evans alieleza kuwa aliingia Urusi kama mtalii, lakini baadaye alidanganywa na mtu aliyempokea hadi akajikuta katika jeshi la Urusi.
“Sijawahi kuwa mwanajeshi, wala sikuwahi kutamani kazi ya kijeshi. Nilikuja Urusi kama mtalii kwa wiki mbili. Siku moja kabla ya kurudi, mtu aliyenipokea aliniuliza kama napenda Urusi. Nilimwambia napenda, akaniuliza kama nataka kubaki nikasema ndiyo, lakini visa yangu ilikuwa imeisha muda wake,” alisema.
Mtu huyo aliahidi kumsaidia kurefusha visa yake na akampa nyaraka za Kirusi atie saini, ambazo baadaye aligundua ni mkataba wa kujiunga na jeshi. Baada ya kusaini, pasipoti na simu yake zilichukuliwa na hapo maisha yake yakageuka.
“Waliokuja kunichukua walikuwa watu tofauti. Tulisafiri kwa saa saba hadi kambi ya kijeshi. Waliniambia: ‘Umetia saini, hauwezi rudi. Ni ujiunge ama uuawe,’” alisema Evans.
Kwa mujibu wa gazeti la The Independent, kati ya wanafunzi 35,000 hadi 37,000 wa Afrika wanasoma Urusi kupitia mipango mbalimbali ya ufadhili wa masomo.
Mnamo Mei 2024, mamlaka za India ziliwakamata watu wanne waliodaiwa kutumia fursa za masomo na ajira kuwanasa watu wanaotafuta maisha bora ili kuwapeleka mstari wa mbele wa vita kwa niaba ya Urusi.
Mwaka mmoja baadaye, serikali ya Togo ilitoa tahadhari kwa wananchi wake kuhusu matangazo ya ufadhili wa masomo na kazi nchini Urusi, baada ya ripoti ya mtu mmoja kudai kupelekwa mstari wa mbele badala ya chuo alichoahidiwa.
Matangazo kama hayo pia yameshuhudiwa hapa Kenya, ambapo mnamo Juni 2024, Wizara ya Elimu ilitangaza nafasi za ufadhili wa masomo nchini Urusi lakini hakuna ushahidi kuwa Wakenya wamepelekwa vitani kupitia mpango huo.
Ripoti ya Mei 2025 ya shirika la Global Initiative Against Transnational Organized Crimes (GIATOC) ilionyesha maelfu ya wanawake kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi, Afrika Kusini, Ethiopia na Zambia wakifanya kazi hatari kwenye viwanda vya kutengeneza silaha Urusi.
Zaidi ya wanawake 200 kutoka Afrika Mashariki na Magharibi wameripotiwa kutumiwa kutengeneza silaha na ndege zisizo na rubani kwa ajili ya vita.
Wanavutiwa na matangazo ya mitandaoni yanayoahidi tiketi za ndege za bure, pesa taslimu, na makazi ya bure. Masharti ya kuingia ni rahisi — kama kucheza mchezo wa kompyuta au kujibu maswali ya Kirusi — lakini wanajikuta kwenye mazingira magumu, wakiwa hawana njia ya kutoka.
Ripoti iitwayo Who is Making Russia’s Drones? inaangazia kituo kikuu kinachoitwa Alabuga Special Economic Zone (SEZ) katika mkoa wa Tatarstan, ambacho kinatumia wanafunzi wa kigeni (hasa wanawake wa miaka 18–22 kutoka Afrika, Amerika ya Kusini, Asia Kusini na nchi za zamani za Muungano wa Kisovieti) kama nguvu kazi.
Ripoti hiyo yasema wanawake huchaguliwa zaidi kwa kuwa ni “rahisi kudhibiti” kuliko wanaume.
Mohamed Hussein, mwenye umri wa miaka 29 kutoka Somalia, alieleza kuwa alidanganywa na marafiki waliomwahidi mshahara wa $2,000 kwa mwezi na malipo ya awali ya $2 milioni. Baada ya kukubali, alipelekwa karibu na mstari wa mbele. “Sio kwamba napenda vita, lakini mimi ni baba. Nataka watoto wangu wale, wasome, waishi bila hofu,” alisema Mohamed akiwa kwenye kambi ya mateka wa vita Ukraine.
Richard Mensah, raia kutoka Ghana mwenye miaka 37 na baba wa watoto wawili, alikamatwa siku ya kwanza tu baada ya kuwasili. Alikuwa amevutiwa na ahadi za ajira, akaomba visa ya Urusi na kupata kwa haraka. “Sikujua kuna vita. Nilifikiri nakwenda kufanya kazi tofauti nikaambiwa nisaini mkataba kwa Kirusi,” alieleza akiwa kwenye kambi ya wafungwa wa vita nchini Ukraine.
Katika kambi hizo, waandishi walikutana na raia wa Somalia, Ghana, Misri, Sierra Leone, Togo, Afrika Kusini, Cuba na Sri Lanka — wote waliodanganywa kwa njia tofauti lakini wakajikuta kwenye vita wasiokuwa wamejiandaa.