Makala

Wakenya wamtaka Raila ‘awanie’ kumrithi Papa Francis

Na CECIL ODONGO April 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wameendelea kumshinikiza Kinara wa Upinzani Raila Odinga ajitose rasmi kwenye kinyang’anyiro cha upapa licha ya kuwa si Mkatoliki au Kadinali.

Baada ya Papa Francis kuaga dunia mnamo Jumatatu asubuhi, wengi wamekuwa wakipendekeza Bw Odinga kwa wadhifa huo licha ya kwamba kivyovyote vile hawezi kuwa Papa.

Mitandaoni picha zinazomwonyesha Raila akiwa amevalia nguo za Papa zimekuwa zikienea kila mahali tangu Jumatatu ihali waziri huyo mkuu wa zamani ni muumini wa Kanisa la Kianglikana nchini.

Mnamo Julai 2020, Raila alibatizwa na mhubiri tata Mchungaji Dkt David Owuor wa Kanisa la The Ministry of Repentance and Holiness.

Pia kuwa Papa lazima kadinali awe hajafikisha umri wa miaka 80 na Raila ashafika 80 wala si kadinali na hawezi kushiriki kura ya kumchagua Papa mpya.

Kejeli hizo zinatokana na hali kwamba Bw Odinga amekuwa akiwania ‘kila kitu’ na kubwagwa. Raila aliwania uchaguzi mkuu mnamo 2022 na akashindwa na Rais William Ruto.

Kwenye chaguzi za 2013 na 2017 alilambishwa sakafu na Rais Uhuru Kenyatta (amestaafu) kushindwa huku kukimwaandama 2007 mikononi mwa marehemu Mwai Kibaki kisha 1997 akabwagwa na marehemu Daniel Arap Moi.

Mnamo Februari 2025, Raila alibwagwa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja ya Afrika (AUC) na Mahmoud Ali Youssef raia wa Djibouti.

Kwenye kejeli ya mitandaoni, baadhi ya Wakenya waliunga ‘azma’ ya Raila kumrithi Papa Francis huku wengine wakipinga wakisema bado tu atashindwa.

“Hata Mungu hawezi kubali,” akaandika Manpower kwenye video ya Raila iliyoandamana na nyimbo za kikatoliki kwenye Tiktok

“Halafu tena ashindwe na Muislamu,” akaandika Chris Ochola.

Wengine walisema Raila hushindwa katika kila kinyang’anyiro na wakauliza atakata rufaa wapi kwa sababu kwenye kura ya Papa, hamna mwanya wa rufaa.

“Huyu atakula sadaka na fungu la kumi,” akaandika Dennis Omwega akionekana kurejelea imani kuwa Raila alijiunga na utawala wa Rais Ruto ili kunufaikia jasho la Gen Z walioandamana mwaka jana.

“Wacha mzee ajaribu hii tena labda bahati yake iko hapa,” akaandika mwingine.

Juhudi za Mbunge wa Kimilili Didmus Baraza za kuwataka Wakenya wamheshimu Raila hazikufua dafu kwani naye alilengwa na kila aina jibu mitandaoni.

“Mheshimiwa Raila Odinga ni mwanasiasa nguli nchini na anastahili kuheshimiwa. Kusambazwa kwa picha zinazomwonyesha akiwa amevalia nguo za baba ni ukosefu wa heshima sio kwake tu bali kwa Kanisa Katoliki na Ukristo kwa jumla,” akaandika Bw Barasa kwenye ukurusa wake wa Facebook.