Makala

Wakenya wapunguza furaha, kulikoni?

March 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

KENYA imeshuka katika orodha ya mataifa yenye kiwango cha juu zaidi cha furaha kote duniani.

Hayo ni kulingana na ripoti kuhusu Hali ya Furaha Duniani 2024, iliyotolewa Jumatatu.

Kwenye ripoti hiyo, Kenya iliorodheshwa katika nafasi ya 114 kipindi cha 2021-2023 kati ya mataifa 193 kote duniani.

Hata hivyo, nafasi hiyo ni mpomoko, ikilinganishwa na ripoti iliyotolewa mwaka 2023, ambapo Kenya iliorodheshwa katika nafasi ya 111 kipindi cha 2020-2022.

Mwaka 2022 Kenya ilikuwa katika nafasi ya 119.

Ripoti iliyaorodhesha mataifa hayo kwa kuzingatia masuala sita, ambayo ni: imani katika uthabiti wa kiuchumi wa nchi, usaidizi katika masuala ya kijamii, matarajio ya maisha mema, uhuru wa kufanya maamuzi ya kimaisha, ukarimu na dhana kuhusu ufisadi.

Kijumla, kiwango cha furaha nchini ni 4.47, ikilinganishwa na Finland, iliyoibuka bora, kwani kiwango chake cha furaha ni 7.471.

Hata hivyo, Kenya iliibuka bora ikilinganishwa na majirani wake kama Uganda na Tanzania, ambayo kiwango chake cha furaha ni 4.372 na 3.781 mtawalia. Uganda iliorodheshwa katika nafasi ya 117 huku Tanzania ikiorodheshwa katika nafasi ya 131.

Orodha hiyo ilitayarishwa kutoka kwa maelezo katika mashirika ya Gallup World Poll na Gallup/Meta State of Social Connections.

Ripoti hiyo hutolewa kila mwaka, na huwa inatokana na majibu yanayotolewa na watu 1,000 katika kila nchi kuhusu masuala tofauti yanayolihusu taifa lao.

Mataifa kumi bora yenye kiwango cha juu cha furaha duniani ni: Finland, Denmark, Iceland, Uswidi, Israeli, Uholanzi, Norway, Luxembourg na Uswisi.

Mataifa yenye kiwango cha chini zaidi cha furaha ni: Afghanistan, Lebanon, Lesotho, Sierra Leone na Congo, Zimbabwe, Botswana, Malawi, eSwatini, Zambia, Yemen na visiwa vya Comoros.

Ripoti hiyo inatolewa ikiwa tayari aliyekuwa gavana wa Meru Kiraitu Murungi amebuni ‘tiba’ kwa mahangaiko wanayopitia watu wengi.

Bw Murungi anasisitiza kuwa lazima Wakenya waanze kukumbatia furaha na kicheko kama njia ya kufuta mahangaiko hayo.

Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Furaha, ambayo huadhimishwa Machi 20, Bw Murungi aliongoza shughuli za uzinduzi wa Furaha Kenya Club.

“Wakati umefika tuanze kukita maisha yetu katika masuala ya furaha, upendo na kicheko. Tunaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Furaha ili kujikumbusha kuhusu furaha na umuhimu wa furaha katika maisha yetu; na muhimu zaidi, duniani kote,” akasema Bw Murungi wakati huo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria (KSL), Prof Patrick Lumumba, alisema kuwa licha ya changamoto nyingi ambazo Wakenya wanapitia, wanafaa kutafuta na kubuni njia za kupata furaha.

Alitoa wito kwa Wakenya na Waafrika kwa ujumla kukumbatia uadhimishaji wa Siku ya Kimataifa ya Furaha, akisema watapata maana halisi ya kuishi.

“Si wengi wanaojua kwamba mnamo Juni 28, 2012, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilipitisha Machi 20 kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Furaha. Inasikitisha kuwa siku hii haisherehekewi kwa mbwembwe zinazofaa,” akasema Prof Lumumba.

Kuzinduliwa kwa Furaha Kenya Club kulijiri baada ya Bw Murungi kusema mwaka 2023 kwamba alikuwa amekamilisha shahada ya digrii kutoka kwa Taasisi ya Mafunzo ya Furaha na kufuzu.

“Nina furaha kutangaza kwamba nimemaliza shahada ya digrii ya mwaka mmoja ya mafunzo ya furaha kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Furaha na kufuzu. Kwa sasa, nina ujuzi wa kutosha kuendesha mwamko mpya wa furaha katika nchi yangu,” akasema mnamo Novemba 2023.

Siku ya Kimataifa ya Furaha ilirasimishwa na Umoja wa Mataifa (UN) mnamo 2012 na huadhimishwa kila Machi 20.