Makala

Wakili wa Ruto ICC, wengine 14 wateuliwa majaji wa Mahakama ya Rufaa

Na RICHARD MUNGUTI January 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MMOJA wa mawakili waliomtetea Rais William Ruto katika kesi aliyoshtakiwa ICC baada ya ghasia za 2007 /2008 zilizopelekea watu zaidi ya 1,000 kuuawa na wengine zaidi ya 600,000 kuhamishwa makwao ni miongoni mwa watu 15 walioteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Bw Katwa Kigeni alichaguliwa pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka Ahmed Issack Hassan.

Wengine ambao waliteuliwa na tume ya kuajiri wafanyakazi wa mahakama JSC ni pamoja na jaji mwenye tajriba ya juu Chacha Mwita, jaji na mkufunzi hodari wa masuala sheria katika baadhi ya vyuo vikuu Munyao Sila na Jaji Mathew Nduma Nderi ambaye amebobea katika masuala ya sheria za ajira.

JSC pia iliwateua, Jaji Hedwiq Ong’udi, Jaji Linet Ndolo (wa mahakama ya ajira ELRC), Jaji Lucy Mwihaki Njuguna, Jaji Samson Okong’o (kutoka kitengo cha kesi za mazingira na mashamba), Jaji Rachel Ng’etich na Jaji Stephen Radido (kutoka ELRC)

Pia wakili mwenye tajriba ya juu Paul Lilan, aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha wanasheria nchini (LSK) John Okoth Okello, Brown Murungi Kairaria na Jaji Byram Ongaya (kutoka mahakama ya ELRC).

Majina ya wateule hawa yamepelekewa Rais Ruto atakayewaapisha.

“Tume ya JSC imekamilisha zoezi la kuwateua majaji wa mahakama ya rufaa na imeyapeleka majina kwa Rais Ruto kuwaapisha,” taarifa iliyotolewa na Jaji Mkuu Martha Koome ilisema.

Rais Ruto atawaapisha majaji hawa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa katika Kifungu nambari 166 cha Katiba.

Majaji hao waliteuliwa baada ya kuhojiwa na JSC.

Zoezi la kuwahoji ilipeperushwa moja kwa moja kutoka afisi za JSC.