WAKILISHA: Rais wa shule yake anayekuza demokrasia
IMEKUWEPO mijadala mingi kuhusiana na ukuzaji wa demokrasia humu nchini Kenya na hata bara zima la Afrika.
Wachanganuzi wengi wa masuala ya kisiasa na uongozi wamedai kuwa njia ya pekee ya kuwa na kizazi kitakachothamini demokrasia siku zijazo ni kuibuka na mafunzo maalumu kuhusu mbinu za kukuza demokrasia katika taasisi za elimu.
Kutokana na hayo, shule nyingi zimeweza kuwachagua viongozi wao kidemokrasia.
Pinkette Wanjiru, 14, ni mwanafunzi wa Darasa la Nane katika Shule ya Msingi ya KBA Maziwa, Kahawa West.
Wanjiru ni binti wa kwanza wa Bw Peter Mwangi na Bi Esther Maruga.
Pinkette maarufu ‘Pinky’ ndiye Rais wa shule yake.
Nyota huyu hakuficha furaha yake kuchaguliwa na hatimaye kuwa kiongozi wa ngazi ya juu sana katika shule yake.
“Nafurahia sana kuwa rais wa shule yangu. Pia nawashukuru sana wanafunzi wenzangu kwa kunichagua,” alisema Pink.
Kwake yeye, uongozi hutoka kwa Mungu.
Binadamu hutumika tu kutimiza lile ambalo Mwenyezi Mungu ashasema.
“Mtu anafaa kuonyesha dalili za uongozi angali katika shule ya msingi. Hicho ni kama kipawa. Shule zinafaa kuvipalilia vipawa hivyo kwani ni Mungu hupeana,” anasema.
Baada ya kuchaguliwa na kuapishwa kama rais wa shule yake, chipukizi huyu aliapa kutimiza yote aliyowaahidi wafuasi wake.
Anasikitika kuona kuwa kila wakati uchaguzi unapofanyika katika nchi yoyote barani Afrika, lazima wananchi wa taifa hilo wamwage damu.
Anasema kwamba yuko tayari kuwa kielelezo cha uongozi bora na kuwa balozi wa kuhubiri demokrasia na manufaa yake kwa wanafunzi wenzake.
“Viongozi wanawake kama Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani na Dilma Rousseff, Rais wa thelathini na sita wa Brazil wamekuwa vielelezo kwangu,” akasema.
Kulingana naye, shule yake iliwapa wanafunzi wote fursa ya kuwania viti mbalimbali kwanzia kwa Rais wa shule, naibu wake, Waziri wa Michezo shuleni, Waziri wa Elimu na Waziri anayeshughulikia Maslahi ya Wanafunzi shuleni.
Licha ya kupewa nafasi ya kufanya kampeni bila kuwekewa vikwazo wala vizuizi vyovyote na shule, Wanjiru anakiri kwamba ilikuwa ni jambo ghali mno licha ya kupata ufadhili.
“Shule ilifadhili kampeni zetu kwa asilimia kubwa sana. Niliunda mabango mengi mno. Manifesto pia niliunda na isitoshe, nilikuwa na timu ya nguvu sana iliyouza sera zangu vyema,” alieleza.
Kiongozi huyu anasema kwamba alichaguliwa kwa kura nyingi sana bila kutoa hongo yoyote kwa wanafunzi.
“Shule iliweka sheria moja kali mno. Yeyote angepatikana au kusikika kuwa amewashawishi wenzake kwa kuwapa hela ama kuwanunulia mkate hangeruhusiwa kushiriki uchaguzi. Hongo ya aina yoyote haikuruhusiwa,” alisema.
Anafichua kwamba uchaguzi ulipomalizika, wapinzani wake walimpongeza na hata kuahidi kumuunga mkono katika majukumu yake. “Baada ya kuchaguliwa, wapinzani wangu walikubali matokeo na kuahidi kuniunga mkono,” alifichua.
Anakiri kwamba kuwa rais wa shule si jambo rahisi.
“Changamoto si haba. Kwanza kabisa ni kutimiza yale niliyowaahidi wafuasi wangu. Pia kuweza kusawazisha uongozi na masomo si kazi rahisi,” alisema.
Pinky anaipongeza shule yake kwa kuendeleza demokrasia kwani anaamini kwamba kupitia kwa uchaguzi, viongozi wema wenye maadili huchaguliwa.
Isitoshe anawashukuru wazazi na walimu wake kwa kumpa motisha.
“Mwalimu Reagan na Madam Peris wamekuwa kiungo muhimu sana katika uongozi wangu shuleni. Mara kwa mara mimi hutafuta ushauri wao,” alikiri.
Pia hakusita kuwapongeza marafiki zake Shumi, Peris na Brigit kwa wema wao na ushauri wao kwake.
Masomoni, nyota huyu hafanyi ajizi. Yeye angependa kuwa rubani.
“Kila wakati nikiona ndege angani, huwa najiambia rubani wa ndege hiyo ni mimi. Na taaluma ambayo ningependa kusomea ni urubani,” alisema.
Chipukizi huyu anawashauri wanafunzi wenzake kuchangamkia uongozi wangali katika shule za msingi ili kuweza kujiboresha na kujifahamisha na uongozi mapema.