Makala

WAKILISHA: Vichekesho vinamlisha

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

VIDEO zake zimekuwa zikisambaa mtandaoni kutokana na jinsi zinavyowavunja mbavu wengi.

Licha ya kuwepo kwa katika jukwaa hili kwa miezi mitatu pekee, Wanyoike Nyururu, 26, anazidi kujiundia jina miongoni mwa machale wanaotambulika sana nchini.

Kuanzia kwa mhubiri msumbufu kwenye matatu, hadi muuzaji dawa za kuua wadudu barabarani, Coconut kama anavyofahamika jukwaani amefanikiwa kunasa macho ya wengi kupitia ucheshi wake huku akitumia masuala na maisha halisi kupitisha ujumbe wake.

Hii ndio imekuwa siri ya kunasa mawazo ya mashabiki wengi.

“Kwa mfano, hebu fikiria kuangusha kichekesho kuhusu kile kipande cha nguo unachotumia kuoga? Bila shaka kila mtu atacheka anapokumbuka kitambaa hicho kinachoning’inia nyuma ya mlango wa bafu,” asema.

Kwa kawaida yeye hurekodi video fupi ambazo huchukua muda wa kati ya dakika moja na dakika tatu.

“Naweza unda video moja kwa siku lakini nimekata kauli kuunda kati ya video mbili na tatu kwa wiki, ambayo ni sawa na kati ya video nane na 12 kwa mwezi. Hii ni mbinu ya kunipa muda wa kuimarisha ubunifu,” aeleza.

Ucheshi wake Coconut ambaye amesomea masuala ya kurekodi filamu na uzalishaji vipindi vya redio chuoni, umemfanya kupata mialiko katika shoo mbalimbali za televisheni ikiwa ni pamoja na Churchill Show.

“Nilifanya shoo mbili katika kipindi hiki ambapo vichekesho vyangu vilipokelewa vyema na mashabiki,” aeleza.

Sio to kwenye shoo hizi ambapo ameweza kunasa macho ya wengi, hata kwenye mitandao ya kijamii, kazi zake zinazidi kupokelewa vyema.

“Unaweza kupata video zangu kwenye mitandao ya YouTube, Instagram, Twitter na Facebook, zote kwa jina @Coconutkenya,” aongeza.

Ni kazi ambayo imemsaidia kujitegemea kimapato na hata kutoa nafasi ya ajira kwa vijana wengine. “Sina kazi nyingine na video hizi ndo riziki yangu.

Wanyoike Nyururu, 26. Picha/ Maktaba

Nafurahia kwani nimejiajiri. Aidha, nina watu sita wanaofanya kazi chini yangu ikiwa ni pamoja na mhudumu mmoja wa masuala ya ubunifu, ambaye huandaa masuala yote kabla shughuli ya kurekodi kuanza. Pia, nina wana vichekesho watano chipukizi ambao kwa sasa nawalea,” aeleza.

Kipaji chake cha ucheshi kilijitokeza kwa mara ya kwanza akiwa chuoni.

“Kazi yangu ilianza kuonekana chuoni ambapo mwaka wa 2015 nilibahatika kupata mwaliko wa kuonyesha vichekesho vyangu kwenye televisheni,” aeleza.

Hapa alionekana sio tu na wasanii, bali pia mashirika kadha ambayo yalianza kumsaka.

“Kuna kampuni zilizonijia na kunitaka nijumuishe kikosi chao cha ubunifu, vile vile niwe mwandishi wa vichekesho. Ni hapa nilimua kuanza kufanya miradi yangu,” aeleza.

Kulingana naye, jitihada zake zimepigwa jeki na baadhi ya wasanii maarufu nchini ikiwa ni pamoja na Dr King’ori, Butita, Terence, Jalas, Chipukeezy na Kabi Wa Jesus miongoni wa wengine.

“Wamenipa mwangaza na kunifanya nionekane kana kwamba nimekuwepo kwa muda mrefu ilhali ni miezi mitatu pekee,” aongeza.

Kwa sasa anasema hana mipango ya kufanya majaribio katika shoo nyingine yoyote, na badala yake anataka kumakinika na kujiundia kitambulisho chake kitakachokuwa na uwezo wa kuuza bidhaa au huduma yoyote katika soko hili lenye ushindani mkubwa.

“Nimekuwa nikipata ofa nyingi lakini nmezikataa. Ningekuwa naunda kati ya Sh80,000 na laki moja kwa kila mteja yaani angalau laki tatu kwa mwezi, lakini sitaki kwa sasa kwani nataka kumakinika na shughuli za kufanya kitambulisho changu kuwa thabiti kwa imani kwamba pesa zitafuata baadaye,” asema.