Akili MaliMakala

Wakulima Kiambu wanavyopata mazao tele kupitia mpango wa pembejeo

Na SAMMY WAWERU January 14th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KWA miaka mingi, wakazi wa Ndeiya, Kaunti ya Kiambu, wamekuwa wakitegemea misaada ya chakula kutoka kwa serikali kuu, serikali ya kaunti, na wahisani.

Ni hali ambayo imekuwa ikishuhudiwa eneo la Ndeiya, Limuru, Ngoliba, Gatuanyaga, na Thika Magharibi, ambapo wakazi wamekuwa wakikumbwa na misururu ya baa la njaa kutokana na ukosefu wa pembejeo bora za kilimo na hali ya hewa isiyotabirika.

Hata hivyo, kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, hali hii imebadilika pakubwa.

Wakazi wameanza kupata mavuno ya kuridhisha kufuatia mpango wa Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi, wa kusambaza pembejeo za bure, zikiwemo mbolea na mbegu za mahindi yanayostahimili athari za tabianchi – kiangazi.

Esther Wariara akionyesha mahindi aliyozalisha kutoka shambani mwake Kiambu. Picha|Sammy Waweru

Wamenufaika kupitia mpango huo wa Gavana Wamatangi uliokuwa sehemu ya ahadi zake za kampeni chini ya ajenda ya “Farm Input Subsidy Program”, ambao umefikia zaidi ya wakulima 600,000.

Kila msimu wa upanzi, wakulima hupokea mbegu za mahindi kulingana na kiwango cha shamba wanachomiliki, pamoja na fatalaiza kuboresha mimea na mazao.

Mary Wanjiku, mkazi wa Thigio, Wadi ya Ndeiya, Limuru, ni miongoni mwa waliofaidika.

Akiwa na shamba lenye ukubwa wa nusu ekari, amepokea pembejeo hizo angalau mara nne ndani ya miaka miwili na nusu.

Mama huyu wa watoto watatu anasema awali alihangaika kupata mbegu bora zinazostahimili ukame katika eneo lake, ambapo ugali na githeri ndicho chakula kinachoenziwa.

Esther Wariara Ng’ang’a akivuna mahindi kwenye shamba lake Kiambu. Picha|Sammy Waweru

Kabla ya mpango huo wa Gavana Wamatangi, anadokeza kwamba alikuwa akinunua madebe mawili ya mahindi kutoka sokoni kwa ajili ya kupanda, bila kutumia mbolea. Mavuno yake yalikuwa hafifu — yasiyozidi gunia moja la kilo 90.

“Tangu Gavana aanzishe mpango huu, sina wasiwasi tena kuhusu kupata mbegu faafu na mbolea. Hutangaziwa kupitia gari lenye kipaza sauti kwamba gavana atatembelea eneo fulani kugawa pembejeo. Wakulima kutoka maeneo ya karibu hukusanyika, maafisa wa kilimo wanathibitisha majina, na kila mtu anapewa pakiti ya mbegu na mbolea. Gavana mwenyewe huhakikisha kila mmoja anapata haki yake. Sikuwahi kushuhudia jambo kama hilo awali,” anasema Wanjiku.

Anaongeza: “Tangu nianze kupata pembejeo hizi, sijawahi kukosa chakula nyumbani. Wakati mwingine hata huuza mazao yangu.”

Kwa upande wake Gavana Wamatangi, anasema lengo la usambazaji wa pembejeo za bure ni kukabiliana na uhaba wa chakula na kupunguza gharama ya bidhaa za kimsingi. Anabainisha kuwa mpango huo unalenga hasa wakulima wadogo (wale wa mashamba madogo) na unafadhiliwa kikamilifu na Serikali ya Kaunti ya Kiambu.

Chini ya mradi wa ufadhili wa pembejeo unaoendeshwa na Gavana Kimani Wamatangi, wakulima Kiambu wameandikisha kiwango cha mazao kuongezeka. Picha|Sammy Waweru

“Baadhi ya viongozi hawajaelewa kwa nini tumeweka mkazo katika kugawa mbegu na mbolea. Wakulima wakipata mavuno mazuri, hawahangaiki tena kuhusu bei ya unga — wanapeleka tu mahindi yao kusagwa,” anaelezea Wamatangi.

Anasema ni kwa sababu hiyo, kwa miaka miwili na nusu iliyopita Kiambu haijaandikisha visa vya watu kupelekewa chakula cha misaada.

Margaret Wangari kutoka eneo la Githunguri, anasema serikali ya kaunti huhakikisha wakulima wanapata mbegu na mbolea kabla ya mvua kuanza. “Kwa sasa, ninavuna mazao niliyopanda mwanzoni mwa mwaka huu, na tayari nina mbegu kwa msimu ujao,” anasema.

Ni mpango wa kuboresha sekta ya kilimo Kiambu ambao mkulima David Wathika Ngigi anakiri kiwango cha mazao kimeongezeka mara dufu.

“Kwa mfano, sehemu iliyokuwa ikizalisha maguno matano sasa mavuno yamekuwa mara dufu,” Wathika akaambia Akilimali.

Mkulima huyo wa Githunguri, pia, ni mfugaji wa samaki.

Kabla ya usambazaji wa pembejeo za kilimo, Serikali ya Kaunti ya Kiambu kupitia idara ya kilimo ilifanya utafiti kubaini mbegu na mbolea zinazohitajika katika maeneno lengwa.

Margaret Wangari mkulima wa mahindi Kaunti ya Kiambu. Picha|Sammy Waweru