Makala

Wakulima Nyandarua wanavyokimbiza mavuno yao kwa ‘benki ya chakula’ kuepuka hasara

Na FRIDAH OKACHI December 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKULIMA zaidi ya 600 katika Kaunti ya Nyandarua wanakumbatia mpango wa benki ya Chakula ‘Food Bank Kenya’ (FBK) ili kutatua hasara inayotokana na mavuno kukosa soko na kuharibikia shambani.

FBK huchukua mazao ya ziada kutoka kwa wakulima ambao hushindwa kutafuta soko na kuwalipa kabla ya kusambaza jijini Nairobi kwa jamii zilizo na mapato ya chini.

Mpango huo, umewezesha FBK kuweka konteina kubwa katika kaunti hiyo ambayo hukusanya chakula hicho.

Konteina la kuhifadhi chakula hicho limewekwa karibu na kituo cha polisi. Kila siku malori yakichukua chakula hicho na kusambazwa katika sehemu mbalimbali jijini Nairobi.

Bw Benson Kagai ambaye ni mwanachama wa kundi hilo, alisema awali alipata hasara kutokana na nusu ya mazao yake kutupwa kwa kukosa soko.

“Karibu nusu ya matunda na mboga ninazozalisha mashambani haziliwi wala kufika sokoni kwa wakati unaofaa. Hali hiyo ilinisababishia kupata hasara,” alisema Bw Kagai.

Bw Kagai ambaye ni mkulima wa karoti, mchicha, sukuma wiki, na viazi, mara kwa mara huchangia chakula cha ziada na kuuzia FBK.

“Baada ya kujiunga na FBK, huwa napata wageni mara kwa mara ambao hunitembelea wakiwa na vikapu vya kuvuna mazao hayo kutoka shambani,” alisema Kigai.

Benson Kagai ambaye husambaza mazao zaidi kwa FBK kabla ya kuharibikia shambani. Picha|Fridah Okachi

Hata hivyo, Kagai anasikitika kwamba wakulima wengi katika eneo hilo hupanda zao moja, jambo linalosababisha ukosefu wa soko la ndani.

“Sisi sote hulima mazao yale yale kwa sababu ya asili ya udongo wetu. Baadaye tunakosa soko la kuuza, na hivyo kupata hasara baada ya mavuno. Njia ya FBK angalau inatusaidia kupata fedha kidogo za kununua mazao mengine muhimu,” Kagai aliongeza.

Kagai alijiunga na FBK mwaka wa 2021, alitaja ushirikiano na wakulima wengine umezaa matunda kwani kiwango cha upotevu wa chakula kimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Kando na pesa, FBK pia hutupatia mbegu za kupanda kwa msimu unaofuata. Tuna bahati na hali ya hewa hapa, tunaweza kulima mwaka mzima bila matatizo makubwa, jambo linalotufanya tuwe na chakula muda wote,” alisema wakati wa mahojiano.

FBK inajaribu kulisha takriban asilimia 36.5 ya Wakenya wanaokabiliwa na uhaba wa chakula kwa kutumia ziada inayotolewa na wakulima.

Mwanzilishi Mwenza na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa FBK Moses Nyoro, alisema mpango huo pia unasaidia kupunguza utoaji wa gesi ya methane kwa kutumia teknolojia ya Food Verse, inayofuatilia kiasi cha kaboni kinachookolewa chakula kinapookolewa.

Bw Nyoro anakiri changamoto za ukosefu wa sera kuhusu usambazaji wa chakula na uhamasishaji wa wakulima zaidi kujiunga na mpango huo.

“Kwa usaidizi wa GFB, FBK hununua malori tisa ya kusambaza chakula, hatua inayowezesha kuwafikia wahitaji zaidi.”