Makala

Wakulima wahimizwa kujiunga na mitandao ili kupata soko la mazao kwa urahisi

June 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KILIMO ni tegemeo kubwa nchini Kenya na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hii ni kutokana na hali bora ya hewa pamoja na maeneo mengi yenye udongo wenye rutuba.

Ni sekta ambayo inategemewa pakubwa hasa katika kulisha taifa, wakulima kupata mapato pamoja na serikali kuingiza ushuru.

Aidha, zaraa imebuni nafasi nyingi za ajira kupitia wakulima wanaoikumbatia, viwanda vinavyoongeza thamani katika mazao na hata kuajiri wafanyakazi mashambani na katika viwanda hivyo.

Kimsingi, ukulima unasaidia kuimarisha na kustawisha uchumi.

Licha ya tija tele zinazotokana na uzalishaji wa mazao, wakulima wamekuwa wakipitia changomoto za hapa na pale. Ukosefu wa soko na bei duni, ndicho kikwazo kikuu kwa wakulima.

Ni wengi ambao mazao yao yameishia kuuzwa kwa bei duni, kwa sababu ya soko kudorora. Kutia chumvi kwenye kidonda kinachouguza, hili pia limechochewa na kuwepo kwa mawakala.

Mawakala wanatuhumiwa kunyanyasa wakulima kwa kununua mazao kwa bei duni, licha ya kuwa wao ni daraja kati ya mkulima na wanunuzi.

Ni katika visa vingi wamelaumiwa kuyauza kwa zaidi ya faida ya asilimia 100, ikizingatiwa wameyanunua kwa bei ya chini.

Ili kukwepa changamoto za aina hiyo, wakulima wanashauriwa kujiunga na mitandao ya kijamii hasa Facebook.

Kufuatia kuimarika kwa teknolojia mpya, wanunuzi wamegeukia mitandao kutafuta mazao.

“Ni hatua ambayo imerahisishia wafanyabiashara kupata mazao ili yamfikie mlaji,” anasema Bw Dennis Njenga afisa msimamizi wa mauzo na soko, e-Farmers Africa, kampuni yahuduma za kidijitali zinazolenga wakulima.

Njenga anasema wakulima wakiitikia kuenda na nyakati za teknolojia, itakuwa rahisi kukabili kero la mawakala na kuweza kupata wanunuzi wa moja kwa moja.

Kwa mfano, katika mtandao wa Facebook kuna makundi kadha wa kadha yaliyofunguliwa na kuleta pamoja wakulima kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Ni katika hilo ambapo wakulima wanahimizwa kuchapisha mazao yao, pamoja na kupakia picha za mavuno.

“Wafanyabiashara wamefurika mitandaoni wakitafuta bidhaa, wakulima watapata soko la moja kwa moja la mazao yao wakiikumbatia,” asema Bw Njenga.

Hata hivyo, unashauriwa kuwa makini kwani kuna wachangiaji matapeli kwenye mitandao ya kijamii. Kabla kusafirisha mazao sokoni, hakikisha kuna mikakati salama ili kuepuka kuhadaiwa.

Bw Njenga alitoa wosia huo, wakati akizungumzia wakulima wa eneo la Karii, kaunti ya Kirinyaga, wiki hii katika hafla ya uhamasishaji wa kilimo bora iliyoandaliwa na H.M Clause, kampuni inayounda mbegu za nyanya, mboga, matikitimaji na pilipili mboga.

Eunice Kaseo, mkulima, aliibua suala la kuwepo kwa mbegu bandia sokoni akilalamika kwamba limechangia kwa mazao duni na ya hadhi ya chini.

“Tunashauri kampuni za kuunda mbegu ziangazie jambo hili. Kuwepo kwa mbegu bandia kunatuhangaisha kama wakulima,” alisema Bi Eunice.

Bi Emmah Wanjiru, mtaalamu na afisa H.M Clause alisema mbali na mbegu, kuna fatalaiza na dawa za magonjwa na wadudu zisizoafikia ubora wa bidhaa nchini.

Mdau huyu anawataka wakulima kuwa makini, akiwahimiza kununua pembejeo kutoka kwa kampuni na maduka yaliyoidhinishwa.

“Unapaswa kukagua mbegu, dawa na fatalaiza unayonunua iwapo ina stempu ya halmashauri ya kutathmini ubora wa bidhaa nchini (Kebs). Ni muhimu kukukumbusha kuwa katika mitandao kampuni na mashirika mengi, hutoa mafunzo mahususi ya mbinu bora za kilimo,” akasema Bi Wanjiru.

Mdau huyu pia anahimiza wakulima kukumbatia utumizi wa mitandao kusoma habari za wakulima waliobobea na kufanikisha kilimo, kwani vyombo vya habari kama vile magazeti na mitandao hupakia hadithi zao.

 

Katika picha iliyo hapo juu, Bi Eunice Kaseo, mmoja wa wakulima Kirinyaga akieleza kuhusu vikwazo vya pembejeo. Picha/ Sammy Waweru