Makala

Wakuu wa kanisa la PCEA wasukumwa jela

Na RICHARD MUNGUTI December 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wawili wakuu wa kanisa la PCEA wamesukumwa jela kwa kukaidi agizo la mahakama katika ibada iliyohudhuriwa na Rais William Ruto mnamo Aprili 2024.

Jaji Stellah Mutuku alimwadhibu Katibu Mkuu wa Presbyterian Church of East Africa (PCEA) Rev. Dr. Patrick Waihenya na Modareta Rev. Patrick Thegu Mutahi kwa kumtawaza David Nderitu Ndumo kuwa mweka hazina mkuu wa dhehebu hilo kinyume cha maagizo ya mahakama asitawazwe kwa vile alikuwa anakabiliwa na kesi ya mkopo Sh7.4milioni aliothaminiwa na watu 15.

Jaji Mutuku alisema madai dhidi ya Nderitu kwamba alikaidi Katiba ya Kanisa la PCEA na pia agizo la mahakama yalithibitishwa.

Akipitisha hukumu Jaji Mutuku alisema lazima maagizo ya mahakama yafuatwe na kila mmoja.

“Hii mahakama imewapata na hatia na itawahukumu iwe funzo kwa watu wengine wanaodharau amri za mahakama,” Jaji Mutuku alisema.

Wawili hao walishtakiwa na  Bw Benjamin Njoroge Mburu, mshirika wa PCEA aliyelalamika kwamba maafisa hao wawili wakuu wa kanisa walikaidi na kudharau maagizo ya mahakama kwa kumtawaza Ndumo ilhali mahakama ilikuwa imezima zoezi hilo.

Katika uamuzi wake Jaji Mutuku alisema Waihenya na Mutahi

Walijua kuna amri ya mahakama wasiendeleze zoezi la kumtawaza Ndumo kuwa mweka hazina wa kanisa hilo.

“Nimeridhika kwamba agizo la hii mahakama lililotolewa Aprili 8,2024 ilikaidiwa na kuvunjwa,” jaji huyo aliamua.

Mahakama ilitupilia mbali tetezi wa wafungwa hao wawili kwamba hawakukabidhiwa kwa njia nzuri maagizo hayo ya mahakama.

Walidai walitumiwa ujumbe katika mtandao wa Whatsapp na ujumbe mwingine kwa email.

Jaji huyo alisema upeperushaji wa maagizo kwa mtandao wa Whatsapp na email unakubalika kisheria.

Jaji huyo pia alisema kuna ushahidi wa video uliotolewa wakati wa mkutano mkuu wa kanisa hilo ambapo maagizo hayo ya korti kupinga kutawazwa kwa Ndumo yalijadiliwa.

Hata hivyo mahakama ilisema mkutano uliendelea licha ya kujulishwa zoezi hilo la kumtawaza Ndumo lilikuwa limesitishwa na Mahakama Kuu.

“Nimeridhika kabisa washtakiwa waliendelea na zoezi la kumtawaza Ndumo huku wakijua mahakama imepiga marufuku zoezi hilo,” Jaji Mutukua alisema.

Mahakama ilikataa ushahidi kwamba washtakiwa waliomba msamaha akisema “bado Ndumo ameendelea kuhudumu kama mweka hazina wa kanisa hilo.”

Mzozo wa uteuzi wa Ndumo unatokana na madai kwamba uteuzi wake unakumbwa na dosari kufuatia madai amesakama na madeni.

Mahakama ilielezwa Ndumo amekaidi kulipa mkopo wa Sh7.4m na kwamba jopo la Benki ya Cooperative imesema hajalipa pesa alizokopa kwa Sheria Sacco.

Baada ya kuthibitisha kwamba washtakiwa wamepatikana na hatia aliagiza Dkt Waihenya ambaye ndiye Katibu Mkuu wa PCEA, atumikie kifungo cha mwezi mmoja.

Rev Mutahi naye alihukumiwa kutumika kifungo cha miezi miwili.

Pia Jaji Mutuku alimpa Dkt Waihenya kifungo badala cha kulipa faini ya Sh100,000 naye Rev Mutahi aagizwa alipe faini ya Sh150,000.

Wote wawili waliamriwa walipe faini hizo katika muda wa siku 30 zijazo.