Makala

Walevi wa kuchelewa kurudi nyumbani walawitiwa kwa mitaro

February 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

NDURU hutanda kukiwa na giza na katika mitaro kando ya barabara mbalimbali Kaunti ya Murang’a ambapo walevi wa kiume wanaochelewa kufika nyumbani hulawitiwa na magenge.

Kufuatia hali hiyo, maafisa wa usalama wameonya walevi wawe na nidhamu ya kulewa mapema na kuanza mwendo wa kurejea nyumbani mapema ili wajihakikishie usalama wao.

Hali ni mbaya kiasi kwamba Naibu Mkurugenzi wa huduma za Matibabu wa Kaunti Stephen Ngigi amefichua kwamba hospitali za umma zimewekwa katika tahadhari za kuhudumia waathiriwa.

“Wengi hufika katika hospitali wakiwa na majeraha ya kulawitiwa yakiwemo yale ya mshipa mkuu wa haja kubwa kuning’inia nje,” akasema Dkt Ngigi.

Alisema hali hiyo imetanda katika wadi zote 35 na ni suala la kutamausha.

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Gitonga Murungi aliambia Taifa Leo kwamba “ndiyo sababu tunapambana na ulevi kiholela kwa kuwa mtu anayejielewa hata awe mlevi hawezi akalawitiwa kwa kuwa atakuwa amejipa kinga za kimsingi”.

“Ukilewa kwa nidhamu na uanze mwendo wa kuelekea nyumbani mapema kukiwa na mashahidi barabarani, ni vigumu ukumbane na unyama huo,” akasema Bw Murungi.

Alisema wale wa kulewa kiholela hadi saa tano usiku na kisha saa sita kwenda juu, wanajipata wamelala kwa mitaro wakiwa hoi.

Naibu Kamishna wa Maragua Joshua Okello aliomba walio na mamlaka ya kutoa leseni za baa “watufanyie haki”.

“Watii wito wa Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua wa kupunguza idadi za baa hasa zile za kuuza pombe za bei ya chini,” akasema Bw Okello.

Alisema kutokuwa na utaratibu wa leseni hizo kumeifanya kazi ya utekelezaji sheria kuwa ngumu hasa katika kudhibiti udhalimu dhidi ya walevi.

Alisema ni vigumu kufuatilia safari za walevi gizani hadi wafike nyumbani salama.

Kamanda wa polisi wa Kigumo Kiprono Tanui alisema kwamba “tunazingatia walevi wasio na nidhamu waelewe kwamba kuna shida kubwa na wanaweza wakageuzwa vyombo vya mahaba kinyume na maumbile gizani na kwa mitaro”.

Aliwataka walevi kujihakikishia usalama wao kwa kulewa kiustaarabu na kuchukua tahadhari ya kimsingi ya kuelewa hata janga kuu la kupoteza maisha linaweza likawaandama.

Ujumbe kama huo umetolewa na Kamanda wa polisi wa Ithanga Thomas Mong’are aliyesema kwamba “tutajizatiti kuchunga kila mtu lakini hata nanyi walevi mtusaidie kuweka usalama unaowahusu”.

Alisema atakuwa mdhalimu sana kwa wamiliki wa baa wanaovunja sheria eneo hilo “na pia magweni ya pombe haramu”.

Hata hivyo, alisema “wa kulawitiwa ni uamuzi wake kwa kuwa sisi tutadumisha usalama kwa wote ambao wako tayari kushirikisha harakati hizo kupitia kujiepushia balaa za kuhatarisha maisha yao kimakusudi”.

[email protected]